Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Naomy Duncan Mwaipopo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NAOMY D. MWAIPOPO aliuliza: - Je, Serikali ina mikakati gani ya kutatua Migogoro ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji?
Supplementary Question 1
MHE. NAOMY D. MAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa muda mfupi walivyopewa dhamana ya kusimamia Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninampongeza Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma Ndugu Gwakisa Tumaini kwa namna ambavyo anapambana kutatua migogoro kwenye mkoa wetu, lakini hasa kwenye Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada ambazo Serikali imeendelea kuzifanya hasa Wizara hii ya Ardhi, wamefanya kliniki kwenye Wilaya za Kigoma, lakini bado kuna changamoto, ambayo inawagusa wanawake wajane na wazee. Ni ukweli usiopingika kwamba…
MWENYEKITI: Naomba uulize swali.
MHE. NAOMY D. MWAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa waathirika wakubwa wa migogoro ya ardhi ni wanawake wajane na wazee, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuna sheria mahususi itakayowalinda na kuwatetea wanawake hawa kwenye migogoro hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na migogoro kwa baadhi ya ardhi inasababishwa na watumishi ambao siyo waadilifu kwenye Wizara hii ya Ardhi, je, Serikali ina mpango gani kuwachukulia hatua na pia kuwarudisha kwenye maeneo yao husika ili kutatua migogoro?
Name
Kaspar Kaspar Mmuya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru, na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, tunapokea pongezi ambazo amezitoa na ninamhakikishia nitazifikisha pongezi hizi kwa watumishi wote wa Wizara ya Ardhi kwa sababu ndio wao wanaoleta matokeo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wajane na wazee, ni ukweli alichokisema kuwa walio wengi ndio wanamiliki ardhi kulingana na historia za kimila ambazo wanakuwa na ardhi hiyo. Ndiyo maana Waziri wetu wa ardhi alitoa maelekezo tukaanzisha kliniki maalum ambayo tuliita ‘Samia Ardhi Kliniki’ kwa ajili ya wanawake pamoja na makundi hayo maalum ya wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumepokea ushauri wake na tutaendelea kuona jinsi gani ya kuwafikia kwa rahisi pamoja na kwenda kufanya kliniki hizi katika ngazi ya kata au vijiji pale ambapo tutaona wingi wa changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Watumishi ambao wanakiuka taratibu za kiutumishi aidha za kinidhamu, mara nyingi tumekuwa tunachukua hatua. Ninaendelea kuwaimiza Makamisha Wasaidizi wote wa Mikoa wahakikishe wanasikiliza changamoto hizi za kiutumishi kutoka kwa wananchi wanaolalamika na kuchukua hatua mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo wanaona kuna hitaji la kupeleka Wizarani, Katibu Mkuu wetu Eng. Anthony Sanga yeye ni mahiri katika usimamizi hasa eneo hili la kinidhamu. Ninaamini hakuna Mtumishi ambaye tutamhamisha tu eti kwa sababu amechafua eneo moja, hapana. Utaratibu wa kinidhamu utafuatwa na atapata adhabu kulingana na kosa ambalo amelifanya ikithibitika. (Makofi)
Name
Neema William Mgaya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NAOMY D. MWAIPOPO aliuliza: - Je, Serikali ina mikakati gani ya kutatua Migogoro ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itatatua changamoto ya mgogoro wa ardhi uliokuwepo Kijiji cha Kanamalenga kati ya Mwekezaji na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kanamalenga? (Makofi)
Name
Kaspar Kaspar Mmuya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Neema kwa kuwa karibu na Wizara hii katika kusaidia kusikiliza kero za wananchi mpaka akatambua uwepo wa mgogoro huu kati ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Neema, baada ya hapa niko tayari pamoja naye kukaa na kupanga tuweze kutembelea eneo hilo na kuwasikiliza wananchi na kuweza kutatua changamoto hiyo.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved