Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bazilio Kapunda Mbwilo
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Meli za Liemba na Mwongozo zitaanza tena kutoa huduma ndani ya Ziwa Tanganyika?
Supplementary Question 1
MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ili hizi meli ziweze kujiendesha kwa faida, zinahitaji abiria wa kutosha na kivutio kimojawapo cha abiria kutumia meli hizi, ni pamoja na bandari. Sasa bandari mbili zilizoko ndani ya jimbo langu, Bandari ya Kipili na Kabwe, zote zimezama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha bandari hizi zinakuwa nzuri ili zivutie watu wengi zaidi kutumia usafiri huu wa meli?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Watu wengi sana wa mwambao wanafanya biashara na nchi jirani ya Congo na husafirisha mizigo, hasa kwa kutumia maboti ambayo yamesababisha vifo vya mara kwa mara kwa hawa wafanyabiashara. Je, Serikali itaweka ratiba ya walau mara mbili kwa mwezi; moja ya hizo meli iweze kwenda Congo, Mji wa Moba na Kalemie, ili wawe salama zaidi? Ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji na maswali yake ya nyongeza, ambayo ameuliza. La kwanza, ameuliza kuhusiana na upatikanaji wa abiria. Ni kweli, Serikali inatambua kwamba meli hii na nyinginezo ambazo zinajengwa ni kwa ajili ya kusaidia abiria pamoja na mizigo. Kimsingi abiria wapo, na changamoto kubwa, ambayo imeipata nchi yetu kwenye takribani maziwa yote matatu ni kujaa kwa maji.
Mheshimiwa Spika, tayari tupo na mkakati wa muda mfupi ambao tunaendelea nao kupitia TPA. Pamoja na mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba yale maji ambayo yamejaa kwenye Bandari zetu karibu zote kuanzia Kabwe, Kasanga mpaka kule Kigoma zinaweza kuondolewa, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa kwamba, tunalifanyia kazi jambo hilo kwa lengo la kusaidia wananchi wetu ambao baada ya kutokea maji haya, kwa kweli wanashindwa kusafiri kwenye bandari hizo.
Mheshimiwa Spika, hoja yake ya pili, tuichukue kama ni ushauri. Meli itakapokamilika kupitia mpango wa kibiashara, tutatazama, kupitia TASHICO, kuona wapi iende kulingana na uhitaji utakaokuwepo, ikiwa ni pamoja na ushauri wake anaoutoa kwenda kwenye nchi jirani, kupitia Bandari ya Moba, Kalemie, pamoja na maeneo mengine.
Name
Arif Suleiman Premji
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Meli za Liemba na Mwongozo zitaanza tena kutoa huduma ndani ya Ziwa Tanganyika?
Supplementary Question 2
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Spika, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya 2025/2030 imeainisha ujenzi wa meli katika Mkoa wa Mtwara ambayo itatoa huduma kati ya Mtwara na Comoro. Je, ni lini utekelezaji huu utaanza?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Arif kwa swali lake la ziada ambapo anataka kufahamu mpango wa Serikali hii katika kujenga meli kwenye ukanda wa mwambao, pamoja na Wabunge karibu wote wanaopakana na Bahari ya Hindi, wamekuwa wakiuliza maswali haya mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa nijibu kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri mpango wa Serikali. Hatua ya kwanza iliyofanyika ni kutaka kufahamu, je, hali ya biashara na mahitaji katika Bahari ya Hindi ikoje?
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshakamilisha tathmini hiyo na kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kwa bajeti ambayo imepitishwa hapa, tunakwenda kuanza kujenga meli kwa ajili ya kusafirisha abiria pamoja na mizigo kwenye ukanda wa bahari ikiwa ni pamoja na Mtwara, Tanga pamoja na maeneo jirani kama vile Mombasa, Comoro, Sychelles na maeneo mengine kadri itakavyoonekana inafaa.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved