Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Mussa Utaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga na kukarabati miundombinu ya Kiwanja cha Ndege - Lindi ili kukidhi haja ya uwekezaji wa mradi wa kuchakata gesi ya LNG?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imeingia mkataba na mkandarasi huyu tarehe 22 Julai, 2024 na sasa yapata miezi 15 bado mkandarasi huyu hajalipwa malipo ya awali jambo ambalo limemfanya ashindwe kuanza kazi, je, ni lini Serikali italipa malipo ya awali kwa mkandarasi huyu ili aweze kutekeleza wajibu wake katika kujenga kiwanja hiki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Serikali tayari imesaini mkataba wa miezi 24 wa utekelezaji wa ujenzi wa kiwanja hiki, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kulieleza Bunge hili kwamba ni kiasi gani cha fedha kimetengwa katika bajeti ya mwaka huu 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa kiwanja hiki cha ndege cha Lindi? Ahsante sana.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mohamed Utaly kwa kufuatilia Uwanja wa Ndege wa Lindi ambao ni muhimu sana na una historia kubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kulitambua hilo, ilishafanya hatua mbalimbali sambamba na kumtafuta mkandarasi, kama ambavyo nimezungumza kwenye jibu la msingi, uwanja huu unajengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 120. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi ambavyo Serikali imebeba kwa uzito mkubwa sana uwanja huu wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, maswali yake mawili yameuliza, lini na kiasi gani kimetengwa? Kutokana na umuhimu wake katika mwaka huu wa fedha, na bajeti iliyopitishwa hapa, Mheshimiwa Waziri baada ya kupokea maelekezo ya viongozi wakuu, tunafanya maboresho ndani ya bajeti yetu.

Mheshimiwa Spika, awali tulitenga shilingi 3,800,000,000 lakini tayari tunatafuta fedha nyingine karibu shilingi 70,000,000,000 ambazo zitakwenda kwenye maeneo manne. Moja, kwa ajili ya kulipa fedha za malipo ya awali kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Mwanza uanze kujengwa kama ambavyo tulisikia wote mjadala unavyoendelea, na pili, ni kwa ajili ya kuhakikisha uwanja wa ndege wa Mtwara ambao tulishapata mkandarasi, na alikuwa hajalipwa fedha za malipo ya awali.

Mheshimiwa Spika, tatu, kuhakikisha uwanja wa ndege wa Lindi ambao tulishapata mkandarasi na hakulipwa fedha za awali na yeye aanze kulipwa mwaka wa fedha unaoanza uanze kujengwa. Nne, kuendeleza kasi ya maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Njombe.

Mheshimiwa Spika, hivyo, ninamsihi Mheshimiwa Utaly atupe nafasi, tukishaanza utekelezaji, kazi hii inakwenda kuanza kama ilivyoahidiwa kwenye kampeni na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.