Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kijakazi Mohamed Yunus

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED aliuliza: - Je, lini Mkataba wa kuchakata Gesi Asilia (LNG) Lindi utasainiwa na kuanza utekelezaji?

Supplementary Question 1

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tulimsikia pia jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akitoa maelezo yanayofanana na haya. Ningependa kufahamu, au ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mosi, kama ilivyoeleza Serikali kwamba wako kwenye majadiliano ambayo yanaelekea ukingoni kwenda kusainiwa kwa mkataba, je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanatoa elimu, sambamba na uwezeshaji kwa wananchi wa Tanzania hususan wanawake wa Mkoa wa Lindi pamoja na vijana ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuzipata fursa, hususan zile zinahusiana na sheria ya local content ili waweze kunufaika na mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mwaka 2023/2024 Wizara ya Nishati iliingia makubaliano na Wizara ya Elimu kupitia Arusha Technical College kwa ajili ya ujenzi wa chuo kitakachofundisha masuala ya nishati na mafuta; na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilitoa eneo lenye ukubwa wa square meter 256,000 katika eneo la Kikwetu pale Lindi. Kwa mujibu wa makubaliano, ilikuwa ujenzi wa chuo kile ujengwe haraka iwezekanavyo ...

SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali lako.

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: ...lakini mpaka sasa bado ujenzi haujaanza, ningependa kufahamu, je, ni lini ujenzi wa chuo kile utaanza? La, kama Serikali haipo tayari, kwa nini, isirejeshe eneo lile kwa manispaa ili waendelee na shughuli nyingine, ikiwemo kuuza maeneo yale ili manispaa iweze kupata mapato?

Name

Salome Wyckiffe Makamba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kijakazi Mohamed, almaarufu Binti Lindi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufutilia mradi huu wa LNG. Ninajua kuwa anafanya hivyo kwa sababu anajua kuwa huu ni mradi wa kihistoria ambao ukifanikiwa kuanza mikoa ya kusini itabadilika sana kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, linahusiana na kuwajengea uwezo wanawake na wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Sasa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaendelea kutoa elimu kupitia VETA, SIDO na vyuo vingine, lakini pia kuna ujenzi mkubwa wa shule ya amali unaendelea kwa ajili ya kutoa elimu juu ya namna ambavyo wananchi wanaweza kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huu wa LNG ambao utaanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na chuo cha elimu ya juu ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, ni kweli. Kwanza tunawashukuru Wanalindi kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki; na hii ni kwamba elimu juu ya uchakataji wa mafuta na gesi bado ni jambo geni kidogo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza kwa hilo, na Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba chuo hiki kinajengwa ili wananchi waweze kupata ujuzi na kushiriki katika mradi huu wa kimkakati na tutafanya hivyo kwa kadri ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyowezekana. Ninaomba kuwasilisha.

Name

Arif Suleiman Premji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED aliuliza: - Je, lini Mkataba wa kuchakata Gesi Asilia (LNG) Lindi utasainiwa na kuanza utekelezaji?

Supplementary Question 2

MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunaongelea Mradi wa LNG wa shilingi trilioni 100. Chombo cha habari cha Citizen na Reuters ya London vilichapisha habari tarehe 27 mwezi wa kwanza mwaka huu; na kwenye habari hiyo ilimnukuu mmoja wa Waziri akisema kwamba mkataba utasainiwa mwisho wa mwezi wa Sita. Jana tumesikia kwamba kuna majadiliano bado. Je, ni ipi kauli rasmi ya Serikali kuhusiana na kusainisha mkataba huo? Ahsante sana.

Name

Salome Wyckiffe Makamba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa kauli jana, na kama ambavyo majibu yangu ya msingi ya swali hili nimeyaeleza hapa leo mbele ya Bunge hili Tukufu, mradi wa LNG upo katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya kisheria na ya kimkataba ili waweze kusaini mikataba na kuanza mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.