Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chanzo cha maji kilichobebwa na mafuriko katika Kata ya Maore Same Mashariki?

Supplementary Question 1

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza ninaomba nirekebishe jina la Kijiji kimoja, siyo “Kadandu” ni “Kadando.”

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo yamewasilishwa hapa kidogo yananitia utata, siyaelewi, kutokana na hali halisi ya site ilivyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami kwenda site kuona hali halisi ilivyo? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Zuena kwa kazi nzuri, kwanza akiwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, kwa mchango wake wenye tija katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, ninafahamu kazi kubwa aliyoifanya katika ushawishi wake na Mradi wa Maji wa Same – Mwanga – Korogwe wenye zaidi ya shilingi bilioni 406 uliotekelezwa katika maeneo ya Same, katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, kwa ombi la Mheshimiwa Mbunge, Serikali dhamira yake ni kusikiliza changamoto za wananchi na kuchukua hatua. Serikali kupitia Wizara ya Maji, tuko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kujionea hali halisi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba ili tuweze kuchukua hatua kulingana na tathmini ambayo tutakuwa tumeifanya. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chanzo cha maji kilichobebwa na mafuriko katika Kata ya Maore Same Mashariki?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, nami niulize swali dogo la nyongeza. Hivi tunavyozungumza, miradi ya Bunda ya Maji ya kati ya yenye thamani ya shilingi bilioni saba imesimama. Mradi wa Wariku, Mradi wa Migungani kwenda Kaswaka, Mradi wa Kisangwa ambao maji yanaenda mpaka Chuo cha Kisangwa imesimama.

Mheshimiwa Spika, lini fedha zitakuja ili wakandarasi waendelee na kazi? Katika hili wala sitaki tuambatane wote kwa sababu Mradi mmoja alikuja akauzindua, sasa tunahitaji fedha ili miradi ya maji ikamilike, wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wapate majisafi na salama. Lini wataleta shilingi bilioni saba? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya, na ninatambua kwamba mimi pamoja naye tulikuwepo Jimboni kwake na tulifanya shughuli mbalimbali, lakini pia tunatambua kwamba tunayo miradi mingi ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba Mkandarasi alikuwa ana madai yake, alikuwa hajalipwa na tumeshapokea hati zake na tayari tumeshaziandaa kwa ajili ya kuziwasilisha Wizara ya Fedha. Tutakachokifanya ni kuongeza msukumo kuhakikisha kwamba fedha hizi zinafika kwa wakandarasi ili waweze kuendelea na mradi huu ambapo tunaamini utakapokamilika na maji yatakapotoka, wananchi wa Bunda wataweza kufurahia sauti ya Mbunge wao anapokuwa anawasemea. (Makofi)

Name

Zainab Rashid Kawawa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chanzo cha maji kilichobebwa na mafuriko katika Kata ya Maore Same Mashariki?

Supplementary Question 3

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaomba nianze kwa kuipongeza Wizara ya Maji kwa jitihada za kutumia maji ya Mto Rufiji kama Mradi wa suluhisho la kudumu la kutuletea maji katika Mkoa wetu wa Lindi ambapo sehemu nyingi zitanufaika. Mradi huu ni mpango wa muda mrefu, lakini bado haujaanza nadhani, kwa hiyo, unatupa tu matumaini.

Mheshimiwa Spika, swali langu sasa, kwa kuwa tunavyo vyanzo vingine vya mito ama vya maji ambavyo vinaweza vikatumika wakati tunasubiria mradi huu uje kuanza, kwa mfano katika taarifa…

SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali…

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: … Kijiji cha Nahama ambacho kina uhaba mkubwa wa maji, tuna vyanzo vya mapango ya Nang’ole katika Kijiji cha Nandete ambavyo vina maji ya kutosha. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutumia chanzo hiki kama suluhisho la muda, wakati tunaendelea kusubiria mradi mkubwa ambao unakuja?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali na umekuwa utaratibu wa Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kulingana na uhitaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini. Ombi la Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kupitia sekta ya maji tunalipokea badala ya kusubiria suluhisho la kudumu. Wananchi wa eneo lake wanahitaji kupata huduma ya maji na sisi tutaenda kufanya hivyo ili waweze kupata maji wakati tukiwa tunasubiri utekelezaji wa mradi mkubwa.