Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sigrada Wilhem Mligo
Sex
Female
Party
CHAUMMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SIGRADA W. MLIGO K.n.y. MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Je, lini ujenzi wa bandari ndogo ya Kagunga na Soko la Kagunga utakamilika ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Burundi?
Supplementary Question 1
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nina maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa SGR mpaka Kigoma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege Mkoa wa Njombe ambapo ni Serikali hii tangu mwaka 2005 imeweka mkakati wa kuijenga lakini mpaka leo haijaanza? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Sigrada Mligo, kwa maswali yake ya nyongeza ambayo ameuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Kiza Mayeye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti na imekwishaanza ujenzi wa miradi ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ambapo takribani kilometa 722 zimekamilika kwa zaidi ya 99% na sisi sote ni wanufaika tumeshanza kuona matunda yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutoka pale Makutopora mpaka Tabora kwenye kilometa 368 mkandarasi yuko site na yuko 14.5% na kutoka Tabora mpaka Isaka kilometa 165 mkandarasi yuko anafanya kazi yake vizuri na tunakabiria asilimia tisa. Vilevile, Isaka mpaka Mwanza karibu kilometa 341 napo mkandarasi anafanya kazi kwa zaidi ya 68%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pia kutoka Tabora mpaka Kigoma ambapo ni kilometa 506 mkandarasi ameshaanza kazi tayari yuko site na ukipita utamuona na tuko 10.3%. Kama haitoshi kutoka pale Uvinza kwenda mpaka Malagarasi na kutoka Malagarasi mpaka Msongati kwenda nchi ya pili tayari mkandarasi ameshapatikana, ameshasaini mkataba na kazi inaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Kiza Mayeye, kupitia Mheshimiwa Sigrada Mligo ambaye ameuliza swali hili, Serikali hii imedhamiria kukamilisha miradi hiyo haraka iwezekanavyo ili wananchi siyo tu wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla wanufaike na uwepo wa kimkakati wa nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ambalo ameuliza kuhusiana na uwanja wa ndege wa Njombe, ninafahamu kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe na mikoa ya jirani ya Mbeya, Iringa, Songea kwa maana ya Ruvuma na Kusini kwa ujumla wamepaza sauti kwa muda mrefu ili kuhakikisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Njombe unakamilika. Kwa nini?
(i) Kwa sababu ya kusafirisha mazao ya mboga mboga kama horticulture na kadhalika;
(ii) Tunao mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma katika Mkoa wa Njombe; na
(iii) Tunayo madini na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba aondoe mashaka. Serikali tumeshakubaliana, tumeshamkabidhi site mkandarasi ili akamilishe usanifu wa kina na pengine kabla ya mwezi wa sita mwaka huu atakuwa ameshakamilisha. Baada ya kukamilisha usanifu wa kina, taratibu za ujenzi zitaanza.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved