Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwanaisha Ng'anzi Ulenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: - Je, lini Serikali itatwaa maeneo ya karibu na Bandari ya Tanga, ili kuongeza eneo la utekelezaji wa shughuli za Bandari?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mchakato wa kutwaa maeneo aliyoyataja Naibu Waziri katika Bandari ya Tanga ulianza mwaka 2014 na mwaka 2015, takribani miaka 10 sasa. Ninaomba kuelewa, mpaka sasa Serikali inafeli wapi kuweza kutwaa maeneo hayo?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Serikali ilishatwaa maeneo katika Bandari ya Mwambani zaidi ya miaka 10 sasa. Takribani shilingi bilioni 10 zilitumika kuwalipa wananchi wale waliopisha maeneo yale. Je, ni nini mkakati wa sasa wa kuendeleza maeneo ya Bandari ya Mwambani? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulenge kwa ufuatiliaji wake mkubwa, makini wa Bandari ya Tanga na miradi yote ya kimkakati, ambayo ina maslahi makubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pili, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali haijafeli, inatambua umuhimu wa Bandari yetu hii ya Tanga kwa uchumi wa Taifa letu na wananchi wa Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana bandari hii ambayo ilianzishwa miaka 146 iliyopita ilifanyiwa maboresho karibu mara mbili, mwaka 1913 na mwaka 1954. Ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2023 aliyetimiza ndoto za kufanya mabadiliko na mageuzi makubwa ya kibandari katika Bandari ya Tanga, ambapo alitoa fedha shilingi bilioni 429.1 ambazo zilikwenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye bandari, tumeona kina kimeongezeka, eneo la kugeuzia meli limeongezeka, pamoja na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko hayo makubwa ya kibandari, tumeshuhudia shehena imeongezeka zaidi, mzigo umetoka tani 735,000 mpaka takribani tani milioni 1.4. Tumeona magari ambayo yalikuwa hayahudumiwi mwanzoni kwenye Bandari ya Tanga, kwenye mwaka wa fedha uliopita yamehudumiwa magari 15,618. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata mawakala wa meli wamechangamkia fursa. Tulikuwa na mawakala 29 tu, wakafika 33, na hata idadi ya meli zimeongezeka zaidi kutoka 113 mpaka takribani meli 458; hata makasha yalitoka 7,000 mpaka 9,000. Unaweza kuona kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ameifanya kwenye bandari hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu mkubwa, leo Bandari ya Tanga watu wengi wanakimbilia kwenda kupata huduma zao. Ninakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge makini anayefuatilia jambo hili kwamba, sasa tunahitaji maboresho makubwa. Ndiyo maana hata ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokwenda huko hivi karibuni aliiagiza Wizara hii na kumwagiza Mheshimiwa Waziri wetu na sisi wote tuhakikishe kwamba, tunabuni zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge wetu kwamba, Serikali kama ambavyo nimesema, haijafeli, imeshaanza mchakato wa kutwaa ekari saba pembeni mwa Bandari ya Tanga. Hivi ninavyozungumza, kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, mchakato umeshaanza. Tunachokifanya ni tuweze kulipa fidia, tuweze kuongeza gati nyingine tatu zifike tano. Vivyo hivyo kwa upande wa Mwambani, kama alivyozungumza, tayari tumepokea maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wetu na wenzetu wa TPA wameshaanza mchakato.
Mheshimiwa Spika, katika zile acre 174 zilizokuwa zimetwaliwa takribani miaka 10 iliyopita, ambalo ndiyo swali lake la pili, tumeshakamilisha upembuzi yakinifu. Sasa tumetwaa eneo, huwezi kupanga matumizi bila kujua unataka kwenda kufanya kitu gani? Tumemaliza upembuzi yakinifu, na tayari tunaanza kwenda kutekeleza. Pengine mwaka wa fedha ujao, nini tutakwenda kukifanya? Ninawaahidi, wakati tunasubiri kuanza kutumia eneo hilo kubwa tayari ndiyo eneo ambalo tunalitumia kwa ajili ya maegesho yetu ya magari.
Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha, ninawaomba wenzetu wa Wizara ya Ardhi watusaidie kukamilisha kwenye utwaaji wa ardhi hiyo na kuiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kwamba, wakamilishe haraka iwezekanavyo kwa sababu, uhitaji wa Wanatanga na Watanzania kuona bandari hiyo inazidi kuboreshwa zaidi ni mkubwa zaidi. (Makofi)
Name
Cornel Lucas Magembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato Kaskazini
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: - Je, lini Serikali itatwaa maeneo ya karibu na Bandari ya Tanga, ili kuongeza eneo la utekelezaji wa shughuli za Bandari?
Supplementary Question 2
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wapo wananchi wengi katika eneo la Kata ya Katende na Bukome katika Jimbo la Chato Kaskazini, ambao maeneo yao yalitwaliwa, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato. Mpaka sasa, karibu miaka saba hadi nane, hawajawahi kulipwa fidia yao, na wananchi wale hawana maeneo mengine ya kwenda kufanya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Spika, sasa kauli ya Serikali ni nini juu ya wananchi hao? Ni lini sasa wanakwenda kulipwa fidia yao, ili waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali? Ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na eneo lake na pengine, kwa sababu yanaweza kujitokeza maswali ya namna hii mengine, ni kwamba, tayari Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania imeshaanza kuandaa orodha ya maeneo yote ambayo tumeshayatazama, kama ni potential, ambayo ni muhimu, ili kutazama namna ya kuwalipa fidia wananchi hao na kisha tuweze kuyapangia matumizi.
Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane na mimi kwamba, tulikuwa na miradi mingi, Dar es Salaam mradi mkubwa, Tanga, Mtwara na kwenye Maziwa Makuu, kama vile Kigoma, Mbamba Bay kule Nyasa, Kemondo na kadhalika. Naomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda kidogo, siyo muda mrefu. Tutakapokuwa tumekamilisha tutakwenda kuipangia matumizi na kwenda kulipa maeneo yote ambayo pengine tulikuwa hatujakamilisha.
Name
Kijakazi Mohamed Yunus
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: - Je, lini Serikali itatwaa maeneo ya karibu na Bandari ya Tanga, ili kuongeza eneo la utekelezaji wa shughuli za Bandari?
Supplementary Question 3
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Tunafahamu kwamba, hakuna mpango wa Serikali ambao hauna timeframe kwa hiyo, na mimi ningependa kuuliza swali, kama ilivyo kwa Jimbo la Mheshimiwa Magembe kule Wilaya ya Kilwa, hususan eneo la Kilwa Masoko, wanakabiliana na changamoto ya namna hii.
Mheshimiwa Spika, upanuzi wa airport umeahidiwa kwa muda mrefu sana, maeneo ya watu yamechukuliwa na mpaka sasa hawajalipwa fidia, wananchi wale wanaendelea kuteseka. Napenda kufahamu, ni lini wananchi wa Kilwa Masoko watalipwa fidia ili waweze kuendelea na maisha yao? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Kijakazi amezungumza, ni kweli kabisa. Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo la Kilwa Masoko kuendeleza kiwanja kile, tulishatazama takribani wananchi karibu 600, na fedha tuliainisha. Siyo eneo hilo tu moja peke yake, tayari na maeneo mengine ya viwanja vya ndege nchini ambayo tumeona ni muhimu kwenda kuyaendeleza tumekamilisha kufahamu mahitaji, tumepeleka Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kulingana na upatikanaji wa fedha, tunakwenda kulipa fidia katika eneo hili.