Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 1

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, nikiri kwamba kupitia kwa Waziri Mkuu wakati ninauliza swali langu la papo kwa papo kuhusiana na suala hili, alitoa majibu mazuri sana na maelekezo yanayotoka kwa Serikali akizitaka shule hizo na walimu waweze kusitisha mara moja hiyo michango holela, lakini maelekezo haya, huko chini hayapo katika uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari sasa kutoa waraka mwingine maalum wa kuzitaka shule hizi kusitisha mara moja michango hii ambayo kimsingi inawatesa sana watoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tutakubaliana kwamba kimsingi michango hii ambayo inatozwa huko mashuleni ilipaswa kubebwa na ruzuku kwa maana ya capitation grant inayotolewa na Serikali kwenda kwenye hizi shule za msingi na sekondari ili kuziwezesha kujisimamia, lakini ruzuku ni ndogo sana, na ilipitishwa miaka mingi sana. Shule ya msingi wanapewa shilingi 10,000 na shule za sekondari shilingi 25,000. Katika hali ya kawaida hakuna namna shule hizi zinaweza zikajiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maisha kupanda, mfano, mambo ya manunuzi yamepanda, na hivyo kiasi hicho kimekuwa kidogo, je, ili kumsaidia huyu mzazi, Serikali ipo tayari sasa kupandisha ile ruzuku ya shilingi 10,000 kwa shule za msingi na shilingi 25,000 kwa sekondari? Ninaomba kusikia tamko la Serikali kwamba iko tayari kupandisha hizi ruzuku ili ziende kusaidia hizi shule ziweze kujisimamia.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Segerea, kwa kweli anawatendea haki wananchi wa Jimbo la Segerea, anawasemea kwa dhati kabisa. Nimhakikishie kwamba Serikali hii sikivu itaendelea kushirikiana naye na wananchi wa Segerea kuhakikisha miradi ya maendeleo na huduma za kijamii zinaendelea kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mbunge kwamba maelekezo ya viongozi wetu wa Kitaifa tunayatekeleza kwa uthabiti wa hali ya juu. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba alishatoa maelekezo hayo, na sisi tayari tumeshatoa maelekezo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na tunasimamia utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri yoyote ambayo itakiuka maelekezo hayo, Serikali itachukua hatua za kinidhamu dhidi yake. Kwa hiyo, hilo nikuhakikishie kwamba linasimamiwa na Serikali kwa ufanisi unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kweli kwamba tunahitaji kuendelea kuboresha huduma za elimu ya msingi. Serikali inatoa ruzuku na elimu inatolewa bila ada, lakini kuna component ya cost sharing kwa wazazi, angalau kuchangia kwa makubaliano rasmi na kwa michango ambayo imekubalika kwenye Kamati, Bodi za shule, vikao rasmi vya wazazi na Mkuu wa Wilaya husika kujiridhisha kwamba mchango huu siyo holela na ni mchango ambao unaboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tutaendelea kuwashauri wananchi wetu kuwa na wajibu wa angalau kushiriki katika kutoa elimu wakati Serikali inatoa ruzuku kwa kiasi kikubwa na elimu bila ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie, msimamo wa Serikali mpaka sasa, michango hii yote haitakiwi kuathiri utaratibu wowote ambao umetolewa. Kwa mfano, kwenye joining instruction kwa wanafunzi wa bweni, na pili, hakuna mwanafunzi yeyote ambaye anatakiwa kukosa masomo au kuzuiliwa kwenda shule hata kama mzazi wake hajafanikiwa kuchangia mchango uliokubalika rasmi na wazazi, kamati au bodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na makubaliano, hakuna mwanafunzi ambaye anatakiwa kukosa fursa ya kusoma. Wanafunzi wote waende wakasome bila kujali amechangia, au hajachangia kwa sababu elimu ni kipaumbele nambari moja.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 2

