Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 9 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) | 91 | 2026-04-15 |
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -
Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la Wazazi kuchangia Mitihani, Masomo ya Ziada na Chakula Shule za Msingi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Jimbo la Segerea, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2016 Serikali ilianza utekelezaji wa Elimu Msingi bila ada kupitia Waraka wa Elimu Namba Tatu wa mwaka 2016. Waraka huu pamoja na mambo mengine, unabainisha majukumu ya mzazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mtoto anapata vifaa vya kujifunzia, sare za shule, chakula na huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kuboresha ujifunzaji na ufundishaji ikiwa ni pamoja na ustawi wa wanafunzi, Kamati na Bodi za Shule kupitia vikao vya wazazi zimekuwa zikianzisha michango mbalimbali. Ili kudhibiti michango holela, Serikali imekuwa ikiwaelekeza viongozi wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa michango ya aina yoyote inaridhiwa kupitia vikao rasmi vya wazazi na kamati au bodi za shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa wanafunzi wa bweni, Serikali imeweka katika fomu za maelekezo ya kujiunga (joining instructions) mahitaji na michango muhimu ambayo mwanafunzi anatakiwa kwenda nayo shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifuatilia kuhakikisha kuwa hakuna michango holela; na kiongozi au mwalimu yeyote anayebainika kuanzisha michango iliyo kinyume na utaratibu, hatua za kinidhamu na za kiutawala zimekuwa zikichukuliwa. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved