Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: - Je, lini Kiwanda cha Chai cha WATCO kilichopo Katumba – Tukuyu Wilaya ya Rungwe, kitafunguliwa?

Supplementary Question 1

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niipongeze sana Serikali kwa hatua iliyochukua, kwamba tarehe 2/2/2026 Kiwanda cha WATCO kinakwenda kufunguliwa. Ninashukuru sana kwa kuwa mmeelewa vizuri shida ya wananchi wa Wilaya ya Rungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Wanawake wa Wilaya ya Rungwe pamoja na wananchi kwa ujumla wamezoea sana kuamka saa 11.00 alfajiri kwa ajili ya kwenda kuchuma chai, maana hiyo ni sehemu ya ajira yao. Ajira hiyo sasa hivi imekuwa kama ni ndoto kwao kwa sababu Kiwanda cha Chivanje kimefungwa, sasa hii ni miaka miwili imepita. Je, ni lini Serikali itakwenda kufungua Kiwanda hicho cha Chivanje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwenye hicho hicho Kiwanda cha Chivanje, kwa sababu kipo kwenye Tarafa ya Pakati na WATCO iko kwenye Tarafa za huku Ukukwe na Tukuyu Mjini. Wakulima wa Wilaya ya Rungwe wanalima mazao mengi, ikiwemo pamoja na zao la parachichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bei elekezi ya Serikali kilo ya parachichi ni shilingi 2,500, lakini sasa hapo katikati wameingia watu ambao wanaitwa madalali ambao wanawaumiza sana wakulima wa Wilaya ya Rungwe ambapo wamepelekea bei ya kilo ya parachichi kuwa shilingi 1,200 mpaka 1,500. Inaleta hasara kubwa sana kwa wakulima. Je, Serikali ina mkakati gani wa kwenda kusimamia bei hizo ili wananchi wa Wilaya ya Rungwe waweze kupona?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Suma Fyandomo kwa maswali mazuri, lakini pia kwa ushirikiano ambao amekuwa akiufanya na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo husika, ni jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ninamhakikishia ni kwamba, kila hatua tunayoifanya sisi Serikali ni hatua. Hatua ya kwanza ni kufungua Kiwanda cha WATCO ambacho kilikuwa na changamoto ya muda mrefu. Baada ya hapo, maana yake tutahamia katika hatua inayofuata kwenda katika eneo la Kiwanda cha Chivanje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wanauza chai yao, na pia kwa akina mama ile ajira ambayo wamekuwa wakiipata ya kuchuma chai inaendelea. Kwa hiyo, hilo lipo katika mipango ya Serikali na tutalitekeleza kwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu parachichi na hao madalali ambao wamekuwa wakifanya hiyo kazi, maelekezo ya Serikali yako pale pale, kwamba bei elekezi ndiyo ambayo inatakiwa ifuatwe kwa wanunuzi wote wa parachichi. Ndiyo maana sisi Serikali tumekuwa tukisisitiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili wawe na nguvu ya pamoja katika kupigania bei ambayo sisi tumeiainisha. Kwa hiyo, kwa sababu ameitoa hapa kama taarifa nasi tutaendelea kufuatilia ili tuhakikishe ile bei ambayo imetolewa inafuatwa na wanunuzi wote. Ahsante.

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: - Je, lini Kiwanda cha Chai cha WATCO kilichopo Katumba – Tukuyu Wilaya ya Rungwe, kitafunguliwa?

Supplementary Question 2

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wakulima wa chai wa Tarafa ya Bungu wameteseka kwa muda mrefu baada ya mwekezaji kufunga viwanda; na pamoja na ahadi nyingi, lakini hawaoni mwelekeo mpaka sasa. Je, Serikali ina mpango upi wa kuwaondolea adha wakulima wa chai wa Tarafa ya Bungu kule Korogwe?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze vilevile Mheshimiwa Mnzava, ninafahamu kwamba amekuwa akilifuatilia jambo hili kwa muda mrefu. Nimwambie tu jambo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tuna uhakika na hiki ninachokisema. Ni kwamba Serikali tayari tumeshanunua kiwanda kwa ajili ya kupeleka katika eneo la Jimbo lako katika AMCOS ya Sakare pale, kiwanda kwa ajili ya kuchakata chai. Kimekamilika pale nchini China, sasa hivi tuko katika harakati za kusafirisha na kuleta hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, awahakikishie wananchi wake kuwa, pamoja na kwamba mazungumzo mengine yanaendelea, lakini sisi kama Serikali tumeshanunua kiwanda hicho na tutakuja kukifunga ndani ya muda mfupi ambao naamini itakuwa ni suluhisho la kudumu kwa wakulima wa chai katika eneo lake, ahsante sana.