Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa utaanza kujengwa?

Supplementary Question 1

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Naishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kampeni yake aliwaahidi wananchi wa Misenyi na Mkoa wa Kagera kwamba ndani ya siku 100 ataanza utakelezaji wa mradi huo, na sasa ni ushuhuda, kutokana na majibu ya Serikali ndani ya siku 100 mtaalamu mwelekezi amefika site na kuanza upembuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hatua hiyo, chini ya Wizara ya Uchukuzi, chini ya Waziri, Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Naibu Waziri, Mheshimiwa David Kihenzile, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, uwanja huo ni wa Kimataifa, na utainua uchumi mkubwa Mkoa wa Kagera na Jimbo la Misenyi kwa ujumla, je, ni mkakati gani ambao Wizara ya Uchukuzi inaweza kuuratibu pamoja na halmashauri kupima na kupanga maeneo yote yanayozunguka eneo la uwanja huo, ili kuweza kuleta taswira nzuri na kuwainua wananchi hao kiuchumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa, uwanja huo utakuwa wa kimkakati ukihudumia nchi za Maziwa Makuu, ni mwongozo upi ambao Serikali inautoa ili tuweze kujiandaa kwa shughuli za kiuchumi, ili uwanja huo sasa ukianza uwe na tija kubwa kwa wananchi wa Misenyi, Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla? Ahsante sana. (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Kyombo kwa kutambua kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais Samia, ambaye ndani ya siku 100 aliahidi na ameanza kutekeleza kwa ajili ya kujenga uwanja mkubwa wa Kyabajwa. Ninakubaliana naye, Serikali iko tayari kushirikiana na halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba halmashauri waweke mkakati huo na yeye mwenyewe Mbunge akiwa ni sehemu ya halmashauri, ili tupime maeneo yale yawe vizuri, wananchi wasivamie kwa sababu, uvamizi unatokea pale ambapo halmashauri ilikuwa inajua kwamba kuna jambo zuri linakuja, lakini haikuweka mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba waanze kuweka mpango huo mzuri. Sisi kama sekta, kwa maana ya Wizara ya Uchukuzi, chini ya Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, pamoja na TAA, tuko tayari kushirikiana na nyie kuhakikisha kwamba, tunaweka jambo hili vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumza kuhusiana na tija ya uwanja huo. Natoa wito na rai kwa wananchi pamoja na viongozi Mkoa wa Kagera kwamba, mradi huu ni mkubwa sana, utakwenda kuunganisha nchi yetu na mikoa ya jirani, utakwenda kuunganisha nchi yetu na mikoa ya jirani, utakwenda kuunganisha nchi yetu na nchi jirani. Ni vyema wakaanza kuchangamkia fursa za kiuwekezaji na tuwaombe wananchi wetu walinde ardhi yao, wasiuzeuze tu, maana hii inayokuja sasa ni neema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia anawaletea neema. Itakuwa ni jambo la kusikitisha baadaye ardhi yote imechukuliwa na watu wa nje, wao hawana ardhi. Hivyo basi, tuchangamkie fursa, tutazame cha kufanya kuhakikisha kwamba, uwanja huu unakwenda kuwa na tija kubwa kwa wananchi na Taifa letu.

Name

Yagi Maulid Kiaratu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa utaanza kujengwa?

Supplementary Question 2

MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Singida wana hamu sana ya kupata usafiri wa anga. Pamoja na kuchagiza shughuli za kiuchumi, usafiri na usafirishaji Singida ni katikati ya nchi. Singida ni jirani na Dodoma, ikitokea rubani akashindwa kutua Dodoma, mji wa karibu kutua ni Singida; lakini kwa sababu, Singida ni Katikati, itakuwa kiungo kizuri cha usafirishaji ndani ya nchi. Ninaomba kauli ya Serikali, ni lini sasa Singida watajengewa uwanja wa ndege? (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Singida Mjini na Mheshimiwa Mstahiki Meya Mstaafu kwa ufuatiliaji wake wa uwanja huu mzuri na muhimu kwa Taifa letu. Kama alivyoeleza yeye mwenyewe, uwanja huu ulijengwa miaka ya 1950 na Serikali imekuwa ikiutumia, lakini kwa kweli, kiwango chake kiko chini ni wa changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maombi ya Waheshimiwa Wabunge na wakati mwingine viongozi, Serikali imepokea kilio hicho na imeanza kufanya usanifu. Ninamhakikishia, tunakwenda kujenga Uwanja wa Singida na mwaka wa fedha 2026/2027 tunaingiza kwenye bajeti. Tunaenda kuongeza runway kutoka 1,000 mpaka 2,000, tunaweka lami pamoja na kuhakikisha kwamba, tunaweka taa, ili uwanja utumike mchana na usiku.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa utaanza kujengwa?

Supplementary Question 3

MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, hususan Mkoa wa Mwanza. Uwanja huu mpaka sasa haujakamilika na ukizingatia ni wa muhimu kwa kuwa, tuko karibu sana na hifadhi ya Serengeti, ni kilomita 130 tu. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha uwanja huu, ili angalau wananchi wa Mkoa wa Mwanza waanze kufaidika na uchumi unaotokana na masuala ya utalii?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nitakwenda kujibu kwa kifupi kama ulivyonielekeza. Ninampongeza Mheshimiwa Mary Masanja kwa kutambua umuhimu wa uwanja huu ambao kimsingi ndiyo kitovu cha Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kulitambua hilo, moja, imeanza mchakato, kwa ajili ya kuboresha jengo la abiria; na pili, imeanza na documentation ili kuufanya kuwa wa Kimataifa pamoja na mambo mengine, kama vile kumaliza mgogoro wa wananchi ambao walivamia eneo la pembeni ili uweze kuwa na ulinzi. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inalitambua hilo na itaongeza kasi kuhakikisha kwamba, inauboresha na kuufanya uwanja huu kitovu ndani na nje ya nchi yetu.

Name

Jafari Wambura Chege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa utaanza kujengwa?

Supplementary Question 4

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nijue ni lini Uwanja wa Ndege wa Musoma, kama kielelezo cha Mkoa wa Mara, utakamilika?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mkoa wa Mara, ilianza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mara. Pale Serikali inajenga runway, kwa maana ya njia ya kuruka na kutua ndege, pia inajenga na majengo mbalimbali. Tayari runway imekamilika, tunakwenda kumalizia majengo yaliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema ninaomba kurejea kauli yangu niliyoitoa siku tano au sita kwamba, kuanzia mwezi ujao au unaofuatia, Serikali ina mpango wa kuanza kufanya testing ya ndege za Shirika letu la Ndege ATCL kwenye viwanja vitatu; Uwanja wa Musoma, Shinyanga na Sumbawanga. Hii ni kuthibitisha dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, ameamua kuitendea haki nchi hii kwenye sekta ya anga.