Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Devotha Daniel Mburarugaba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:- Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
Supplementary Question 1
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa katika urejeshaji wa mikopo na tunafahamu Serikali yetu imekuwa ikitenga fedha kwa kila halmashauri kila mwaka, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri, changamoto za urejeshaji zimekua ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itaamua kuweka elimu ya fedha kwa wanufaika hawa ili waweze kuelewa biashara wanazoenda kuzifanya, ili tuweze kukusanya mapato yetu kwa ukamilifu? (Makofi)
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Daniel kwa kuuliza swali la nyongeza ambalo anawapambania wananchi, hasa wa Mkoa wa Kagera, lakini ni kwa nchi nzima ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tumekwishaelekeza watalamu wetu, Maafisa Maendeleo waweze kutoa elimu ya mikopo. Sambamba na hilo Kamati ya TAMISEMI ilitoa maelekezo mahsusi na sisi kama Wizara tumeyachukua na tumewaelekeza wataalam wetu kule halmashauri waweze kutoa elimu ya mikopo hii na pia waweze kutoa elimu ya namna ya kusaidia vikundi hivi kuweza kufanya marejesho, lakini pia waweze kupata zile kazi za 30% za PPRA ili kuweza kusaidia vikundi hivi katika mikopo viweze ku-qualify na vile vingine ambavyo ni vipya vianze kukopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mikopo hii liko wazi katika miongozo kwa maana ya kwamba ni kuwasaidia mitaji. Kwa hiyo, tunawaomba sana Watanzania wanaopata mikopo hii ya vikundi waweze kufanya marejesho kwa wakati ili tuweze kuwakopesha na wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Faraji Buriani Nandala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:- Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
Supplementary Question 2
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Swali langu, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ndanda, nataka kufahamu ni lini Serikali itaona ipo haja ya kupunguza siku za maombi ya mikopo hii kutoka siku 90 zilizopo sasa hivi mpaka siku saba au 14, ili tuweze kuwafikia Watanzania wengi kwa muda mfupi? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyoliuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi siku 90 zipo kwa utaratibu, kwa maana ya kwamba wapewe elimu ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoka kuuliza ni kipindi cha kupewa elimu, lakini kufanya ufuatiliaji wa kuona kwamba vikundi ambavyo vimeomba ni kweli vina haki ya kupewa mikopo ile na vina uwezo wa kurejesha. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunauchukua ushauri wake na tutaufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Christina Solomon Mndeme
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:- Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
Supplementary Question 3
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya na hususan kuhakikisha kwamba suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linatekelezwa ipasavyo. Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa malengo haya ambayo yanakwenda kumuongezea kipato mwananchi kuanzia ngazi ya kaya mpaka Taifa na hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuiuliza Serikali swali hili, katika malengo haya mazuri ya Serikali ya kuwakopesha wajasiriamali hususan wanawake na hasa wanawake wa Mkoa wa Tabora.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mikopo hii wanayopewa wanawake wajasiriamali, wanazalisha bidhaa zenye kukidhi haja na soko lililopo sasa hivi nchini na nje ya nchi ili sasa bidhaa zao zile wanazozalisha ziweze kuwa na tija na kukidhi soko la ndani na soko la nje ili waweze kuinua kipato chao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ufuatiliaji wa mikopo hii, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inafuatiliwa na kweli inakwenda kuzalisha kwa tija?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji majibu ili sasa wanawake hawa waweze kuzalisha kwa tija na hususan wanawake wa Mkoa wa Tabora ili kipato chao kiweze kukua kuanzia ngazi ya familia na Taifa. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania wananchi hasa akinamama wa Mkoa wa Tabora, anataka tuhakikishe tunapeleka tabasamu. Ninapokea pongezi ambazo amezitoa na hiyo ndiyo nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha anatukomboa kiuchumi wapambanaji wetu akinamama wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishatoa maelekezo kwamba maafisa maendeleo wetu hawana kazi tu ya kukusanya fedha na kuzipeleka kwenda kwenye mikopo, wanayo kazi ya kutoa elimu ya tija ya kutosha na kufuatilia marejesho ili tuweze kuwakopesha na wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Name
Dr. Christina Christopher Mnzava
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:- Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa Serikali imeshatoa kanuni, imetoa maelekezo, lakini bado kuna wananchi ambao wako vijijini hawajapata elimu ya mikopo, nini mkakati wa Serikali? (Makofi)
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mnzava kama ambavyo ameliuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuendelea kutoa elimu na kufanyia marekebisho mapungufu ambayo yanaendelea kujitokeza. Nimesema awali ya kwamba, Kamati ilitoa ushauri wa kutosha kabisa, Kamati ya TAMISEMI nasi kama Wizara tunakwenda kufanyia kazi ili kuendelea kurekebisha yale maeneo yenye upungufu ili elimu iwafikie wakopaji na waweze kukopesheka, waweze kujiinua kiuchumi na waweze kufanya marejesho kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.