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Waheshimiwa Wabunge hapa watakuwa mashahidi kwamba jambo hili la wazazi kuchangia huko chini linaendelea kila mahali, kila siku na kila Mkoa. Ninadhani tatizo lililopo hapa ni utaratibu tuliouweka wa hizo kamati na bodi ndizo ambazo pamoja na majibu hapa, Waziri Mkuu ameelekeza, Serikali inaelekeza hii michango inaendelea kule na madhara yake ni makubwa sana. Sisi Wabunge ni mashahidi tunaosumbuliwa na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari kubadilisha huu utaratibu wa hizi bodi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la kupitisha hii michango lifutwe. Kama hii fedha inakuwa inapitishwa hapa, inapelekwa kule, na bado hii michango ipo kule, na wakati mwingine watoto wanazuiliwa kwenda kufanya mitihani na kwenda madarasani. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kwa hili swali muhimu. Ninarejea kusisitiza kwamba Serikali inaendelea kutoa ruzuku na elimu bila ada, lakini pia tunataka kujenga angalau utamaduni wa wazazi kuwa sehemu ya kuchangia elimu za watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa-exclude wazazi kwa 100% wasishiriki kabisa katika elimu za watoto wao, tunaweza tukajenga utamaduni ambao mwisho wa siku utakuwa na changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ni kwamba lazima michango yote iwe na sababu za msingi, lakini iwe rasmi kupitia kamati, bodi na Mkuu wa Wilaya ajiridhishe. Ile michango ya shule za bweni, ni lazima Ofisi ya Waziri Mkuu ijiridhishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, tunachukua wazo la Mbunge Nape Moses Nnauye, tutaendelea kulitafakari na kuona namna ya kuboresha ili tuhakikishe tunaondoa kero hizo. Pia tunaboresha elimu katika ngazi ya msingi kote nchini.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 3

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuna baadhi ya maeneo wale watoto ambao wazazi wao au walezi hawakufanikiwa kuchanga chakula wakati wenzao wanakula wanafungiwa kwenye chumba fulani, wenzao wakimaliza kula wanawafungulia wanaenda kuwafundisha. Jambo ambalo kisaikolojia mtoto huyu hawezi kuelewa kabisa kwa namna hiyo. Je, nini kauli ya Serikali katika maeneo ambayo kuna hivi vitendo vya udhalilishaji kufanyika dhidi ya wanafunzi hao? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jambo hilo nimelipata hapa kwa Mheshimiwa Waitara, na ninaomba nilipokee, tutafuatilia kuona shule zipi ambazo zinafanya utaratibu huo? Huo utaratibu haukubaliki na wala siyo wa kiungwana, na ninafikiri wanakwenda hata kinyume na haki za mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunalipokea, nitoe maelekezo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kwamba Wakuu wa Shule, Wakurugenzi na Viongozi wote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa yetu, wahakikishe wanafuatilia kwa karibu suala la chakula cha wanafunzi mashuleni ili waweze kuwa na afya njema na wajifunze vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wazazi kama wazazi, wanachangia katika maeneo hayo, uwekwe vizuri kwa kila mzazi kushiriki kwa namna inavyowezekana ili mtoto apate haki sawa na watoto wote wapate chakula shuleni na waweze kupata masomo kwa usawa unaotakiwa.

Name

Morris Joseph Makoi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 4

MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nilikuwa ninaomba kama Waziri wa TAMISEMI anaweza akatusaidia kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi na sekondari zinatumia mashamba waliyonayo kulima chakula kwa ajili ya kuwapunguzia wazazi hizi gharama za kuchangia, hasa kwa kuzingatia umaskini ambao upo vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri zetu kama Wakurugenzi wakielekezwa, wanaweza wakatenga fedha wakawasaidia wale walimu kununua mbegu na pembejeo nyingine, na wanafunzi wakashirikishwa, wakalima na mwishoni wakavuna chakula cha kutosha na pengine hili jambo la kila mara Serikali inatoa mwongozo, na mwongozo hauzingatiwi lingeweza likamalizika. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, ni ushauri mzuri, lakini nimhakikishie tu kwamba Serikali kupitia mapitio ya Sera ya Elimu ya 2014, Toleo la 2023, limeweka utaratibu mzuri sana wa kuboresha mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na elimu ya kujitegemea iliyoboreshwa zaidi ambayo itahusisha maeneo ya ujasiriamali, uzalishaji, kilimo, ufugaji, lakini tutakuwa tuna maeneo ya elimu ya amali ya kihandisi na isiyo ya kihandisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunapoelekea kutekeleza sera mpya ya elimu, haya mambo yote tutayachukua kwa maeneo ambayo wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji, watafanya shughuli hizo kujenga uwezo wa watoto, pia kuwezesha kupunguza gharama za michango.

Name

Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 5

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kimsingi masuala haya ya kuchangisha wazazi kupitia shule zetu nchini hayawezi kuepukika kwa baadhi ya maeneo. Kwa mfano, walimu wanaojitolea sasa hivi katika shule zetu nchini ni wengi sana ambao hawajaingia kwenye mfumo wa ajira na ile michango yao inachangwa na wazazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kufanya mapitio upya ya maeneo ambayo yangeruhusiwa kwa mfumo usio rasmi kuchangia ama kwa namna nyingine yoyote ili kuleta uwiano wa kutoa huduma hii ya nafasi ya kufundisha kwa wanafunzi wetu nchini?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishapitia na itaendelea kupitia kwa kadri itakavyohitajika na kutoa miongozo na maelekezo ya maeneo ambayo Kamati, Bodi na Vikao na mikutano rasmi ya wazazi inaweza ikafikiria kuchangisha ikiwa kutakuwa kuna ulazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaacha dirisha wazi kwamba kila mchango uchangishwe, na ndiyo maana tumeweka utaratibu na Mkuu wa Wilaya na Serikali yake wanajiridhisha kwamba mchango huu ni sehemu ya michango ambayo inaweza ikawa na tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Issaay kwamba, tutaendelea kuboresha, na ikiwa kuna maeneo, kuna michango holela na isiyokubalika, tutachukua hatua ili kudhibiti michango holela katika maeneo hayo.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 6

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa makundi ambayo yanatajwa yanapaswa kujiridhisha kwa ile michango muhimu mahsusi ikiwemo Wakuu wa Wilaya na wazazi, lakini kundi la Wabunge halijatajwa ambalo ndilo wanapelekewa malalamiko hayo, na ambao ndio wako kwenye mikutano ya hadhara, wananchi wengi wanajitokeza kulalamikia michango holela katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, je, Serikali ipo tayari kuwahusisha Wabunge kuwa sehemu katika suala zima la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba michango hiyo ni ya msingi kwa wakati mahsusi? Ahsante sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kupitia Kamati za Kudumu za Mabaraza ya Madiwani, ipo Kamati ya Elimu, Afya na Maji ambayo Wabunge wanaweza wakashiriki kupitia eneo hilo kwa kofia ya kuwa Baraza la Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mabaraza ya Madiwani wanaweza wakashiriki kupitia michango hiyo, lakini kwa nafasi zao wenyewe kama Mbunge mwenyewe, anayo haki ya kupitia michango na akiona hiyo michango inaleta kero katika eneo hilo anaweza akashauriana na mamlaka husika, na pia akafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Kwa hiyo, wazo la Mheshimiwa Mbunge ni sahihi na mfumo huo upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwaombe, kama kuna maeneo katika Majimbo yetu tunaona kuna michango ambayo ni kero na ni michango holela, tunaomba kupata taarifa ili tuweze kuchukua hatua kwa utaratibu ambao Serikali imeuweka.

Name

Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?

Supplementary Question 7

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, sera inasema ni elimu bila malipo, wala siyo cost sharing, na kwa kuwa wananchi wamekuwa wakichangishwa fedha nyingi hasa kwenye suala la chakula hadi shilingi 400,000 na shilingi 500,000. Je, Serikali sasa iko tayari kuongeza bajeti ili twende kwenye sera ya elimu bila malipo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke taarifa sawa kwa Mheshimiwa Simon Songe, kwamba siyo elimu bila malipo, hakuna utaratibu wa elimu bila malipo. Kwa Mwongozo ule wa Mwaka 2016, ni elimu bila ada. Kwa hiyo, haya ni mambo mawili tofauti. Serikali inatoa ruzuku kwa wanafunzi wote kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, wanasoma bila kulipa ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko gharama ndogo ndogo ambazo kamati, wazazi na bodi wakiona inafaa, kama wajibu wao kama wazazi, wanatumia fursa hiyo kuboresha elimu, na tunaendelea kusimamia kuepuka kutoa michango ambayo ni holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kuboresha ruzuku kwa ajili ya kuboresha elimu katika maeneo haya. (Makofi)