Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza: - Je, lini malipo ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi (SPM Mgololo) yatafanyika, ukizingatia kuwa ni ya muda mrefu sana?

Supplementary Question 1

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wafanyakazi hawa wa Kiwanda cha SPM - Mgololo walishinda kesi ya msingi mwaka 2007 na katika kesi hiyo ya msingi Mahakama iliamuru wadai hawa walipwe kwa pande zote mbili, kwa maana ya mwekezaji kwa wale wafanyakazi wachache aliokuwa amewachukua, lakini na Serikali iwalipe wale wafanyakazi 760 ambao walikuwa hawajapewa barua ya kusitishiwa ajira yao na wala hawaendelei na kazi; kwa maana kwamba walikuwa wameachwa hewani. Mahakama ikaamuru kwamba walipwe tokea mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; sasa je, Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro ili Watanzania hawa ambao walifanya kazi kubwa ya uzalishaji katika kiwanda kile, katika kujenga nchi yetu na wao wakapata haki yao ambayo wameitumikia kwa muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Rais wetu mpendwa kupitia Bunge hili alisema anatamani wakati anaondoka, angeacha tabasamu kwa Watanzania. Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro kwa kuona ni namna gani wanawafidia wafanyakazi wale ambao kwa kipindi kirefu sasa wanaisubiri hii fedha na kiwanda kile kilikuwa kikifanyiwa kazi na Watanzania kutoka nchi nzima na wanashindwa kuondoka Mgololo kwa sababu wamefanya kazi muda mrefu, hawana fedha na hawajapata mafao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba majibu ya Serikali. (Makofi)

Name

Denis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi na utu ndiyo kaulimbiu yetu na tabasamu la utu katika utumishi ni moja ya malengo ambayo tunayafanyia kazi chini ya maelekezo yake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wetu. Kwa muktadha huo, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lutevele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaingia hapa kwa sababu yenyewe ndiyo ilikuwa mmiliki wa kiwanda hiki kabla ya ubinafsishwaji wake. Kimsingi ninaomba nikiri kwamba madai haya chimbuko lake ni kupunguzwa kazi kwa baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hiki na mwekezaji ameshalipa madai ambayo yanayomhusu kwa upande wake. Uhakiki ulifanyika kwa upande wa Serikali katika dhana ile ile ya kuacha tabasamu la utu na tayari Serikali ilifikia tamati kwa kupata kiwango cha fedha ambacho ni malipo stahiki kwa watumishi wa kiwanda hicho. Serikali ilitoa fedha hizo katika mwaka 2017 na 2018. Hata hivyo, wafanyakazi hao walikataa kuchukua kiasi hicho kwa madai kwamba ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Serikali imeshtakiwa na suala hili bado liko Mahakamani na kinachogombewa hapa ni kwamba, kiwango ambacho kimetoka ni kidogo, lakini nia ya Serikali ni kumaliza mgogoro huo ili wananchi hawa wapate haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.