Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
John Francisco Nzilanyingi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI K.n.y. MHE. ERICK J. SHIGONGO aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa chanjo ya homa ya ini kwa Watanzania wote?
Supplementary Question 1
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Erick Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yanazidi kuongezeka na hii ni kwa sababu chanjo hii ya homa ya ini hutolewa miezi sita baada ya mtoto kuzaliwa; na hivyo watoto wengi wanapata maambukizi haya katika kipindi cha miezi kuanzia sifuri mpaka miezi sita. Je, Serikali haioni haja ya kuanza kuitoa chanjo hiyo mapema tu pindi mtoto anapozaliwa, kama ambavyo nchi nyingi duniani zinafanya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, gharama za chanjo hii zinaonekana kuwa kubwa kwa Watanzania. Je, Serikali haioni haja ya kuziweka kwenye bima ya afya ili watoto wengi na wananchi wengi waweze kupata huduma hii?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali ya nyongeza kwa Mheshimiwa Shigongo ambaye amekuwa kinara wa kupambana na ugonjwa wa homa ya ini katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, kwanza, ninaomba nikuthibitishie, chanzo ya homa kwa mtoto inatolewa mara tu baada ya mtoto kuzaliwa na siyo baada ya miezi sita. Kwa hiyo, hakuna takwimu zinazoonesha kwamba maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanaongezeka kutokana na chanjo.
Mheshimiwa Spika, chanjo hii ya mtoto inatolewa bure na Serikali, na chanjo hii imeanza kutolewa tangu mwaka 2002. Hiyo kuchangia, kwamba watoto wote waliozaliwa mwaka 2002 hadi leo, kwa maana ya watoto wa mwaka mmoja hadi 24 wamekingwa kuambukizwa na ugonjwa wa homa ya ini. Chanjo hiyo hutolewa bure kwa watoto wote hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu gharama ya chanzo. Kwanza kabisa hapa niaipongeza Serikali ambayo kwa makusudi kabisa ilileta chanjo kwa watu wazima, kwa maana sasa ni wale wa umri wa 25 na kuendelea ambao hawakupata ile chanjo ya utoto. Chanjo hii inatolewa katika hospitali zote baada kuwa umepimwa na kuthibitisha kwamba huna chanjo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa makusudi kabisa iliwalipia watalaamu wote wa afya kupata hii chanjo ya homa ya ini bure nchini ili wasiweze kupata maambuziki kwa sababu wako katika hatari. Hata hivyo, wale ambao wanajilipia gharama ya chanjo ni shilingi 10,000 kwa sindano moja ya chanjo hiyo ya homa ya ini. Serikali imeshaanzisha rasmi huduma ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo tumeshaanza utekelezaji wake kwenye Kundi la pilot.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, lengo la Serikali na lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanakuwa na afya njema. Kwa kupitia bima ya afya, hakuna mwananchi atakayebaki nyuma bila kupata huduma hii ya chanjo.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwaasa Watanzania wote waende hospitalini wakapime, wakajue hali yao ya homa ya ini, kwa sababu changamoto kubwa ni kwamba mpaka sasa chanjo hiyo ya homa ya ini kwa watu wazima uptake yake ni ndogo, Watanzania hawaendi kuchanja ilhali chanjo hiyo ipo. Kwa hiyo, waende wakachanje kwa sababu ipo na hospitali zote nchini zinatoa hiyo chanjo. Ninaomba kuwasilisha.
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI K.n.y. MHE. ERICK J. SHIGONGO aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa chanjo ya homa ya ini kwa Watanzania wote?
Supplementary Question 2
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona. Ugonjwa huu wa homa ya ini kwa Watanzania wengi unaonekana kama ni ugonjwa mgeni ambao haujafahamika sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa Watanzania walio wengi kwa ugonjwa huu hatari ili waweze kufika kwenye vituo vya afya ama kwenye hospitali zetu ili waweze kupimwa na ikigundulika waweze kupatiwa tiba ama kupatiwa chanjo?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Hawa kwa kuwa alilolisema ni suala dhahiri kabisa. Watanzania wengi wanaona kwamba ugonjwa huu wa homa ya ini hauwahusu, lakini nikuhakikishie, kwamba takwimu zinaonesha prevalence ya ugonjwa huu katika nchi hii ni asilimia tatu nukta tano ya Watanzania wana ugonjwa huu. Iko mikoa ambayo iko juu sana kama Katavi, Rukwa, Kigoma, na Geita, imefika mpaka asilimia sita, nne, ambapo wako juu ya kiwango cha nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa wajawazito takwimu zinaonesha prevalence ni asilimia saba. Kwa hiyo, hili tatizo la homa ya ini ni tatizo katika nchi hii, na ni tatizo dunia nzima. Katika Afrika nzima watu milioni 60 wanaishi na tatizo hili la homa ya ini. Kama Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Kutoa Elimu ya Afya tumeendelea kuwaelimisha Watanzania, waende hospitalini wakaangalie afya zao na kujua kama wameathirika ili waweze kupata chanjo au tiba; na hasa ni Hepatis B ambayo imeonesha uwezekano mkubwa wa kusababisha kwanza kuleta ugonjwa wa ini wa kudumu ambao unaweza kupelekea mpaka ini kushindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaasa Watanzania wote, tukiwemo sisi wenyewe Wabunge twende tuka-check hali zetu za homa ya ini. Ugonjwa huu upo na unaathiri Watanzania wengi. Chanjo ipo na tiba ipo. Kwa hiyo, tukapime. Kinga ni bora kuliko tiba.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved