Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Edibily Kinyoma Kazala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Primary Question
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza: - Je, ni kwa kiasi gani wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini wananufaika na uwepo wa mwekezaji wa Kitalu cha Makere Forest Reserve?
Supplementary Question 1
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuna baadhi ya majibu hapo naona kama si sahihi ikiwemo shilingi milioni 166 ambazo ziligaiwa kwenye halmashauri kwenye huduma ya macho, DMO amekataa kwamba hizo fedha hazijawahi kufika. Pia hivyo visima sita vinavyotajwa hapo, kati ya hivyo visima sita vipo viwili tu na kimoja ndicho kinachofanya kazi vizuri, lakini pia baadhi ya hizo shilingi milioni nne zinazotajwa hapo nazo zinaonekana baadhi ya vijiji bado wanakiri kutokupokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu…
MWENYEKITI: Maswali Mheshimiwa.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niulize; mwekezaji huyu amekuwa akiwa na changamoto nyingi kwa jimbo langu la Kasulu Vijijini ikiwemo kufyeka zaidi ya hekari 200, kuzuia wananchi kuvua kwenye Mto Malagarasi na kuzuia wananchi kuweka mizinga kwenye miti.
Je, Serikali haioni haja ya kuleta mwekezaji mwingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa mwekezaji amekuwa akigombana sana na wananchi wa Jimbo langu la Kasulu Vijijini; je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kukikata kipande kile ambacho kipo mwekezaji anapopakana na wananchi kimilikiwe na halmashauri ili iongezee mapato na kuepusha migogoro ya Serikali na wananchi?
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge, ameomba kupelekewa mwekezaji mwingine kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la kitalu cha Makere Uvinza Open Area lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambako Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani. Sisi kama Wizara tulipokea ombi kutoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhusu kutenga eneo hili kwa ajili ya eneo la uhifadhi na utalii. Hivyo, mamlaka haya yapo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Kama watakaa chini na wakaamua tena kama Baraza la Madiwani sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii hatuna kipingamizi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la kumega eneo na kuwa sehemu ya halmashauri, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya swali lake la nyongeza la kwanza, eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na wao ndio waliotuomba sisi kama Wizara tuweze kutoa miongozo ya jinsi ya kuendesha eneo hili kwa ajili ya uhifadhi na utalii. Hivyo kwa kuwa eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ninaomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge arejee kwenye Baraza la Madiwani na waweze kuketi kuona jambo gani wanaweza kufanya kwa maslahi mapana ya halmashauri yake ya Kasulu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved