Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nuru Issa Kashakari

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Primary Question

MHE. NURU I. KASHAKARI aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Malagarasi, Kijiji cha Ilagara ili kuwasaidia wananchi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika?

Supplementary Question 1

MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Daraja la Mto Malagarasi kule Ilagala ni nyeti sana kwani wananchi wa Kata za Mwakinzega, Ilagala, Sunuka, Sigunga, Herembe, Igalula, Buhingu, Karia na Hifadhi ya Mahale ni waathirika, wanaishi Tanzania kama hawaishi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mto Malagarasi pale Ilagala, ukifika pale wewe mwenyewe ukajionea wananchi wanavyohangaika na kutaabika, kwa kweli inaumiza sana. Ninaomba kuuliza swali Serikali. Je, ni lini sasa huu mpango utakamilika ili kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wanapata huduma za barabara na lile Daraja la Mto Malagarasi kule Ilagala?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anakubali kuambatana nami twende akajionee jinsi wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wanavyopata adha katika nchi yao?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, mimi ninajibu kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Kwa bahati mbaya wakati ninakuja sikumwuliza kama atakubali hii hoja ya pili ya kwenda. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba nitakwenda kumfikishia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na kumwomba ili aweze kuambatana naye. Kama atanituma mimi kwa idhini ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi pia sitakataa maelekezo hayo, nitafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja yake ya kwanza, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara hii pamoja na daraja hilo; na ndiyo maana imeshaanza hatua za awali za kufanya usanifu wa kina na baadaye tutafute fedha ili kuhakikisha kwamba wananchi aliowataja na maeneo mengine wanaweza kupata huduma hiyo ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.