Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zacharia Paulo Issaay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ambao umesimama kwa muda mrefu?
Supplementary Question 1
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, na ninaishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa sasa Serikali imeahidi kukamilisha Mahakama hiyo ya Mbulu ifikapo mwezi Novemba, je, Serikali ina mpango gani wa kuleta samani na vitendea kazi vya kisasa kwenye jengo hilo la Mahakama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa jengo hilo la Mahakama ni la zamani, limechukua miaka mingi na ni chakavu sana na Watumishi wa Mahakama Waandamizi, na Waandamizi wengine hawana majengo ya kuishi, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga makazi ya Watumishi wa Mahakama katika Wilaya ya Mbulu?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay kwa swali lake zuri la ufuatiliaji wa maendeleo katika Mahakama na hasa katika Wilaya ya Mbulu anayotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama kwa wakati huu, kama nilivyojibu, inatekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ambao ni mpango wa miaka mitano, umegharimu mpaka wakati huu jumla ya shilingi bilioni 524.9. Mahakama imekuwa ikifanya maboresho na ujenzi wa katika ngazi mbalimbali ikiwemo katika ngazi ya wilaya. Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ni mnufaika wa mpango huu na ndiyo maana tunatarajia mpaka itakapofika Novemba, 2026 itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upatikanaji wa samani, vitendea kazi na mifumo yote, pindi ujenzi unapokuwa umekamilika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ukamilifu wa jengo hili la Mahakama ya Wilaya ni pamoja na kuwepo na mifumo yote muhimu inayohitajika kwa ajili ya kutoa huduma hizi za Kimahakama. Kwa hiyo, samani zitapatikana, na mifumo ya ki-TEHAMA yote itakuwepo na rasilimali watu kwa ajili ya kutoa huduma za Kimahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambalo ameuliza kuhusiana na kupatikana kwa makazi kwa ajili ya Watumishi wa Mahakama, kweli katika mpango huu wa kuboresha miundombinu katika Mahakama, Mahakama pia inatazama siyo tu miundombinu ya majengo, lakini pia makazi ya Watumishi katika Mahakama, lakini inafanya hivyo kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kadiri fedha itakapokuwa inapatikana Mahakama imeweka kipaumbele pia kuzingatia ujenzi wa nyumba za watumishi katika Mahakama na wakati ukifika na fedha ikipatikana Mahakama itafika Mbulu pia kwa ajili ya kujenga makazi hayo.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved