Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Alan Thomas Mvano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kakonko
Primary Question
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: - Je, lini Barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama kilometa 41.43 itajengwa kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninaipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali yetu hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara hii ya Ujenzi inafanya kazi kubwa sana katika nchi yetu. Pongezi kubwa sana na ushirikiano tunauona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa barabara hii ya kutokea Kakonko kwenda kwenye mpaka wa Burundi eneo la Muhange ni potential sana kwenye Wilaya yetu. Kwa sababu ya umuhimu wake jambo la kwanza ninamuomba Waziri utayari wake, twende Kakonko aone barabara hii, kwanza aone umuhimu wake vilevile aone hali ya barabara kwa sasa. Jambo la muhimu sana hilo ninaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba, barabara hii inategemewa na wananchi wa Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Muhange, Kasuga, na Kakonko; wananchi zaidi ya 60,000 wanaitegemea barabara hii. Sasa kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha barabara hii imekwishapandishwa hadhi, sasa hivi ipo TANROADS.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika vizuri kwa sababu siku chache zilizopita lori limeanguka, limepata ajali katika barabara hii kwa sababu ya ubovu wa barabara kwa ajili ya mvua …
MWENYEKITI: Swali, Mheshimiwa tunakushukuru.
MHE. ALAN T. MVANO: … sasa nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika kwa viwango vya TANROADS wakati tukisubiria upembuzi yakinifu ufanyike? Nashukuru.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mvano, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, tupokee pongezi zake kwa kazi kubwa ambazo zinafanyika katika shughuli ya miundombinu na hasa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara kwanza ilikuwa ipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini; na kwa sababu ya umuhimu wake, tunajua ni barabara ya mpakani, ndiyo maana imepandishwa hadhi. Si hadhi tu, kwa sababu inaunganisha nchi na nchi, tunajua wenzetu wa Burundi wamesogeza makao yao makuu ndiyo maana hata imepandishwa kutoka hadhi ya barabara ya mkoa kuwa trunk road. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba umuhimu huo tunautambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuhakikishie nipo tayari, tutakapopata muda wakati wowote tunaweza kwenda tukaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupitika ni suala la kiutendaji. Ninaomba nimuagize Meneja wa Mkoa wa Kigoma ahakikishe kuwa tutakapomaliza Bunge hili apate muda wiki hii akaione na ahakikishe kwamba anafanyia ukarabati ili iweze kupitika na wananchi waweze kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji katika barabara hiyo. (Makofi)
Name
Kijakazi Mohamed Yunus
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: - Je, lini Barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama kilometa 41.43 itajengwa kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa barabara iliyoelezwa hapa, Barabara ya Ngongo – Milola – Michiga kwa muda mrefu sana imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Pamoja na jitihada za Serikali za kufanya marekebisho mara kwa mara, ningependa kufahamu, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ukizingatia kwamba barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Jimbo la Lindi Mjini, Mchinga na Jimbo la Ruangwa?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi kuwa kama alivyosema, barabara hii inaunganisha majimbo mawili; Jimbo la Mheshimiwa Salma na Mheshimiwa Mmuya. Wamekuwa pia wakifuatilia sana kuhusu ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Tumekwishafanyia usanifu na sasa tunatafuta fedha tuijenge kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kati ya barabara zetu ambazo sasa hivi tunatafuta teknolojia mpya ambayo ni rahisi kujenga barabara kwa kiwango cha lami. Hii ni moja ya barabara ambayo ipo kwenye mpango wa kuifanyia pia majaribio katika hiyo teknolojia mpya. Kwa hiyo, tuna uhakika wakati tunatafuta fedha, lakini pia imeingia kwenye mpango wa kufanyia majaribio, hii tunayosema teknolojia mpya ya barabara.
Name
Joseph Kasheku Musukuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Primary Question
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: - Je, lini Barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama kilometa 41.43 itajengwa kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Mavitu ya kizungu haya! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kazi nzuri inayoendelea kwenye jimbo langu ya utengenezaji wa barabara kilometa 20 za lami kuanzia Nkome mpaka Sungusila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, pamoja na kwamba yupo kwenye maandalizi ya ujenzi, lakini kile kipande sasa ni awamu ya pili hakina mkandarasi wa kukikarabati, ukitokea Geita kilometa 37 mpaka anapoanzia kinapewa bajeti ya kukarabatiwa, lakini kutokea pale Sungusila kwenda Nkome haijawahi kukarabatiwa, imekuwa kama adhabu.
Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kumsisitiza ile barabara awe anaifanyia ukarabati?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli kwamba hii barabara ipo kwenye mpango, ina mkandarasi. Mkandarasi akishapatikana mara nyingi ndiye anakuwa na wajibu wa kufanya ukarabati wa barabara hiyo. Kwa hiyo, kwa kuwa mkandarasi yupo, nimwelekeze Meneja wa Mkoa wa Geita, kwanza ahakikishe kwamba anafanya ukarabati wa hii barabara ili iweze kupitika muda wote na hasa katika kipindi hiki cha mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nimuhakikishie Mheshimiwa Musukuma, moja; hiyo barabara nimeshaitembelea lakini pia nipo tayari kwenda tena kuitembelea barabara hiyo ili kuhakikisha tu kwamba tunahakikisha kwamba hiyo barabara inaanza haraka kujengwa, ahsante.
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: - Je, lini Barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama kilometa 41.43 itajengwa kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 4
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mbinga – Muyangayanga – Litembwa – Nkili iliahidiwa muda mrefu na Mheshimiwa Rais wakati akiwa Makamu wa Rais; je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo?
MWENYEKITI: Majibu, Mheshimiwa Naibu Waziri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani ningemwomba aweze kurudia swali Mheshimiwa Mbunge.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jonas Mbunda, tafadhali rudia swali lako kwa kifupi.
Mheshimiwa Jonas Mbunda.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba Barabara ya kutoka Mbinga – Muyangayanga – Litembwa – Nkili ni barabara ambayo tumeiombea kwa muda mrefu sana na ilitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiwa Makamu wa Rais. Swali langu ni kwamba, je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli na nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wa kitaifa na hasa Mheshimiwa Rais huwa ni suala la kipaumbele katika kutekeleza zile ahadi za viongozi wa kitaifa na hasa Mheshimiwa Rais. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo barabara kwanza tutaipitia upya kwa maana ya ku-review ile design tukiwa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami kama alivyokuwa ameahidi Mheshimiwa Rais.