Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariam Anzuruni Mungula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM A. MUNGULA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wanawake juu ya magonjwa ya tezi ya shingo (thyroid) na yanayosababisha ukomo wa hedhi?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa, tunafahamu kwamba tezi ya shingo na kukoma kwa hedhi, moja ni hali na nyingine ni ugonjwa unaotokana na upungufu au unachangia sana kwenye upungufu wa kubadilikabadilika kwa homoni kwenye mwili wa mwanamke, sasa swali langu la kwanza ni, kwenye huu upande wa kukoma kwa hedhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wanawake kipindi wanapitia hali hiyo, na wako makazini kwa sababu, inachangia sana katika kupunguza ufanisi na utekelezaji wa majukumu yao ya kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Serikali ina mkakati gani wa kuwahudumia wanawake ambao wanaathirika na ugonjwa wa tezi ya shingo wakiwa kazini? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninampongeza Mheshimiwa Mariam kwa kazi nzuri ya kuwatetea na kuwapigania wanawake wa Tanzania, hususan wafanyakazi. Ni ukweli usiopingika kwamba, tatizo la tezi ya shingo na ukomo wa hedhi wa akinamama unafanana sana katika dalili zake kwa sababu, vichocheo vya mwili vinavyosababisha utendaji kazi kwa mwanamke vinashabihiana katika kufanya kazi na mwanamke huyu anapitia hali hii katika ukuaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke ana stage tano za kukua: utoto, mwaka sifuri mpaka miaka 18; balehe, miaka 10 mpaka 19; uzazi, miaka 15 mpaka 49; na ana kipindi hiki ambacho ndiyo kina tatizo, miaka 45 mpaka 55 ambapo, tunaita ni perimenopause na menopause, kuelekea kukoma hedhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukoma hedhi kiukweli anakuwa na dalili nyingi ikiwemo dalili za kimwili, ambapo hutokwa na jasho sana na mabadiliko ya hali ya akili, kwa mfano kuwa na hasira sana na kuchoka mwili.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, anachotaka ni mkakati. Usitoe somo.

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mikakati ya Serikali ni kuwasaidia hawa wanawake ambao wanapitia katika hali hii, ambayo inafanya ufanisi wao wa kazi usiwe mzuri, uwasaidie katika muda wanaopita. Kwanza, kuwagundua mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba, hali hii inasababishwa na nini; na watumishi viongozi makazini, kwa maana wakuu wote wa kazi wafahamu kwamba, kipindi hiki anachopitia mwanamke miaka 45 mpaka 55 ni kipindi anachopata usaidizi wa afya ya akili. Pale anapokuwa na hasira sana au anashindwa kutimiza wajibu wake, basi aweze kusaidiwa. Hata kwenye ngazi ya familia, wenza wajue kwamba, mwanamke anapopitia katika hali hiyo, sio yeye, ni yale mabadiliko yanayotokea katika miaka 45 mpaka 55 ndio yanamfanya awe hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili. Serikali imeendelea kuboresha huduma za uchunguzi na hapa ninampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka vifaa vya uchunguzi katika hospitali zote nchini ikiwemo hospitali za halmashauri na kuwagundua wanawake hawa wenye tezi ya shingo kwenye kupima damu, kwa maana ya biochemistry, kucheki T3 na T4, ambayo inafanyika katika ngazi ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, uchunguzi wa ultrasound ambapo utaweza kuonesha ukubwa wa tezi ya shingo na aina ya tezi ya shingo na hivyo kugundulika mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, nawasihi wanawake wote wa Tanzania, hususan wanapokuwa wanapitia miaka hii 45 na 55, hali hiyo siyo ugonjwa, ni mabadiliko. Wafike hospitali mapema na watapata matibabu kwa sababu, ni hali ambayo ni ya mpito. Ahsante.