Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fadhili Fabian Ngajilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 1

MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kutujengea soko hili la Machinga Complex ndani ya Iringa Manispaa. Kwa kweli jambo hilo litakuwa limefurahisha sana wananchi wa Iringa Mjini na tupo tayari kutoa ushirikiano kwa ajili ya ujenzi wa hilo soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi pia kwamba masoko ya namna hii, sehemu nyingi za nchi yetu yakijengwa huwa yanatelekezwa na machinga wenyewe au wafanyabiashara kwa sababu wanakuwa hawakushirikishwa wakati wa ujenzi, na usipomshirikisha mfanyabiashara maana yake atashidwa kujua afanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Wizara inanihakikishiaje kwamba kabla ujenzi huu wa hili soko itawashirikisha wadau wakubwa wa ujenzi ambao ni machinga wenyewe wa Iringa Manispaa katika huu ujenzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa mradi huu utaanza kujengwa? Ninashukuru kwa majibu mazuri, lakini ni lini sasa mradi huu utaanza kujengwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, ninapokea pongezi nyingi za Mheshimiwa Ngajilo kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita na ni hakika kwamba Serikali hii imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa miundombinu ya masoko, stendi na miradi mingi ya kimkakati na zoezi hili linaendelea kutekelezwa kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Ngajilo kwamba katika ujenzi wa miradi yote ya kimkakati, jambo la kwanza halmashauri zenyewe, mabaraza ya madiwani, na Mkurugenzi lazima wawashirikishe wadau wa eneo husika. Kwa hiyo, ninatumia nafasi hii kukuhakikishia kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutashirikiana kwa karibu na Mkurugenzi wa Manispaa na Baraza lake la Madiwani katika Manispaa ya Iringa kuwashirikisha wadau, wafanyabiashara wadogo na machinga kuridhia eneo hili na aina ya majengo na mpangilio wa majengo kwa bidhaa husika ili wafanyabiashara hawa wapate eneo mwafaka kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla hatujaanza ujenzi, tutajihakikishia kwamba tumepata consensus ya pamoja, tumekubaliana, na ujenzi utaanza ili soko hili lisitelekezwe, liwe na tija kama yalivyo malengo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tayari kwa mwaka wa fedha ujao 2026/2027 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza, lakini tunamwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuandaa andiko la mradi wa kimkakati, wawasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tulifanyie tathmini, lakini waendelee kutenga fedha kwa awamu kwenye mapato ya ndani wakati Serikali Kuu inatafuta fedha kuwaunga mkono kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 2

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina soko maarufu linaitwa Soko la Azimio, soko lile ni la muda mrefu na miundombinu yake siyo rafiki. Wakati wa mvua soko lile linavuja na wafanyabiashara wanatamani kufanya biashara sehemu salama kwa ajili ya usalama wa biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kujua, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha na sisi Tunduru tunapata soko zuri na rafiki kwa wafanyabiashara? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mpango na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunaboresha miundombinu ya biashara kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumsisitiza na kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwamba, kipaumbele cha soko ni cha juu katika halmashauri yoyote kwa sababu, kwanza kinaboresha huduma za jamii, na pia, ni chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza wafanye tathmini ya gharama zinazohitajika katika ujenzi au ukarabati wa soko hilo. Pili, walete huo mradi wa kimkakati Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Tatu, waanze kutenga fedha kwa awamu kwenye mapato yao ya ndani, kwa ajili ya kuanza ujenzi na ukarabati wa soko hilo wakati Serikali Kuu ikiona uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi na ukarabati. (Makofi)

Name

Jonas William Mbunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 3

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itaanza kujenga soko la kisasa kwa Mji wa Mbinga, kupitia Mradi wa TACTICS ambao ulitakiwa utekelezwe kwa awamu ya tano?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunda amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na ujenzi wa soko la kisasa katika Mji wa Mbinga. Ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali hii kwa kuthamini umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya biashara katika Mji wa Mbinga, imeuingiza mji huo kwenye Mpango wa TACTICS Awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa taratibu za tathmini na manunuzi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo zinaendelea. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mbinga Mjini kwamba, mara baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi na tathmini, tutapeleka wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa soko pamoja na miundombinu mingine iliyopangwa.

