Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amosy William Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha SGR katika eneo la Nyahuwa ili kuboresha usafiri na usafirishaji?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kata ya Nyahuwa ni moja ya Kata ambazo ziko bondeni sana na hivyo kufanya miundombinu ya barabara na hususan wakati wa masika inakuwa ni shida sana, hivyo wananchi wa Kata ya Nyahuwa hutegemea sana usafiri wa reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu aliyoyatoa kwamba hawa wananchi wanaweza wakatumia vituo vya karibu ikiwemo Kituo cha Malongwe pamoja na Goweko, vituo hivyo viko mbali. Mfano, upande wa Mashariki ni Kituo cha Malongwe ambacho kipo umbali wa kilometa 34, lakini upande wa Magharibi ni Kituo cha Goweko ambacho kiko umbali wa zaidi ya kilometa 32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuweka kile kituo au kupitia upya zile tathmini pamoja na upembuzi ili wananchi wa Nyahuwa waweze kuwekewa kituo cha stesheni pale?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Naibu Waziri utakuwa tayari kuambatana nami ili kujionea jiografia na mazingira ya Kata hii ya Nyahuwa kwamba kweli kuna haja ya hawa wananchi kuwekewa hicho kituo? Ahsante sana.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mbunge Maganga kwa uzalendo wake na jinsi anavyowajali wananchi wa Sikonge, pamoja na maeneo hayo ambayo ameyasemea ikiwemo Nyahuwa, Igigwa na mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimejibu jinsi ambavyo tunafanya utaratibu wa kuweka vituo. Kama tungetoa nafasi hapa, Wabunge wengi sana wangependa pengine tusogeze vituo maeneo yao ya jirani. Hapa kwa mbali ninamwona Mbunge wa Dodoma Mjini, ninajua na yeye anataka kuuliza swali kama hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Wabunge pamoja na Mheshimiwa ambaye yuko hapa kwamba kwa sasa, tuanze na vituo vilivyopo, lakini Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina, hatua kwa hatua kulingana na mahitaji yaliyopo. Kwa sababu, tukisema pia hii reli ya treni ya mwendokasi tuweke kituo mara kwa mara kila sehemu, yatakuja malalamiko tena, kwa sababu kama ilitakiwa ifike kwa masaa mawili, manne vituo vikiwa vingi zaidi, vitafika hata kwa masaa nane, hata dhana nzima ya reli ya mwendokasi, treni ya mwendokasi itapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na ombi la Mheshimiwa Maganga kwamba nipo tayari kwa niaba ya Waziri wetu, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, kuambatana naye na timu yangu ya watalaam, twende tukatazame eneo hilo upya, ikionekana na ikithibitika kuna ulazima huo mkubwa sana, pengine tutakuwa katika nafasi nzuri ya kupitia upya maamuzi yetu ambayo tulishayafanya pale mwanzoni.
Name
Dr. Yahaya Esmail Nawanda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha SGR katika eneo la Nyahuwa ili kuboresha usafiri na usafirishaji?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Nina swali dogo la nyongeza. Tayari Serikali imeshakamilisha upembuzi yakinifu wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi reli hiyo?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Nawanda kwa jinsi anavyofuatilia maendeleo, siyo tu ya nchi yake, lakini pia na miradi ya kimkakati ya upande wa Kusini. Sote tunakubaliana, na Serikali ya CCM imethibitisha, Mheshimiwa Dkt. Samia ametuhakikishia kwamba reli ya kusini inayotoka Mtwara mpaka Mbamba Bay ni jambo ambalo halijadiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumweleza kwa kifupi sana kwamba, ambacho tumekifanya kama Serikali mpaka sasa ili yeye pamoja na wananchi anaowapigania na Wabunge wengine wote wa Kusini ambao nina uhakika wangependa kufahamu, Serikali imefanya mambo kadhaa. Moja, tayari ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay imeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka reli hii inaunganisha maeneo mawili, Mbamba Bay na Mtwara. Shilingi bilioni 80 ziliidhinishwa na Rais na ujenzi umeshaanza na tuko hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pamoja na kufanya ukarabati mkubwa wa shilingi bilioni 157 kwenye Bandari ya Mtwara, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitambua kwamba reli hiyo itasafirisha mzigo wa makaa ya mawe, ameidhinisha fedha shilingi bilioni 435 kwenye bandari mpya, bandari ya Kisiwa Mgao ambayo ni maalumu kupitisha bidhaa chafu yaani dirty cargo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, kwa kuzingatia kwamba eneo hili, reli hii itapitisha mzigo wa makaa ya mawe kama nilivyozungumza, wananchi wa Ludewa, zaidi ya 1,000, wameanza kulipwa fidia. Hatua inayofuata sasa ilikuwa ni kufanya usanifu wa kina ambao nao umekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta mkandarasi ambaye tutashirikiana naye kwenye ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge, kama ilivyokuwa kwa reli ya kati, ilikuwa hayawi hayawi, leo yamekuwa. Tunasafiri kwa SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, tunao wakandarasi ambao wanafanya kazi kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma mpaka Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imedhamiria na imethibitisha kwenye Ilani ya CCM ya miaka mitano ijayo kwamba itakwenda kuijenga reli hii. Tujipe muda, tutakwenda kufanya kazi hiyo muda utakapofika.
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha SGR katika eneo la Nyahuwa ili kuboresha usafiri na usafirishaji?
Supplementary Question 3
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Tabasamu la wananchi wa Dodoma, Morogoro, mpaka Dar es Salaam wameliona na wanaendelea kulifurahia. Ninamwuliza Waziri, ni lini sasa SGR itakamilika kutoka Dodoma – Tabora – Shinyanga - Mwanza ili tabasamu hili wanalolipata wananchi wa kuelekea Dar es Salaam, basi waanze kulipata na hawa wananchi wanaoelekea upande wa Kanda ya Ziwa? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mary Masanja kwa kufuatilia mradi huu wa SGR ambao watanzania wote unawanufaisha na wengine wanausubiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imethibitisha dhamira ya kufikisha SGR Mwanza. Hivi navyozungumza, wakandarasi wako site kutoka Dodoma - Tabora na kutoka Tabora - Isaka na kutoka Isaka - Mwanza. Ni dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia mikataba mbalimbali ambao tumeingia kukamilisha na kufikisha treni ya kisasa Mkoani Mwanza na Kigoma kabla ya 2030. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved