Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwanahamis Athumani Munkunda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kituo cha Umahiri eneo la Mwakitolyo kutokana na ushiriki mkubwa wa wachimbaji wa madini wanawake na vijana?

Supplementary Question 1

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninaipongeza sana Serikali hasa Wizara ya Madini kwa kuendelea kufanya vizuri hasa kwa wachimbaji wadogo, na kwa kweli kutujengea CIP kwenye eneo letu la Mwakitolyo, tutakuwa tumewasaidia sana wachimbaji wadogo na hasa wanawake na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi na jitihada zote ambazo Serikali inafanya ya ujenzi wa CIP ambayo itakuwa na uwezo wa kuchakata tani 120 kwa saa, ni uwekezaji mkubwa. Sasa Serikali haioni haja wachimbaji tunaowazungumzia hapa, ambao ni wachimbaji wadogo, ambao hawana uwezo wa kuzalisha mzigo huu utakaochakatwa kwa siku kwa tani 120; ushauri ni kwamba Serikali ije na CIP ndogo ndogo ili tuweze kuwasaidia wachimbaji wadogo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali. Umeuliza swali la kwanza. Uliza swali la pili.

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, CIP ambazo ninashauri ni zile ndogo ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogo tunaowalenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni haja sasa, kwa kuwa ujenzi wa vituo hivyo vya umahiri vinahitaji uwekezaji mkubwa, watumie Vyuo vya VETA kama Centre of Excellence kwa sababu vyuo hivyo vya VETA viko kila halmashauri ndani ya nchi yetu?

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mwanahamisi kwa jinsi ambavyo amekuwa mtetezi wa kweli wa wachimbaji wadogo katika masuala ya kusaidia Vituo vya Uchakataji Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwanahamisi, hata mwezi haujaisha aliuliza swali ambalo limekaribia kufanana na hili, na nimelijibu hapa hapa, lakini kwa maswali yake haya mawili ya nyongeza, moja ni ushauri. Ushauri wake kwamba hiki kituo kinachochakata tani 120 kwa siku siyo kwa saa, huenda hakitatoa huduma kwa wachimbaji wadogo ambao hawawezi kuleta mzigo wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mwanahamisi kwamba vituo hivi vinajengwa na Taasisi ya Serikali na haimkatalii mtu yeyote mchimbaji mdogo mzigo wowote anaoleta ili asaidiwe kuchakata. Dhamira ya kweli ya Serikali siyo tu kuwachakatia madini yao, ni kutumia vituo hivyo kuwapa mafunzo ili wale ambao wataweza kufikia vigezo na wakawa na mitaji inayoridhisha, wakaanzisha vya kwao hata vidogo vidogo. Ushauri wake tunaupokea kwamba Serikali iendelee kusaidia utengenezaji wa CIP ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia ninatoa wito kwa wachimbaji wadogo ambao wanaokuja kwenye vituo vyetu kujifunza, wachukue teknolojia wakazalishe vituo vidogo vidogo vya CIP. Ninawapongeza wale wote ambao wameshajifunza pale na wameanzisha maana wako wengi kabisa katika kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kutumia VETA zetu kama mbadala wa maeneo ya kutolea haya mafunzo na kuanzisha CIP katika maeneo ya wachimbaji madini, huu ushauri ni mzuri sana, ninampongeza kwa kuishauri Serikali. Hivyo na sisi tutapenda pia kuupokea huo ushauri na kuona namna zile VETA zilizoko katika maeneo ya wachimbaji zinavyoweza kuingiza somo la kujenga mitambo ya kusaidia uchakataji. Pale pale wanafunzi wetu wanaosoma kwenye vyuo hivyo wapate hiyo taaluma, na baadaye nao wakawe wachimbaji wanaojua kufanya kazi hizo.