Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Peter Majule

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wahitimu wa vyuo kutumia vyeti vyao kama dhamana kupata mikopo ya kuanzisha miradi ya uwekezaji?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, nitakuwa maswali mawili ya nyongeza. Vyuo vikuu vingi duniani sasa hivi vinaandaa wahitimu ambao wanaenda kuajiri wengine, yaani wenyewe wanakuwa waajiri ili waajiri wengine; na wameanzisha Career Development Department ambayo kazi yake ni kuwa-groom hawa wawekezaji vijana ili watakapotoka, wafungue miradi mikubwa kuanzisha miradi na kuajiri wengine.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ya nchi yetu ipo tayari sasa kuanza kubaini wawekezaji wakiwa bado wapo chuoni na kuweza kuwapa mikopo mikubwa ili wakafungue miradi mikubwa na kuweza kuajiri wengine?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali itaanza lini sasa huu mpango wa kutumia vyeti kama dhamana, kwani uwekezaji ni kitu kikubwa, na kinahitaji mtaji mkubwa?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ipo tayari kutoa mitaji mikubwa ya kuanzisha na kufanya uwekezaji kwa kutumia vyeti, au watahitaji dhamana nyingine? Ahsante. (Makofi)

Name

Laurent Deogratius Luswetula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Dkt. Neema kwa uwezo wake mkubwa sana wa kuweza kujenga hoja hapa Bungeni. Pia, ninaendelea kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa kutuletea mtu kama huyu hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kwanza ni kweli kabisa Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwawezesha vijana kiuchumi na kujiajiri. Mfano mkubwa ni shilingi bilioni 200 ambazo tayari zimeshatolewa. Pia kupitia asilimia 10 ambazo zinaendelea kutolewa nchi nzima na programu nyingine zinazotoa mikopo kwa vijana kwa riba nafuu kabisa.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu wanakuwa hawana misingi ya kufanya biashara kubwa na uwekezaji mkubwa, lakini pia wanakuwa hawana elimu ya kufanya uwekezaji mkubwa pamoja na sifa zinazoendana na hizo. Kwa maana hiyo, pamoja na mawazo mazuri ambayo sasa wanakuwa nayo hawa vijana wetu wanaomaliza vyuo vikuu, bado misingi hii hawana.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sisi kama Serikali, tunashauri ni lazima tuone mwendelezo wa biashara tangu biashara inapokuwa ndogo mpaka inapofikia kuwa kubwa kufanya investment ya shilingi milioni zaidi ya 600, shilingi milioni 800 na kuendelea. Kwa maana hiyo, sisi tunashauri kwamba vijana hawa pia lazima tuangalie trend ya biashara wanazozifanya na mitaji yao.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kuna biashara za aina nyingi kidogo hapa, kuna biashara ambazo ni ndogo kabisa ambazo tunaziita ni micro business ambazo mtaji wake ni kama zinaanzia shilingi milioni tano ambazo na zenyewe zinaweza kuajiri vijana kuanzia mmoja mpaka wanne.

Mheshimiwa Spika, pia kuna biashara ambazo ni ndogo, small businesses ambazo zenyewe zinaanzia mtaji wa shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 200 ambazo zina uwezo wa kuajiri kuanzia vijana watano mpaka vijana 49. Pia tunazo biashara nyingine ambazo ni hizi za kati ambazo mtaji wake ni kuanzia shilingi milioni 200 mpaka shilingi milioni 800 ambazo zinaweza kuajiri vijana kuanzia 50 mpaka 99.

Mheshimiwa Spika, mwisho, tunao wale wafanyabiashara wakubwa ambao na wenyewe wanaanzia mtaji wa shilingi milioni 800 na zaidi ambao wanaweza wakaajiri watu kuanzia 100 na kuendelea. Kwa maana hiyo, vijana hawa ambao wanatoka vyuo vikuu, hawana misingi mikubwa na elimu ya biashara mpaka kufikia kutoka biashara ndogo kwenda biashara kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kuwahimiza lazima tuone trend ya biashara ya mtu huyu anayetoka chuo kikuu, tumwezeshe kupata elimu ya uwekezaji na namna ya kufanya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunashauri kwamba tutaona trend baada ya kumwezesha sasa kuanza biashara ndogo, micro mpaka large, tuone trend ya biashara inaendaje na baada ya hapo, tuko tayari kuwasaidia vijana ambao sasa trend yao ya biashara watakuwa wanakua kutoka biashara ndogo kwenda biashara kubwa kupitia taasisi zetu za kifedha. Ninaomba kuwasilisha.

Name

Esther Nicholas Matiko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wahitimu wa vyuo kutumia vyeti vyao kama dhamana kupata mikopo ya kuanzisha miradi ya uwekezaji?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninashukuru kwa majibu ambayo Serikali imetoa. Kwa kuwa, tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya 60% ya wahitimu wa vyuo hukosa ajira rasmi na hili ni kundi muhimu sana na kubwa sana kwa jamii, sasa ninataka kujua, Serikali ipo tayari kuanzisha Graduate Credit Guarantee Scheme ambao utakuwa ni mfumo utakaowawezesha wahitimu hawa kutumia taaluma zao na vyeti vyao kama dhamana ili waweze kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara na viwanda vidogo vidogo? (Makofi)

Name

Laurent Deogratius Luswetula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme Waziri Mkuu ameshatoa tamko hapa na amesema kwamba Serikali bado inaendelea kutengeneza taratibu na miongozo hiyo na ikishakamilika, miongozo na kanuni hizo zitaletwa hapa Bungeni kama Muswada, na sisi kama Wabunge tukishaupitisha maana yake itakuwa ni sheria. Vijana hawa ambao wanatoka vyuo vikuu, vyeti vyao vitatumika kama dhamana kupata mitaji na mikopo kutoka kwenye taasisi zetu za kifedha. Ninaomba kuwasilisha.