Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariam Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza Mwongozo wa Ajira na Mazingira ya Kazi kwa Watumishi wenye Ulemavu katika Taasisi za Umma?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, na tunaipongeza sana kwa kweli, tumeona jinsi gani wenye ulemavu katika baadhi ya maeneo wanapewa kipaumbele na hata suala zima la miundombinu ya majengo mbalimbali ya Serikali yamezingatia kundi hili maalumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu. Kwa kuwa katika utaratibu wa ajira, hawa wenye ulemavu wanaingia kwenye interview ambazo sasa hivi zimewekwa kwa njia mbalimbali ambazo siyo rahisi sana kumtambua mtu mwenye ulemavu, na huyu hana ulemavu, na ukizingatia ulemavu mwingine unatofautiana, je, Serikali imejipanga vipi sasa katika mfumo wa ajira katika utumishi kuwatambua kundi hili la wenye ulemavu? (Makofi)
Name
Regina Ndege Qwaray
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na muhimu hasa kwa kundi hili la watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka miongozo mbalimbali kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata haki sawa kama watu wengine. Kwa kupitia Serikali yetu, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka miongozo mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanazingatiwa hasa katika mazingira ya ajira.
Mheshimiwa Spika, kwa kupitia hivyo, watu wenye ulemavu wamekuwa wakizingatiwa anapokwenda kwenye usaili, kwanza kupewa usaidizi wa karibu wakati wako kwenye usaili, lakini hata hivyo wamewekewa mazingira rafiki ikiwemo vyumba wanavyoenda kufanyia usaili, vinakuwa rafiki kwao, pia vifaa wanavyotumia kufanyia usaili vinakuwa rafiki kwao, hasa kwa kuzingatia ulemavu wa aina mbalimbali. Kwa hiyo, kwa kutengeneza mazingira hayo, watu hawa wenye ulemavu wamepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, hata kwenye mfumo wa ajira, nafasi kubwa imetolewa kwa watu wenye ulemavu wanaposhiriki katika ushindani wa ajira hizi kama ambavyo sera yetu ya menejimenti na ajira katika utumishi wa umma inavyoelekeza kwamba ajira zote zinatolewa kwa ushindani bila ubaguzi. Hivyo, watu wenye ulemavu wamepewa miongozo kuhakikisha kwamba wanapoingia kwenye usaili, basi na kipaumbele wanapewa watu wenye ulemavu hata pale ambapo wanapopata tu zile alama za kuingilia basi kipaumbele watapewa kwanza wale watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninapenda kumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa mazingira ni rafiki, na yameendelea kuboreshwa siku hadi siku. Vilevile Serikali imeendelea kupitia miongozo ili kuboresha zaidi watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele, lakini waweze kushiriki katika usaili, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved