Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kija Limbu Ntemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Katoro
Primary Question
MHE. KIJA L. NTEMI aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Zimamoto ili kusaidia majanga ya moto yanapotokea Katoro?
Supplementary Question 1
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, naomba nimwulize Waziri maswali ya nyongeza mawili. Swali la kwanza, kwa sababu ya uharaka wa ujenzi wa kituo hiki, na kwa sababu sasa hivi wale zimamoto wanapata shida sana sehemu ya kuishi, je, ni lini sasa hiyo hati itakamilika, kwa sababu tulipita kwenye mfumo wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan uliokuwa unaitwa Samia Ardhi na ulikuwa kwake Mheshimiwa Waziri, nadhani na katika sehemu nyingi alipita, lini sasa tutapata hiyo hatimiliki kwa ajili ya kuanza ujenzi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya kupata hiyo hati kuambatana na mimi kwenda kutukabidhi hilo eneo ili kuleta motisha katika jamii na watu wa Katoro? Ahsante. (Makofi)
Name
Kaspar Kaspar Mmuya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumpongeza sana Injinia Kija, kwanza kwa ukaribu wake na wananchi wake, anayeweza kufuatilia changamoto za wananchi wake. Ninakiri kuwa jambo hili analifahamu kwa kina na ndiyo maana analifuatilia kujua lini hati itatoka?
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali lake limekuja kwa wakati muafaka, hati hii nikitoka hapa leo nitaenda kuifuatilia na ndani ya wiki ijayo nitampatia jibu ambalo nina uhakika atapata lini hati yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Injinia Kija ni kwamba Wizara ipo tayari na mimi nipo tayari kuongozana naye katika muda ambao atapanga ili twende kwenye eneo hilo, huku nikifahamu jimbo lake ni kubwa na lina ukuaji mkubwa wa kiuchumi. Ninafahamu hata Kata tu ya Katoro pale jinsi ilivyo na watu wengi zaidi ya 92,000 inahitaji huduma za zimamoto za haraka. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na gari ipo, tukijenge kituo hiki, tunawaletea na gari kabisa, ahsante sana. (Makofi)
Name
Alan Thomas Mvano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kakonko
Primary Question
MHE. KIJA L. NTEMI aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Zimamoto ili kusaidia majanga ya moto yanapotokea Katoro?
Supplementary Question 2
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Kakonko ilianzishwa tarehe 8 Machi, 2013 na hadi leo hatuna Ofisi ya Zimamoto wala gari la Zimamoto. Je, ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto na kujenga ofisi kwa kuwa tayari eneo lilishatengwa? Ahsante. (Makofi)
Name
Kaspar Kaspar Mmuya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mbunge kutoka Kakonko kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, nimhakikishie tu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mapinduzi makubwa sana kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani, hususan Jeshi hili la Zimamoto.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie mpaka sasa hivi kwa mkopo ambao ameupata zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 ameweza kununua magari zaidi ya 237 ambayo yamesambazwa katika mikoa na wilaya zake.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza sasa, kuna Wilaya sita tu ambazo hazijapata magari haya na siyo kama hawajapata kwa sababu hawastahili, hapana, ni kwa sababu madereva wanaotakiwa kuendesha magari hayo bado hawajapatikana katika Wilaya hizo.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie, kwa jitihada ambazo Serikali inazifanya, hao madereva, hao Askari sasa hivi wapo vyuoni na watafundishwa na watapatikana na tutampelekea gari pamoja na madereva kwa ajili ya vituo hivyo sita. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved