Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Handeni kupitia Olboloti - Mrijo - Chemba - Kwamtoro hadi Singida utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninatoa masikitiko yangu kwa Serikali. Barabara hii imekuwa ikisemwa kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Mwaka 2025 wakati tunahitimisha bajeti hapa, Serikali iliji-commit kwenda kumaliza hayo majadiliano. Kwa kuwa, anayenijibu ni Naibu Waziri wa Uchukuzi; na TPA kwa maana ya bandari iko kwake, ninatamani kujua, je, ni lini haya majadiliano yatakamilika ili ujenzi huu uweze kuanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa barabara hii ni ndefu, na ina eneo pana, lakini katika uhalisia Wilaya ya Chemba ndiyo tuna eneo kubwa, kilometa 173.3, je, Serikali iko tayari kutupatia mkandarasi atakayeweza kushughulika na kipande hicho cha kilometa 173.3 ya Wilaya ya Chemba?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamwomba Mheshimiwa Kunti Majala apunguze masikitiko, awe ni mtu mwenye furaha, awe na matumaini kwa sababu Serikali iliahidi huko nyuma na imekwishaanza kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi siyo mmoja, ninamwomba aendelee kuelimisha wananchi wetu wawe na subira, kwa sababu tunamhakikishia kwamba barabara hii itakwenda kujengwa na tayari imeshaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Kunti amezungumza kuhusiana na ni lini majadiliano yataanza? Hii barabara awali ilikuwa kwenye mfumo wa EPC+F kama ambavyo tunafahamu, lakini baadaye tumeijenga kwa mfumo wa ubia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inayounganisha Mkoa wa Tanga kwenda Singida mpaka nje ya nchi yetu, tayari mwaka 2025 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Tanga alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo ni Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na TANROADS ili kuona namna ya kwenda kujenga barabara hii. Ndiyo maana nilimwambia atoe mashaka kwa sababu Mkuu wa Nchi mwenyewe ana jicho lake kwenye barabara hii, anatamani kuiona ikijengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kimefanyika? Tayari vikao vimeshafanyika, na hivi ninavyozungumza, wataalam wa TPA wako Bagamoyo, ambapo pamoja na mambo mengine wanajadili jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, mara baada ya majadiliano tutaweka mpango na mfumo mzuri, na ujenzi wa barabara hii utafanyika kwa sababu ni mwarobaini unaokwenda kusaidia kuhakikisha kwamba Bandari ya Tanga, (ambayo Serikali ilipeleka shilingi bilioni 429.1) ili ifanye kazi vizuri, ni lazima tuboreshe miundombinu yake ikiwemo barabara, ambayo kazi hiyo imeshaanza. Tumeshazungumza, pamoja na reli imeshaunganishwa mpaka bandarini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Kunti Majala apunguze kidogo masikitiko yake, awe ni mtu mwenye furaha kwa sababu Serikali hii imedhamiria kuleta tabasamu kwa wananchi wake.