Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kiza Hussein Mayeye
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza: - Je, Serikali imechukua hatua gani za kurejesha Bandari za Kibirizi na Ujiji zilizokumbwa na madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi na kujaa maji?
Supplementary Question 1
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Ujiji na Kibirizi zina mahusiano ya moja kwa moja na Bandari Ndogo ya Kagunga, ambayo iko mpakani mwa Burundi na Tanzania. Sasa nataka kupata majibu ya Serikali, ni lini mtakamilisha miradi fungamanishi, kama Barabara ya Mwandiga - Bubango - Chankere mpaka Kagunga, ambayo itakuwa kitovu cha kuweza kuunganisha nchi ya Burundi na Kongo na kuweza kuongeza uchumi katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Kigoma na Tanzania kwa ujumla?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Serikali imekuwa ikihusisha sekta binafsi katika uwekezaji wa bandari, kwa mfano Kigoma, Dar es Salaam na maeneo mengine. Taifa limenufaika na nini katika kushirikisha sekta binafsi? Ninataka majibu ya Waziri, ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mayeye kwa maswali yake na uzalendo kwa Taifa lake, jinsi anavyosimamia miundombinu na kuunga mkono kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni Wabunge wachache wanaweza kuelewa mchango ambao Mheshimiwa Rais anautoa katika Taifa letu. Kwa muda mrefu Wabunge kutoka Mkoa wa Katavi, Rukwa na Kigoma wamepiga kelele kutaka Serikali zote kuanzia ya kwanza mpaka sasa ziboreshe Ziwa Tanganyika kwa sababu ni uchumi, ni maisha, ni ulinzi na ni ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumtaarifu Mheshimiwa Mayeye, na yeye ni shahidi kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana miaka minne tu, lakini mambo aliyoyafanya kwenye eneo hilo ni ya kipekee. Ukiacha SGR anayojenga kuipeleka mpaka Kigoma ili kuhakikisha kwamba Kigoma inafunguka; ukiacha meli anazokarabati ikiwemo MV Liemba ambayo inakaribia 40%, MV Mwongozo ambayo ipo kwenye mpango wa Manunuzi, MT Sangara na meli ya mafuta inayofanya kazi; ukiacha kiwanda cha meli kinachojengwa pale Katabe, Kigoma, bado Mheshimiwa Dkt. Samia hajawaacha Wanakigoma pamoja na Ziwa Tanganyika kwa ujumla kwa sababu, ni yeye ameidhinisha mradi mkubwa wa maboresho wa Bandari tatu za Kibirizi, Kigoma na Ujiji na akapeleka fedha, shilingi bilioni 32.5 ambazo zimeboresha maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Serikali hii kwa kutambua umuhimu wa Bandari hiyo ya Kagunga ilipeleka fedha shilingi bilioni tatu na kidogo, na tayari tumekamilisha pale gati ya mita 50. Kama nakubaliana naye, ni kweli kabisa, ili Mradi wa Bandari ya Kagunga uweze kuwa na tija kwa Taifa letu, na wananchi wa Kigoma ambao ninaamini wanafuatilia, ni lazima ufungamanishwe na miradi ya soko pamoja na barabara aliyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kulitambua hilo, tayari imeanza kwa upande wa soko. Wenzetu wa TAMISEMI wametenga shilingi bilioni 2.3 na wamemlipa mkandarasi shilingi milioni 222 kuhakikisha kwamba, soko linajengwa na faida ya soko lile inakwenda kufungua bandari. Watakuja wenzetu wa Congo, watakuja watu wa Burundi, watakuja eneo lile kwenye bandari na baadaye tutafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, barabara hii aliyoitaja ya Mwandiga Chankere, Mwamgongo pamoja na Kagunga yenye urefu wa kilomita takribani 65, Serikali imeanza kufanya kazi, imejenga kilomita 18, ili bandari ile iweze kufunguka. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge awe na subira na Wabunge wote wa Kigoma. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kuimarisha na kuendelea kuleta mapinduzi makubwa kwenye Mkoa wa Kigoma.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved