Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: - Je, lini wananchi wa Bukoba watawezeshwa kwa kupewa vizimba vingi zaidi vya samaki ili kushiriki katika kukuza uchumi?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu ya Serikali kuhusu jambo hili la vizimba Bukoba. Hata hivyo, vizimba 44 vilivyopo Bukoba nii vichache sana, tuna ukanda wa ziwa kilometa 59. Kwa hiyo, tunahitaji vizimba vingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali haioni kwamba vizimba vikiongezeka kwa wananchi wa Bukona ni ajira tosha kwa wananchi wale kuwaongezea uchumi na Taifa zima kwa ujumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hata hivyo vizimba vichache vilivyopo 44 hatuna vifaranga hadi twende Mwanza, umbali mrefu sana, vifaranga vinakufa, vinakosa oxygen. Je, Serikali haioni haja ya kujenga miundombinu ya vifaranga pale Bukoba kusudi wananchi wapate vifaranga pale pale kwao?

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kwanza ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Jasson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kwa bidii yake kubwa ya kuendelea kufuatilia mustakabali wa vijana wake, hasa wanaojihusisha na ufugaji wa vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, ni kweli vizimba 44 kwa eneo la ukubwa wa Ziwa lililoko katika Jimbo la Bukoba Vijijini ni vichache, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la awali, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vizimba hivi kwa vijana, wanawake na vikundi maalum vikiwemo vya wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaendelea kuhamasisha taasisi za fedha zikiwemo benki na taasisi nyingine za uwezeshaji kuendelea kuwanufaisha au kuwapa mikopo vijana ili tuweze kuongeza kasi ya vijana hawa wanaonufaika na miradi hii ya vizimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuhusu suala la vifaranga, ni kweli, wakati tunaanza miradi hii, tulikuwa na changamoto kubwa sana kwanza ya upatikanai wa vifaranga, na pili upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishapiga hatua, tangu mwaka 2021 tulikuwa na uzalishaji wa vifaranga takribani 24,024,000 kwa mwaka na sasa hivi tunazungumzia uzalishaji wa vifaranga zaidi ya 140,000,000 kwa mwaka. Maana yake ni kwamba tumeongeza uzalishaji, lakini tunaongeza uratibu wa karibu wa wazalishaji wote ndani ya sekta binafsi na katika taasisi zetu wenyewe ikiwemo TAFIRI kuhakikisha vifaranga hivi vinavyozalishwa vinakuwa na ubora unaofaa ili vinapofikishwa kwa vijana wetu, basi viweze kuwapa tija inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.