Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ado Shaibu Ado
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Tunduru Kaskazini
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 1
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninaomba niseme, ingawa mara kadhaa huwa tunaingia kwenye anga za vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa sababu nilitoa ahadi ya kwamba nitakuwa sauti yao ndani ya Bunge hili kupigania maslahi yao na haki yao, siyo Tunduru tu, na nchi nzima, ninaomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa Serikali iko katika kufanya tathmini na kutafuta fedha, na kwa sababu hali ya gereza lile ni chakavu, na inasikitisha sana kwa kiwango ambacho Askari wale wanakosa hata ofisi za uhakika za utawala; na wameanzisha mpango kwa fedha ndogo za utawala wanazopewa kujenga ofisi ndogo nje ya magereza, je, ni kwa nini Serikali katika hatua ya dharura isiwapige jeki Askari wale kuhakikisha kwamba wanapata ofisi ndogo ya utawala wakati mipango mikubwa ya Serikali ikiwa inasubiriwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hali ya Askari Magereza Wilayani Tunduru katika eneo la nyumba za makazi imekuwa ni duni sana, hali ambayo ni ya nchi nzima kwa Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Jeshi la Zimamoto, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Askari wetu nchini wanapata makazi bora ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kuliko hali ilivyo hivi sasa?
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninampongeza sana Mheshimiwa Ado Shaibu kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Amesema, kwa kuwa wamekuwa wakiingia kwenye anga za vyombo vya ulinzi mara kwa mara, kwanza nimsihi kwamba wasiingie kwenye hizo anga pale isipohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo hivi vya ulinzi na usalama uwepo wake siyo kwa sababu ya kumwonea mtu, ni kwa sababu ya kufuata sheria tulizozitunga sisi Wabunge humu kwa ajili ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuwapiga jeki Gereza la Tunduru, nataka kumhakikishia kwamba Serikali kupitia Jeshi la Magereza itahakikisha kwamba inawapa fedha Gereza la Tunduru ili kuweza kukamilisha ofisi zao kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile hali ya upanuzi kama nilivyoeleza, tutaendelea kutenga fedha kwenye bajeti na fedha hizi nilizozieleza sasa ni zile zitakazotokana na vyanzo vya ndani vya Jeshi la Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali la pili la nyumba za Askari, nikiwa najibu maswali ya msingi jana, nilitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na nyumba za Askari kwa upande wa Serikali. Mpango uliopo ni wa muda mrefu wa kujenga nyumba 6,368 kwa nchi nzima kwa ajili ya Askari Magereza. Ninamhakikishia kwamba tutaendelea kuutekeleza mpango huo kadri ya hali ya fedha zitakavyopatikana. (Makofi)
Name
Tinnar Andrew Chenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 2
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati majengo ya Gereza la Bariadi hususan jengo la mahabusu ambalo kwa kweli liko katika mazingira hatarishi?
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Tinnar, Mbunge wa Bariadi kwa swali lake la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumetoa maelezo ya awali kwamba Serikali ina mpango wa ukarabati na ujenzi wa majengo ya magereza nchi nzima ili kuhakikisha kwamba mazingira ya magereza hayo yanaakisi hali ya sasa, lakini vilevile hali ya ubinadamu hasa kwenye yale magereza tuliyorithi, kazi hiyo tutaifanya kadri ya hali ya upatikanaji wa fedha itakavyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini Gereza la Kihesa Mgagao lililopo Kilolo litahamishwa kwa sababu ni eneo walikuwa wanaishi wakimbizi waliopigania uhuru? Tunaomba Gereza lile litumike kama yalivyo magereza mengine kuliko linavyotumika sasa hivi, gereza la kuweka wafungwa.
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la Gereza la Kihesa Mgagao. Gereza la Kihesa Mgagao ni gereza lenye historia kubwa kwenye nchi yetu. Ni gereza ambalo kwanza limekuwa likitumika kama ni eneo la kufikia wapigania uhuru wa nchi mbalimbali ikiwemo South Africa. Baada ya kupatikana uhuru, gereza lile lilikabidhiwa kwa wenzetu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuwa kama ni Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa eneo lilikuwa ni dogo kwa matumizi ya Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, gereza lile lilikabidhiwa kwa Jeshi la Magereza, na hadi sasa lipo ndani ya mikono ya Jeshi la Magereza. Wazo la kubadilishwa matumizi na hasa kwa kuzingatia historia, wazo hilo Serikali ililijadili katika Awamu ya Nne ya Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yametolewa kwamba sehemu ya gereza hilo inaweza kutumika kama ni shule ili kusudi kutoa nafasi kwa vile vyumba ambavyo vikitumika kwa ajili ya wale wapigania uhuru, kama ni sehemu ya historia kwa maana ya kumbukumbu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wazo hilo linaendelea kufanyiwa kazi ambapo sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunaendelea kutafuta fedha kwa ujenzi wa gereza jipya. Vilevile tuko tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wizara ya TAMISEMI kwa ajili ya shule na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuweka eneo la kivutio cha utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwakilisha.
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 4
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni kweli majengo mengi ya magereza nchini ni chakavu likiwepo Gereza la Wilaya ya Mbulu. Sasa ni upi mpango wa Serikali wa kukarabati gereza hilo?
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na ninataka kumwahidi tu kwamba tunao mpango wa kuendelea kufanya ukarabati wa magereza nchi nzima, na hasa kubadili ule utaratibu wa kizamani wa kuyatumia magereza kama ni maeneo ya adhabu badala yake yawe ni maeneo ambayo wanapelekwa watu kwenda kubadilishwa tabia. Kwa hiyo, mpango huo unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa hali ya kifedha itakavyoruhusu.
Name
Devotha Methew Minja
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 5
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniona. Licha ya kazi kubwa inayofanywa na Askari Magereza, Gereza la Kingolwira ni gereza ambalo linahudumia wafungwa wengi sana, lakini Askari wanaoishi maeneo yale, makazi yao ni duni na hayafai na hayastahili kabisa. Serikali ina mpango gani wa kukarabati nyumba za Askari hawa? (Makofi)
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, ninaomba kuendelea kukumbusha tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi bilioni 13 kwa kazi ya ujenzi na ukarabati pamoja na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nyumba za Askari kwa Gereza la Kingolwira ni sawa na zile za wengine ambazo zipo kwenye mpango wa ukarabati kwa kadri ya hali ya upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kupanga fedha kadri bajeti itakavyoruhusu kwa maana ya ukomo ili tuweze kufanya ukarabati wa nyumba hizo.
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ADO S. ADO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
Supplementary Question 6
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kufahamu, kwa mwaka huu wana mpango gani wa kupeleka magodoro katika Gereza la Ilembo - Mbozi?
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Neema kwa swali lake la msingi la vitendeakazi au magodoro ya kuishi wafungwa wetu kwenye magereza ya maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamwambia kwamba mengi ya magereza yanayo magodoro, lakini kwa mujibu wa bajeti yetu kama nilivyosema, tulitenga shilingi bilioni 13, na miongoni mwa vitu tutakavyonununia ni magodoro. Kwa hiyo, tayari fedha hizo zipo, na utaratibu wa ununuzi unaendelea awamu kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.