Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Emanuel Qambaji Nuwas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuongeza muda wa marejesho ya Mikopo ya asilimia mbili kwa Watu wenye Ulemavu ili kujenga usawa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa watu wenye ulemavu wana changamoto ya kuweza kufika katika ofisi za umma kutokana na wengi wapo katika maeneo ya vijijini, je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia kuweza ku-access huduma za mikopo? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Emanuel Nuwas, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kwa namna anavyowasemea wananchi wa jimbo lake. Vilevile, nampongeza kwa namna anavyofuatilia maslahi ya watu wenye ulemavu katika upatikanaji wa mikopo ya 10%.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweka utaratibu: kwanza, tunazo Kamati za Mikopo ya 10% ngazi ya halmashauri, ngazi ya kata mpaka ngazi za vijiji. Pia tunao Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao moja ya kazi yao ni kuhakikisha wanawafikia watu wenye ulemavu wenye uhitaji, na vikundi vingine vya wajasiriamali kwa maana ya vijana na wanawake wenye uhitaji kutoa elimu, hamasa na kuwawezesha kupata mikopo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watu wenye ulemavu ambao hawawezi kufika katika ofisi za halmashauri, wanafikiwa kupitia outreach services. Pia tutaendelea kuboresha ili Maafisa Maendeleo na wataalamu wawafikie kwa ukaribu zaidi watu wenye ulemavu ili wapate fursa ya kupata mikopo ya 10%.
Name
Stella Ikupa Alex
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuongeza muda wa marejesho ya Mikopo ya asilimia mbili kwa Watu wenye Ulemavu ili kujenga usawa?
Supplementary Question 2
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, kwenye jibu la msingi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mikopo hii haina muda maalum wa urejeshwaji. Hata hivyo, huko site watu wenye ulemavu wamenyang’anywa bajaji kwa madai kwamba hawajakidhi masharti ya kurejesha mikopo hiyo ndani ya miaka miwili au mitatu.
Mheshimiwa Spika, je, nini kauli ya Serikali kwa zile bajaji ambazo zimeshanyang’anywa kwa watu wenye ulemavu kwa kigezo cha kushindwa kurejesha mikopo ndani ya muda uliokuwa umewekwa wa miaka mitatu au miwili? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri sana. Katika maelezo yangu ya msingi, nimesema mikopo ya 10% utaratibu wa marejesho hauna muda maalum, kwa maana kwamba kila mkopo unalipwa ndani ya mwaka mmoja au miwili au mitatu. Kila aina ya mkopo unategemea aina ya shughuli inayokwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano ziko shughuli za kilimo ambapo wakopaji, au wajasiriamali wanahitaji kufanya shughuli za kilimo na kuanza mavuno, maana yake wale hawawezi kupewa muda sawa na mtu anayefanya shughuli ya ujasiriliamali kama mama lishe au baba lishe. Pia wapo ambao wanakopa bajaji au pikipiki, wale tunakubaliana kwamba ndani ya miaka miwili au miaka mitatu wawe wamerejesha.
Mheshimiwa Spika, haimaanishi kwamba aliyekopeshwa pikipiki ni sawa na aliyekopeshwa gari, mfano lori kwamba naye atalipa ndani ya miaka miwili. Hiyo ndiyo maana ya utaratibu wa mikopo ya 10%, hauna ukomo maalum. Uko specific kulingana na aina ya mkopo na aina ya marejesho ya fedha na aina ya shughuli ya ujasiriamali ambayo inatekelezwa na kikundi husika. (Makofi)
Name
Rashid Mohamed Mtima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Mjni
Primary Question
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuongeza muda wa marejesho ya Mikopo ya asilimia mbili kwa Watu wenye Ulemavu ili kujenga usawa?
Supplementary Question 3
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Newala ni miongoni mwa halmshauri ambazo mikopo hii hupitia benki ya NMB. Upatikanaji wa mikopo hii kupitia benki ya NMB umekuwa wa shida sana mpaka sasa vijana, wanawake na walemavu kutoka Halmashauri ya Newala Mji, bado kuna ugumu sana wa kupata mikopo hii.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni haja ya kufanya ufuatiliaji na kufanya marekebisho ili kupitia benki hii, basi wananchi hao waweze kupata mikopo kwa wakati? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini. Ni kweli Serikali imeona changamoto: kwa mfano katika mikopo hii ya 10%, tangu tumeanza utaratibu mwaka wa fedha 2024/2025, zile halmashauri 174 ambazo tumeendelea na mfumo wa ukopeshaji kupitia halmashauri, zaidi ya 85% ya fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya mikopo zimeshakopeshwa ukilinganisha na 22% tu ya fedha zilizopitia kwenye benki ambazo zimekopeshwa kwenye halmashauri zile kumi zinazopitia utaratibu wa benki.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli kwamba kuna changamoto ya kasi ya upatikanaji wa mikopo kupitia benki kwa halmashauri zile kumi ambazo ziliwekwa kama pilot ikiwemo na Halmashauri ya Mji wa Newala. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari tumeshakaa na benki husika CRDB, NMB na wadau wengine kuona namna nzuri ya kuongeza kasi ya kutoa mikopo hii. Pia kuona namna nzuri ya kupitia utaratibu ili lengo la Serikali la kuwafikia wajasiriamali wote kupata mikopo kwa wakati ili waendelee na shughuli zao liweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanyia kazi na hivi karibuni tutaona matokeo makubwa na mabadiliko makubwa kwa halmashauri zote kupata fedha za mikopo mapema na wajasiriamali kunufaika mapema zaidi.
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuongeza muda wa marejesho ya Mikopo ya asilimia mbili kwa Watu wenye Ulemavu ili kujenga usawa?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa akina mama waliozaa watoto wenye ulemavu wanapata shida sana kulea wale Watoto, kwa sababu inakuwa ni vigumu kukopesheka katika makundi ya akina mama.
Mheshimiwa Spika, katika halmashauri zetu, kuna fedha za watu wenye ulemavu. Sasa ni kwa nini Serikali isiangalie uwezekano wa kuwajumuisha akina mama waliozaa watoto wenye ulemavu katika sheria husika ili waweze kukopeshwa na kuwalea watoto wao kwa ufanisi zaidi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wa Jimbo la Kilolo. Hata hivyo, naomba nimhakikishie tu kwamba kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Mikopo ya Ujasiriamali 10%, tunayo makundi matatu, kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba wanawake waliozaa watoto wenye ulemavu, wanawajibika kuwatunza na kuwalea, lakini wanawake hawa pia wanaweza wakanufaika kupitia dirisha la mikopo ya wanawake kwa asilimia nne na wakaweza kufanya shughuli za ujasiriamali na kuendelea kuwalea watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, pia, tunatumia fursa hii kuendelea kuwashauri akina mama au wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu, kwenda kueleza changamoto hizo kwenye halmashauri ili zifanye tathmini na kuona uwezekano wa kuwapa upendeleo maalum katika vikundi vya wanawake ili waweze kupata nafasi nzuri ya kulea watu wenye ulemavu, ahsante.