Name

John Stephano Luhende

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 4

MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Ninapenda kuuliza swali kwa Serikali, ni lini sasa mtaanza ujenzi wa soko pamoja na stendi katika Jimbo letu la Bukene? Maana jimbo hilo halina stendi pamoja na soko. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bukene ni moja ya maeneo ambayo yana uhitaji wa stendi na soko. Mheshimiwa Mbunge katika kipindi hiki kifupi amekuwa anafuatilia mara kwa mara Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bukene kwamba, hiyo ni dhamira na mpango wa Serikali kwenda kujenga miundombinu ya masoko na stendi katika maeneo yote yenye sifa hizo kwa awamu. Tutaendelea kutoa kipaumbele katika eneo la Bukene kwa kadiri tunavyopata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninatumia nafasi hii kusisitiza kwamba, Wakurugenzi wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni lazima wawe na vipaumbele ambavyo ni mahitaji ya wananchi. Katika kila mipango yao ya bajeti ya kila mwaka wahakikishe angalau wana-reflect kwa kuanza kutenga kiasi kidogo cha fedha, kwa ajili ya shughuli hizo wakati Serikali ikiwa inatafuta fedha kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo.

Name

Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 5

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Mafinga tulipata mradi wa stendi ambayo ilikuwa ikamilike kujengwa mwaka uliopita, lakini mpaka sasa tunaambiwa kwamba, wakandarasi wapo kwenye hatua za drawings. Sasa naomba nipate kauli ya Serikali kwamba, ni lini stendi hii itajengwa kwenye Mji wa Mafinga ambao mpaka sasa hatuna stendi ya kisasa na tunaihitaji sana? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Serikali iliweka mpango kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa katika Mji wa Mafinga na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Villa, amekuwa akifuatilia mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie kwamba, kama alivyosema, tayari tuna mkandarasi, lakini kazi haijaanza na tunajua kuna sababu ambazo zimesababisha mkandarasi kutokamilisha kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mafinga tuko kwenye hatua za kuhakikisha mkandarasi anarejea kazini, anaanza kufanya kazi hiyo, ili kukamilisha ujenzi wa sehemu hiyo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi hiyo itafanyika.

Name

Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 6

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Nyehunge ni Makao Makuu ya Jimbo la Buchosa, lakini hauna soko la uhakika. Hivi karibuni tumeandika mradi wa soko ambao ni wa shilingi bilioni nne, na tumepewa ahadi ya kwamba, fedha hizo zitaletwa tuweze kujenga soko letu. Je, fedha hizo zitakuja lini tuweze kukamilisha ujenzi wa soko hili?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Mji wa Nyehunge katika Jimbo la Buchosa ni mji ambao una sifa ya kujengewa soko la kisasa na Mheshimiwa Eric Shigongo amefuatilia kwa muda mrefu. Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imeweka kwenye mpango, na tunatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko hilo kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kufanya hivyo, lakini pia, Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Baraza lake la Madiwani waendelee kutenga fedha kwa awamu, ili waanze ujenzi wakati Serikali Kuu inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuwaunga mkono.

Name

Ramadhani Hamza Singano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 7

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Soni ni miongoni mwa miji mikubwa kibiashara kwa Jimbo la Bumbuli. Ni lini Serikali itafikiria kuwa na soko la kimkakati, kwa ajili ya kuongeza uchumi na kipato kwa wananchi wa Bumbuli?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yenye sifa za kujengewa miundombinu ya stendi, masoko na miundombinu mingine inaendelea kujengwa kwa awamu. Wajibu wa halmashauri ni kuandaa maeneo, kuandaa michoro, kuandaa makadirio na kuanza kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi na kuwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ili Serikali pia iendelee kuandaa bajeti, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Bumbuli, Engineer kwamba, tunatambua suala hilo. Serikali hii itakwenda kulitekeleza, lakini halmashauri pia waanze kutenga fedha kwa awamu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Name

Cosmas Mtesigwa Bulala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwimba

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 8

MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya TAMISEMI. Mji wa Ng’hungumalwa ni wa kibiashara katika Wilaya ya Kwimba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa soko la kisasa katika kata hii na Mji wa Ng’hungumalwa, ambapo mwaka 2025 iliidhinishwa shilingi bilioni 3.9, kwa ajili ya kujenga stendi katika Mji wetu wa Ng’hungumalwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, miundombinu hiyo ni kipaumbele cha Serikali. Serikali inatambua uhitaji wa miundombinu hiyo, kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge na halmashauri kuhakikisha tunaanza kutenga fedha kwa awamu na kuhakikisha kwamba, tunajenga miundombinu hiyo.

Name

John John Nchimbi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 9

MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumwuliza swali kwamba, je, ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na yenyewe itakumbukwa walau kupata kimojawapo kati ya stendi au soko, kama ambavyo zinapata halmashauri nyingine zenye historia kubwa katika Taifa hili, kama Wilaya ya Nyasa? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Nyasa, Jimbo la Mheshimiwa John John Nchimbi, ni moja ya halmashauri mpya ambazo kwa kiasi kikubwa hazina miundombinu wezeshi, kama stendi na masoko. Serikali imeendelea kuweka mpango mkakati wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, miundombinu hiyo inajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, safari ni hatua, tunaendelea kwa awamu na tutahakikisha Halmashauri ya Nyasa inapata miundombinu hiyo muhimu.

Name

Fagason Aron Nkingwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 10

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa sababu, Jimbo langu la Mbogwe lina kata 17, lakini ipo Kata ya Masumbwe yenye wakazi zaidi ya 100,000 na ni kata yenye wafanyabiashara wengi, je, ni lini sasa Serikali itakuja kujenga soko la kisasa kwenye Kata ya Masumbwe?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za masoko ni muhimu, hasa kwenye miji yenye wafanyabiashara wengi, ili kuwawezesha kufanya biashara vizuri na pia kuboresha huduma na mapato ya ndani ya Halmashauri. Kwa hiyo, ninatumia nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Fagason.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii pia, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe, kupitia wataalamu wake na Baraza la Madiwani kukaa na kutathmini, kutafuta eneo na kuona uwezekano wa kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu, lakini pia kuleta taarifa rasmi na andiko la mapendekezo hayo Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ili kwa pamoja Serikali ione namna ya kuendelea kuboresha ujenzi wa masoko katika maeneo hayo.

Name

Mabula Johnson Magangila

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?

Supplementary Question 11

MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Nami naomba niulize swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala. Kwa kuwa, Mji wetu wa Kakola, unakua kwa kasi sana, yaani Bulyang’ulu, ambapo ninafahamu wewe pia ni mwenyeji sana pale, kuna mahitaji makubwa sana ya soko pamoja na stendi. Je, ni lini Serikali itakwenda kuanza ujenzi wa soko na stendi pale Kakola? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mabula, Mbunge wa Jimbo la Msalala kwamba, Msalala ni moja ya halmashauri ambayo inakua kwa kasi na ina wafanyabiashara wengi, na kwa kweli kuna kila sababu ya kuendelea kuboresha miundombinu ya stendi na soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Halmashauri, kwa maana ya Halmashauri ya Msalala na Serikali Kuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutaendelea kufanya tathmini, kuandaa michoro na kutafuta maeneo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi na masoko kwa awamu. Dhamira ikiwa ni kuhakikisha kwamba, huduma hizo zinaboreshwa katika Halmashauri ya Msalala. (Makofi)