Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 34 Finance Wizara ya Fedha 409 2026-05-21

Name

Neema Peter Majule

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wahitimu wa vyuo kutumia vyeti vyao kama dhamana kupata mikopo ya kuanzisha miradi ya uwekezaji?

Name

Laurent Deogratius Luswetula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Dkt. Neema Peter Majule, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, benki na taasisi za fedha hutumia aina mbalimbali za dhamana katika utoaji wa mikopo kwa watu binafsi. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura ya 113, dhamana inayotambuliwa kwa kiwango kikubwa ni ile inayohusiana na mali zisizohamishika hususan ardhi na majengo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mali zinazohamishika Serikali ipo katika hatua za mwisho kuandaa sheria ya dhamana kwa mali zinazohamishika yenye lengo la kutambua rasmi mali hizo kama dhamana katika utoaji wa mikopo. Aidha, mali hizo zinazotarajiwa kusajiliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kuimarisha usimamizi, uwazi na ufuatiliaji wake. Miongoni mwa mali zinazopendekezwa kufanyiwa tathmini ni vyeti vya taaluma vya wahitimu wa vyuo, kwa lengo la kuchunguza uwezekano wa kuvifanya vitumike kama dhamana katika upatikanaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuwashauri vijana wanaohitimu vyuo kutumia fursa zilizopo kupitia mifuko na programu mbalimbali zinazosimamiwa na Serikali, mfano mifuko ya vijana ambayo hutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi. Ninaomba kuwasilisha.