Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Catherine Canute Joachim
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuendeleza utalii wa tiba nchini ili kuboresha huduma za afya na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika pato la Taifa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuendeleza tiba ya utalii, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo imepanga ifikapo mwaka 2050 pato la Taifa linatarajiwa kuwa dola trilioni moja na inatarajiwa kuwa sekta binafsi itakwenda kuchangia 70%, swali langu ninataka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha hospitali za sekta binafsi zinashiriki vipi katika kuchangia pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tunafahamu kwamba nchi ambazo zimefanya vizuri katika utalii wa tiba kama vile Afrika Kusini, India, Morocco na Thailand zimefungamanisha utalii wa tiba na talii nyingine kama vile utaii wa fukwe za bahari, utalii wa tiba mbadala kama wellness program au AUVEDC nilikuwa ninataka kufahamu nini mkakati wa Serikali wa kufungamanisha utalii wa tiba hapa nchini na utalii mwingine?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Dkt. Catherine Joachim kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi, lakini kipekee jumuiya yake anayoiwakilisha Jumuiya ya Wazazi Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya afya ambao huo ndiyo umevutia utalii wa tiba na si hivyo tu, tumemsikia Mheshimiwa Rais ameelekeza ipitiwe sera ya PPP ili tuweze kufanya kazi vizuri na sekta binafsi kwa sababu ndiyo ambayo itakwenda kuchangia pato la Taifa kwa 70%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoendelea kutekeleza tiba utalii tunafanya kazi kwa sasa na hospitali saba na kati ya hizo hospitali tano ni za Serikali, lakini tunafanya kazi na hospitali binafsi mbili. Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi na hizo hospitali binafsi tayari, tunayo timu ya kitaifa inayoratibu tiba utalii nchini, timu hii imeunganisha sekta zote, kama tunavyofahamu utalii ni suala mtambuka, mtalii anapofika kwanza anahitaji viza, anahitaji asafiri kwa hiyo, Wizara zote zinahusika na tunafanya kazi na Wizara zote kuhakikisha kwamba watalii hawa wanaweza kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tumeshaandaa mwongozo na sasa tupo tunaandika mkakati na upo mbioni kukamilika, mkakati ambao utakwenda kuweka mazingira rafiki sana kwa sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sekta binafsi, mazingira wezeshi tayari yameshawekwa na Awamu ya Sita kwa kuweka miundombinu mizuri, kwa kuweka vifaa vizuri na kuwasomesha Watanzania ambao wanaweza kutoa hizo huduma bobezi. Hivyo, ni jukumu la Watanzania kuchangamkia fursa hii ya kufanya kazi hii ya utalii tiba na sisi tupo kwa ajili ya kuwaratibu na kuwawezesha ili waweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake namba mbili, zipo nchi zinazofanya vizuri, ni kweli kabisa, Singapore, Thailand, India wanafanya vizuri na sisi kama Serikali tunaendelea kujifunza kutoka kwenye nchi hizo. Ni hivi karibuni wataalam kutoka Misri walifika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kwa mara ya kwanza walifanya operation kubwa ya mshipa mkubwa wa moyo kwa maana ya aorta.
Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri. Hata hivyo madaktari wetu wameendelea kufanya kambi za tiba katika nchi mbalimbali ili kuendelea kujifunza na kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na taasisi zote ili ku-brand. Ili ufanye vizuri katika utalii lazima ujitangaze, unatangazaje? Kwa kwenda na kuhusisha hizo nchi mbalimbali. Katika mkakati huo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kufungamanisha, ndiyo maana umeona tunafanya kazi na Maliasili kupitia Bodi ya Utalii, ndiyo maana unaona sasa hivi ukipanda SGR pamoja na kutangaza mbuga unatangaziwa pia hospitali zetu, unatangaziwa vifaa vyetu, unatangaziwa huduma tunazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakwenda kufungamanisha huduma zetu na tunakwenda kushirikiana na nchi zilizofanya vizuri zaidi ili na sisi tuweze kufanya vizuri katika utalii tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Ibrahim Mohamed Shayo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuendeleza utalii wa tiba nchini ili kuboresha huduma za afya na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika pato la Taifa?
Supplementary Question 2
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana, ulipokuja Moshi uliwaahidi wananchi wenzangu wa Moshi kwamba Serikali itakwenda kujenga mortuary ya kisasa. Je, ni lini mortuary ile inakwenda kujengwa?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ibrahim, Mbunge wa Moshi kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwapigania wananchi wa Moshi. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekwishakupeleka shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mortuary pale Moshi na mkandarasi ameripoti site wiki iliyopita na tumesema kwa kazi nzuri aliyofanya Mheshimiwa Mbunge pindi ujenzi utakapoanza atakwenda yeye mwenyewe kuweka jiwe la msingi katika mortuary ile ya Hospitali ya Mawenzi.
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuendeleza utalii wa tiba nchini ili kuboresha huduma za afya na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika pato la Taifa?
Supplementary Question 3
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwa kuwa Hospitali ya Kanda ya Kusini - Mitengo iliyopo Mtwara tayari imeshajengwa. Je, ni lini ujenzi wa awamu ya tatu utaanza ili kukamilisha mzunguko wa hospitali ya kitalii?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Agnes Hokororo kwa kazi kubwa anayowapigania wananchi wa Mtwara hususani wanawake wa Mtwara ambao wameendelea kumuamini na kwa kumchagua kwa kura nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge tunazo Hospitali za Kanda ya Kusini ambazo tunazifanyia kazi kimkakati, Lindi pamoja na Hospitali ya Mtwara na ujenzi wa awamu ya pili tunakwenda kuutenga na kwenye bajeti hii tumewatengea shilingi bilioni tatu ili tuendeleze ujenzi wa awamu ya pili ili nao waweze kupata huduma zote kwa sababu ni Hospitali ya Kanda, lakini inatakiwa iwe na huduma bobezi zaidi ya nane, hawajaweza kufikia pale kwa sababu hawajapata majengo yanayotosha hivyo tumetenga shilingi bilioni tatu ili tuweze kupeleka huduma zote waweze kupata huduma bobezi ili waweze kukidhi vigezo vya kuwa Hospitali ya Kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumepeleka fedha na ujenzi utaendelea awamu ya pili. (Makofi)