Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Makao Makuu ya TANAPA Kanda ya Magharibi utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninaishukuru Wizara, imeweka clear kwamba, ujenzi wa Kanda ya Magharibi itajengwa Bunda Mjini na tunashukuru kwa shilingi bilioni 1.8 ambazo zimetolewa. Ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri Halmashauri ya Mji wa Bunda ipo kwenye top ten ya halmashauri ambazo zinataabishwa na wanyama wakali. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanyama hao hawaendi kuwadhuru wananchi pamoja na mali zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Ninatambua Wizara imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza kuwalipa kifuta jasho wananchi 1,483 wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ambao walipata madhara kwenye mashamba na mali zao kutokana na wanyama wakali. Ninatambua zoezi limeanza, lakini linasuasua. Lini wananchi hao watalipwa ili hizo fedha ziweze kuwasaidia katika mambo mengine? Ahsante.
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ester Bulaya, lakini kabla ya kujibu, ninaomba nimpongeze sana kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya. Mara kadhaa yuko ofisini kwa ajili ya madai ya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, niseme tu, mikakati ambayo imewekwa na Serikali ni kuimarisha doria za mara kwa mara na kuongeza vituo vya ujenzi vya Askari. Lingine ni kutumia teknolojia ya kisasa kama vile drones, pikipiki zilizofungwa vifaa maalum, pamoja na ujenzi wa uzio wa umeme katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli alichosema Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi 1,423 wana madai yao, lakini kati ya hao 714 tayari wamelipwa fedha hiyo, na waliobaki ni madai ya wananchi 709 yenye thamani ya shilingi 361,000,727. Malipo hayo yanaendelea kulipwa hivi sasa.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved