Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. KANGI A. LUGOLA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti kero ya mamba wanaodhuru wananchi katika Jimbo la Mwibara?

Supplementary Question 1

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na juhudi ambazo Serikali imezifanya kupambana na hawa mamba, lakini nataka kumthibitishia Mheshimiwa Waziri kwamba mamba ni wengi, ni wengi, ni wengi; na hao mamba hawana simile. Ukitisha mamba mmoja, Veronica Marumbo Isige, siku ya mwaka mpya mwanaye amemchinjia mbuzi, ameenda ziwani pale kuchota maji, yeye ndiye akageuka kuwa kitoweo cha mamba mwaka mpya.

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa Kangi.

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa njia za kupambana na mamba ziko nyingi ikiwa ni pamoja na hivyo vizimba alivyovisema na mamba ni wengi, je, kwa nini Serikali isitumie njia za operesheni maalum ya kuwavuna mamba ikiwa ni pamoja na kukusanya mayai pamoja na vifaranga vya mamba visivyozidi kisheria sentimeta 50?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa wahanga wamekuwa ni wengi; katika kipindi cha miaka miwili walioliwa na mamba na wengine kujeruhiwa wanapata 18; ni lini wahanga hawa kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana, watalipwa malipo yao ya fidia?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami ninampongeza tena Mheshimiwa Kangi Alphaxard Lugola kwa maswali yake mawili ya msingi ambayo yana manufaa makubwa katika jimbo lake. La kwanza, ameuliza kuhusu njia mbadala zikiwemo za kupambana na mamba hasa kufanya operesheni maalumu ya kuvuna mamba hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaja hapa, nilizungumza na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na akanithibitishia tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba ameshawaelekeza TAWA wafike katika eneo lake, wafanye sensa ya mamba na kuhakikisha kwamba katika wale mamba ambao ni wakorofi na wanaleta madhara makubwa kwa wananchi, waweze kuwavuna na kuwahamishia katika maeneo ambayo hayana watu wengi kwa maana hayana athari kubwa kwa wananchi. Kwa hiyo, hilo ni elekezo la Mheshimiwa Waziri na TAWA watalitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa wahanga, vilevile Katibu Mkuu wa Wizara amesema walishapokea maombi hayo na yapo katika mchakato, na watakavyomaliza hizi katika hatua za mwisho, watawalipa wale wananchi. Kwa hiyo, namthibitishia tu kwamba yote Serikali imeshayapokea na inayafanyia kazi.