Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ester Edwin Malleko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa hoteli katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kutokana na umuhimu wa mradi huu, nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha wanapata mwekezaji haraka iwezekanavyo na huu mradi uweze kutekelezwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sekta ya uchukuzi ndio inachochea kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii. Ni namna gani sasa sekta hii inaweza kufanya kazi kwa haraka na kuhakikisha kwamba inapata wawekezaji wa ndani ili mradi huu uweze kutekelezwa kwa haraka? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Esther Malleko, kwa uzalendo wake na jinsi anavyofuatilia kwa ukaribu miradi ya uchukuzi lakini hasa pia uwanja wa ndege kule Kilimanjaro na Kaskazini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishamjibu kwamba usanifu unaendelea. Nimhakikishie mara tutakapokamilisha, tumeshamaliza usanifu sasa tupo kwenye hatua ya kupata mkandarasi. Atupe muda, ninajua anatamani kuona kazi hiyo inaanza hata kesho. Tukishapata mwekezaji ambaye yuko tayari, tukishaelewana naye tutakuwa tayari kwa ajili ya kuanza kazi hii. Na nitoe rai, kwamba wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie fursa hizi za kujenga hoteli kwenye viwanja vya ndege ili kuhakikisha sekta yetu inaboreka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu jinsi ambavyo tumejipanga kama sekta katika kuhakikisha kwamba tunashirikisha wawekezaji wa ndani katika uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi kwenye Taifa letu. Sote tunakumbuka mwaka jana tarehe 17 Julai, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Dira ya 2050. Katika dira hiyo ambayo kimsingi itaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2026 inasema tunataka tujenge Taifa kubwa la Tanzania ambalo litakuwa mfano katika ukanda wa Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujenge Taifa kubwa ambalo uchumi wake kama ambavyo mnakumbuka Mheshimiwa Profesa Kitila mara kwa mara amekuwa akirudia ambayo itakuwa na uchumi wa dola trilioni moja, sasa hivi tunazungumzia uchumi wa karibu dola bilioni kama 87. Anasema tunataka tujenge Taifa ambalo wananchi kipato chao kitakuwa ni dola 7,000 sasa hivi unazungumzia kipato cha kama dola 1,200 au 1,300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ili tufikie azma hiyo, lazima sekta binafsi ipewe fursa ya kushika uchumi kwa sekta 70% kwa sababu hiyo, kama mnataka mjenge Taifa kubwa la namna hiyo ambalo 70% mmetoa kwenye sekta binafsi haukwepi kushirikisha wawekezaji binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama mnakumbuka wakati Mheshimiwa Rais anazindua dira yetu, alisema anataka mapitio ya sheria zetu za uwekezaji ambazo zinakwenda kulinda na kuhamasisha wawekezaji mbalimbali duniani, lakini mkazo ikiwa ni wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Esther Malleko kwamba Serikali inajipanga na nitumie nafasi hii kuwasihi wawekezaji wote wa ndani wachangamkie fursa katika miradi ya uwekezaji kwenye reli, kwenye viwanja vya ndege, kwenye SGR kuweka treni, kwenye bandari ili uchumi wa Taifa letu ushikwe na wazawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe rai kwa wawekezaji wa nje kwamba yapo manufaa makubwa wanayoyapata endapo wakija wakashirikiana na wawekezaji wa ndani ya nchi yetu. Kuna baadhi ya vitu ambavyo kimsingi wanapewa kupitia wenzetu wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved