Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Onesmo Merdson Mnkondya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. ONESMO M. MNKONDYA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga chuo kikuu katika Mkoa wa Songwe?

Supplementary Question 1

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa majibu ambayo imeyatoa kuhusiana na tawi hili la DIT, lakini ninaomba niwe na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kufuatia kile kinachofundishwa kwenye chuo hiki ambacho kiko chini ya Dar es Salaam Institute of Technology – DIT ambacho kimejikita zaidi kwenye ufundi, ni lini upanukaji wake utalenga taaluma ambazo zitaendana na mazingira ya Mkoa wa Songwe, hasa biashara, kilimo na kadhalika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ili kuusisimua Mkoa wetu wa Songwe, ikizingatiwa ni mkoa mchanga na kuupa uchumi na maendeleo zaidi, ni lini Serikali itajenga chuo kikuu Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe ambayo yapo Wilaya ya Mbozi ambapo tayari mahali hapa tuna maeneo ya kuanzia kujenga kama Msense, Mifugo Kata ya Isansa; Zelezeta, Mbozi Missiyon Kata ya Igamba; Ipunga pamoja na Hasamba?

Name

Wanu Hafidh Ameir

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Onesmo kwa ufuatiliaji wake wa karibu kuhusu kuongeza vyuo vikuu katika Mkoa wa Songwe. Alishawahi kunifuata ofisini akifuatilia suala la Chuo cha VETA Songwe ambacho kwa sasa kinaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, hivi sasa Serikali inaendelea na upanuzi wa chuo hicho, na nia ya kuongeza chuo hiki ni kuongeza udahili wa wanafunzi na taaluma ambazo zitatolewa katika chuo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mawazo ya Mheshimiwa Mbunge au ushauri unaenda sambamba na azma ya Serikali katika upanuzi wa chuo hicho. Kwa hiyo, ushauri wake au mawazo yake tumeyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kama nilivyoeleza katika swali la msingi, kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu katika kutanua vyuo vikuu na kuongeza kampasi katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania. Mpaka hivi sasa mikoa 16 imeshapata kampasi ya vyuo mbalimbali ikiwemo hii ya DIT Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, UDSM imepeleka kampasi Lindi na Kagera, AIA imepeleka kampasi Manyara, TIA imepeleka kampasi Mwanza na maeneo mengine na mikoa mbalimbali ina kampasi mbalimbali za vyuo vya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali itaendelea kuongeza taasisi hizi kulingana na uwezo na bajeti itakavyoruhusu. Hivyo, pale bajeti itakaporuhusu, basi tutaweza kupeleka chuo kikuu katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. ONESMO M. MNKONDYA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga chuo kikuu katika Mkoa wa Songwe?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri kabisa ya Waheshimiwa Wabunge. Wilaya ya Kahama ina halmashauri tatu, na iko ukanda wa nchi za East Africa. Sasa, Serikali ina mkakati gani wa kuweka kampasi ya chuo kikuu katika maeneo ya halmashauri ya Ushetu, kwa sababu eneo tayari tumetenga zaidi ya heka 800?

Name

Wanu Hafidh Ameir

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali ina azma ya kusogeza elimu ya juu ya vyuo katika mikoa yote ya Tanzania. Kama nilivyosema, pale bajeti na uwezo utakaporuhusu, basi Serikali pia itafikiria kupeleka chuo kikuu katika mkoa wa Mheshimiwa Chereheni. (Makofi)