Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mgore Miraji Kigera

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza: - Je, Serikali ipo tayari kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki wa vizimba Musoma ili kutoa ajira kwa vijana?

Supplementary Question 1

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninapenda kutoa pongezi nyingi sana na shukrani kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwathamini wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini, kwani tunategemea sana Ziwa kuliko kitu chochote. Hivyo, kwa kuwezesha vijana wetu kupata mikopo ili waweze kufanya ufugaji kwa weledi mzuri, wataenda kufungua fursa ya ajira na mzunguko wa fedha na uchumi utakuwa Musoma Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: Je, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha inawathamini wafugaji wa samaki kwa kupitia vizimba? Kwani wamekuwa na changamoto kubwa sana kwenye suala zima la upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora pamoja na chakula. Kwa kuwa changamoto ya chakula huwa ni shida, inapelekea samaki wengi waweze kudumaa na wafugaji hawa kupata hasara kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki anafugwa kwa miezi nane, wanatarajia apate kilo moja and above, lakini kwa sasa hivi samaki wanafubaa na kupata 0.6 kg mpaka 0.8 kg. Kwa hiyo, ni nini mpango wa Serikali kuwawezesha wafugaji hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, kauli ya Serikali ni ipi kuhakikisha inawasaidia vijana kupata ujuzi pamoja na mikopo ili waweze kuanzisha upatikanaji wa chakula wenyewe katika Manispaa ya Musoma na waache kutoa chakula Kenya pamoja na Kibaha? Kwani ni mwendo mrefu na gharama ya chakula inakuwa ni kubwa sana. (Makofi)

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninarudia tena kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa bidii yake kubwa ambayo anaendelea nayo kufuatilia miradi hii ya vizimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vifaranga na chakula, kama nilivyozungumza hapo awali, tunaendelea na harakati za utatuzi wa changamoto hizi tulizokuwanazo mwanzo. Moja, tumeendelea kuhamasisha sekta binafsi katika kuwekeza, kuzalisha vifaranga na kutengeneza viwanda vya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba tumekuwa na ongezeko kubwa sana la vifaranga pamoja na chakula ambacho kimesaidia wafugaji wetu kwa njia ya vizimba kuweza kupata kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunaendelea kuwapa vijana wetu elimu ya utambuzi ili pale wanapoona vifaranga na chakula sokoni waweze kutambua kile kilicho bora against kile ambacho hakipo bora. Pia, tumeendelea kurekebisha mifumo yetu ya utoaji wa mikopo ambapo hapo awali tulikuwa na wazabuni wa moja kwa moja ambao tulikuwa tunaelekeza vijana wetu kwenda kwao kwa ajili ya kujipatia vifaranga na chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa vile tumeongeza upatikanaji wa vifaranga na chakula, tumeongeza uwazi ili kijana aweze kuingia sokoni na kuchagua kifaranga na chakula kilicho bora kwa ajili ya samaki wake aweze kupata samaki walio bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kuhusu uwezeshaji wa vijana kujipatia ujuzi na mitaji ya kuwekeza katika uzalishaji wa chakula, hiki ndicho ambacho tunafanya mpaka sasa. Tunaendelea kuhamasisha vijana wetu kuandaa maandiko ili ile elimu tunayowapatia tunapokuwa tunawaandaa kwa ajili ya kuingia kwenye ufugaji wa vizimba kupitia taasisi zetu za FETA na programu zetu za BBT-Uvuvi, waweze kuitumia kwa ajili ya kuzalisha chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, waandae maandiko wapeleke katika Halmashauri zetu waweze kunufaika na fedha za 10% na pia waandae maandiko wapeleke katika taasisi zetu za fedha ili waweze kupata mikopo ya kuwekeza katika uzalishaji wa chakula kwa sababu ni fursa kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Wizara tumeandaa mwongozo wa utengenezaji wa chakula cha samaki ili kila anayetaka kuwekeza katika sekta hii ya uzalishaji wa chakula cha samaki aweze kupata wepesi wa uwekezaji huo, na sisi kama Wizara tunaendelea kutoa msaada wa utaalam na maelekezo kwa yeyote ambaye anahitaji kufanya uwekezaji katika uzalishaji wa chakula cha samaki ili tuongeze upatikanaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)