Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 34 | Works and Transport | Wizara ya Uchukuzi | 408 | 2026-05-21 |
Name
Mohamed Mussa Utaly
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Primary Question
MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga na kukarabati miundombinu ya Kiwanja cha Ndege - Lindi ili kukidhi haja ya uwekezaji wa mradi wa kuchakata gesi ya LNG?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Mussa Utaly, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Lindi ili kukidhi haja ya uwekezaji wa mradi wa kuchakata gesi kuwa kimiminika (LNG) pamoja na kuchechemua shughuli nyinginezo za kiuchumi na kijamii. Aidha, ujenzi wa kiwanja hicho uliahidiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2025. Hivyo, ujenzi wa kiwanja hicho ni kipaumbele cha Wizara yetu na Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, tayari imeshaingia mkataba na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group kwa ajili ya ukarabati na maboresho ya kiwanja hicho cha ndege cha Lindi utakaochukua muda wa miezi 24. Ukarabati huo utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio, maegesho ya ndege pamoja na maegesho ya magari.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/2027. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha ili kuendeleza kiwanja cha ndege cha Lindi pamoja na viwanja vingine vya ndege vya mikoa kulingana na mpango wa uendelezaji wa viwanja vya ndege nchini Tanzania.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved