Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Salehe Mbwana Mhando
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. SALEHE M. MHANDO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madaraja yaliyoharibika katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kilindi ili kurahisisha usafiri?
Supplementary Question 1
MHE. SALEHE M. MHANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zaidi ya miaka minne sasa tangu madaraja kadhaa katika Jimbo la Kilindi kukatika kabisa ikiwemo Daraja la Negero, Daraja la Vunila, Daraja la Tamota, Daraja la Kwamfyomi, Daraja la Sambu na Daraja la Makelele. Hali hii imeleta changamoto kubwa sana hasa kwa wagonjwa kwa kipindi chote hicho, lakini zaidi mama zetu wajawazito ambao siwezi kuelezea kwa undani kupitia Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za dharura katika kuhakikisha kwamba inakwenda kuwawezesha TARURA kuweza kurejesha huduma za usafirishaji katika maeneo hayo niliyoyataja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kutokana na bajeti ndogo wanayopata TARURA Wilaya ya Kilindi, na kwa mazingira magumu ambayo nimeyaeleza, Serikali haioni haja sasa ya kuweza kuweka mpango wa kuiongezea bajeti TARURA Wilaya ya Kilindi ili uweze kukabiliana na changamoto kubwa zinazokabili miundombinu ikiwemo madaraja na vivuko katika Jimbo la Kilindi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbwana Mhando Salehe, Mbunge wa Kilindi. Ninafahamu kwamba Jimbo la Kilindi ni moja ya majimbo yenye changamoto za barabara pamoja na madaraja, na Mheshimiwa Mbunge mara kwa mara amewasilisha taarifa za kuhitaji matengenezo hayo. Kwa taarifa njema Mheshimiwa Mhando bajeti ya TARURA kwa Jimbo la Kilindi imeongezeka kwa zaidi ya mara tatu na nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020/2021 bajeti ilikuwa shilingi bilioni moja kwa mwaka, lakini huu mwaka wa fedha 2025/2026 bajeti ya TARURA Kilindi ni takribani shilingi bilioni 3.94.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza Serikali inatambua kwamba tuna uhitaji mkubwa wa kujenga madaraja na barabara ya Kilindi na ndiyo maana bajeti imeongezeka kwa zaidi ya mara tatu. Jambo la muhimu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tumeshafanya tathmini ya madaraja yote yaliyoharibika, na tayari tunaendelea na taratibu za kibajeti kuendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako madaraja ambayo tunaendelea na ujenzi hivi sasa na pia yako madaraja ambayo tunaendelea kuandaa utaratibu wa fedha kwenda kuhakikisha yanajengwa na kurejesha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo litafanyika na bajeti ya Serikali itaendelea kuongezwa kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha ili barabara za Kilindi ziweze kupitika vizuri zaidi.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved