Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara za TARURA za Wilaya ya Makete zenye urefu wa Km. 680.3 kutoka shilingi bilioni 3.2 hadi shilingi bilioni saba?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza natumia nafasi hii kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri kuonesha kwamba trend ya maongezeko ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za TARURA Wilaya ya Makete, kwa niaba ya wananchi wa Makete, tunaishukuru sana Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami, bado kuna changamoto katika majimbo kwa sisi Waheshimiwa Wabunge hususan vijijini hata wa mjini. Kuna majimbo ambayo kilometa ni nyingi, lakini bajeti yake bado ni ndogo na kuna majimbo ambayo kilometa ni chache, lakini bajeti yao ni kubwa na hakuna uwiano wa fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, je, utaratibu upi uliowekwa na Serikali kutengeneza uwiano wa ugawaji wa fedha za ujenzi wa barabara za TARURA kwenye majimbo hayo?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa Wilaya ya Makete tuna changamoto kipindi hiki cha mvua. Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba kuna barabara ambazo zimekatika. Mfano, Barabara ya Mang’oto – Ibaga, Mlondwe, Kipengele, Ijangala – Igole, na Maliwa – Sunti. Ziko barabara nyingi zimekwama kipindi hiki. Ni nini maelekezo ya Serikali kwa Meneja wa TARURA, Mkoa wa Njombe pia na Wilaya ya Makete ili kutumia fedha za dharura (Emergency Fund) ziweze kujengwa na kukarabati barabara zipitike?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, hakika anawatendea haki wananchi wa Jimbo la Makete, anafanya kazi kubwa. Nimhakikishie tu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu mwaka 2021 mpaka leo mwaka wa fedha 2025/2026 imeendelea kuongeza bajeti za Mfuko wa Barabara kupitia TARURA.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mwaka wa fedha huu bajeti yetu ambayo tunaitekeleza ni shilingi bilioni 710.31, lakini bajeti ijayo imeongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 160.93 mpaka kufikia shilingi bilioni 871.24. Kwa hiyo, hii ni dalili ya wazi ya dhamira ya Serikali kuendelea kuongeza fedha za barabara ili kutatua kero za barabara kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Makete na baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto kubwa za barabara. Kuna tofauti ya fedha ambazo zinazopelekwa kwenye majimbo. Kwa sasa vigezo ambavyo vinatumika ni vitatu, kigezo cha kwanza ni urefu wa mtandao wa barabara katika eneo husika, kigezo cha pili ni idadi ya wananchi katika eneo husika na kigezo cha tatu ni hali ya uchakavu wa barabara.
Mheshimiwa Spika, sasa katika eneo hili tumegundua changamoto kwamba yako maeneo yenye hali tofauti za kijiografia, maeneo yenye milima mingi, mvua nyingi ambayo yanahitaji fedha zaidi za barabara. Hivi sasa tuko hatua za mwisho za kupitia formula ya mgawanyo wa fedha za TARURA kwenye wilaya tukizingatia sana hali ya kijiografia terrain, milima, mvua, mabonde na kadhalika ili barabara hizi ziweze kupata fedha ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha Jimbo la Makete ambalo lina milima, barabara zina kona nyingi, lakini mvua za kutosha tutahakikisha kwamba zinapata fedha ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali kila bajeti inatenga fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya dharura za barabara. Hivi sasa tunapoongea Serikali, tayari imeshatoa fedha zaidi ya shilingi 21,000,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizoharibiwa na mvua.
Mheshimiwa Spika, hii ni fedha ya bajeti ya dharura. Serikali itaendelea kutenga fedha hiyo ili kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatengenezwa zikiwemo barabara za Makete ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge, na tayari tunapeleka fedha za dharura.
Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Njombe na Wilaya ya Makete wahakikishe wanakamilisha tathmini na kuleta gharama zinazohitajika kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizokatika.
Name
Esther Nicholas Matiko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara za TARURA za Wilaya ya Makete zenye urefu wa Km. 680.3 kutoka shilingi bilioni 3.2 hadi shilingi bilioni saba?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, madaraja ya Nyasebe na lile la Kimoge kwenda Nyakisese yaliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime yamesababisha madhara makubwa sana ya kijamii na kiuchumi. Wiki iliyopita tu kuna raia walipelekwa na maji na wakapoteza maisha.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Daraja la Kimoge na Nyakisese limekuwa likitengewa fedha, lakini hamna utekelezaji, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kunusuru na ukizingatia kwamba ni la kiuchumi zaidi kuhakikisha fedha ambazo zimetengwa mwaka huu wa 2026/2027 takribani shilingi 900,000,000 zitapelekwa ili ziweze kukamilisha ujenzi wa lile daraja?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Esther Matiko kwa kuwawakilisha vyema wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini kwamba kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na za kijamii za usafirishaji zinaendelea kutekelezwa bila mkwamo wowote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bajeti ambayo imetengwa ya shilingi 900,000,000/= kwa ajili ya daraja hilo na barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, tutasimamia TARURA, lakini Ofisi ya ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuhakikisha zinapelekewa na kazi ya ujenzi inafanyika kwa wakati.
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara za TARURA za Wilaya ya Makete zenye urefu wa Km. 680.3 kutoka shilingi bilioni 3.2 hadi shilingi bilioni saba?
Supplementary Question 3
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Lipembe ambayo inatoka Mbinga Mjini – kikolo – Kihungu sasa hivi imeharibika, liko katika hali mbaya na haipitiki na maeneo yale ni maeneo ya milima.
Mheshimiwa Spika, pia eneo la Kihungu kuna kituo cha afya mara nyingi wagonjwa wanatakiwa wapelekwe katika hospitali la wilaya. Nini tamko la Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inatengenezwa sasa hivi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini. Hata hivyo, ni kweli kwamba barabara inayotoka Mbinga Mjini kwenda katika eneo alilolitaja ni barabara muhimu, na amekuwa akiifuatilia mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, tayari Meneja wa TARURA wa Mbinga na Mkoa wa Ruvuma wameshawasilisha taarifa ya mahitaji ya fedha ili kufanya matengenezo ya barabara hiyo. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunda pamoja na wananchi wa Mbinga Mjini kwamba Serikali ipo hatua za mwisho za kupeleka fedha ili matengenezo yafanyike na barabara hiyo iweze kutumika vizuri.
Name
Juma Ramadhani Mustafa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara za TARURA za Wilaya ya Makete zenye urefu wa Km. 680.3 kutoka shilingi bilioni 3.2 hadi shilingi bilioni saba?
Supplementary Question 4
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itafanya tathmini na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja katika Kata ya Igalula katika Kijiji cha Vumilia, katika Kata ya Kizengi – Kisuli – Ndaki, katika Kata ya Tula – Chatulieni – Mihama, katika Kata ya Mmale, Kijiji cha Mbulumbulu? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mustafa, lakini ninamhakikishia kwamba Serikali imeweka mpango mkakati kwanza wa kutathmini na kutambua maeneo yote yanayohitaji madaraja kote nchini. Tuna database ya kila Jimbo, kila Mkoa; eneo gani linahitaji daraja? Eneo gani linahitaji kalvati na eneo gani linahitaji Barabara?
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, wamekuwa wakiwasilisha hoja hizo na sisi TAMISEMI tumezichukua na tumeziweka kwenye database zikiwemo madaraja ambayo Mheshimiwa Mbunge wa Igalula amesema. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tuko hatua za mwisho za kutafuta fedha na kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga madaraja hayo kwa awamu ili yaweze kupitika vizuri. Ahsante sana. (Makofi)