Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Wilson Charles Mahera

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Primary Question

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza maji Kata za Bisumwa, Bukabwa, Nyankanga, Butuguri, Bwiregi, Buruma, Kyanyari, Buhemba, Mirwa na Kikirango?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuletea mradi mkubwa wa maji wenye uwezo mkubwa sana wa kuweza kuzalisha lita milioni 35 kwa siku, lakini kwa sasa ni lita milioni 17. 5 kwa siku, ila mradi huo kwa sasa unatoa lita milioni tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuweza kusambaza maji katika vijiji ambavyo vinausubiri kwa hamu kubwa, kuna miradi miwili ambayo iko Wizarani ya 4.8 billion na 3.5 billion. Je, ni lini Wizara itatoa kibali ili miradi hiyo iweze kutangazwa wakandarasi wapatikane? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa vile mradi huu ni mkubwa sana na utafika kwenye Kata ya Mirwa, tunayo Kata ya jirani ya Sirorisimba ambayo iko karibu na Wilaya ya Serengeti na Kijiji cha Baranga Kata ya Buswahili hawana mradi wa maji. Je, Wizara ina mkakati gani wa kuanza kuandaa mradi ili vijiji hivyo navyo vipate maji?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, nilipata ziara katika Jimbo lake na alikuwa kwenye safari zake, lakini aliamua kuahirisha na kurudi jimboni kwake ili tuweze kufanya ziara kwa pamoja. Ninampongeza sana kwa namna ambavyo anaendelea kuguswa na changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo lake ni 78%, lakini tunayo miradi miwili inayoendelea yenye gharama ya shilingi bilioni tano lakini vilevile, mradi huu ambao Mheshimiwa ameongelea, ni mradi ambao unatokana na ahadi za Viongozi wa Kitaifa. Ni mradi ambao sisi kama Serikali na sekta ya maji ni lazima mradi huu utekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mradi huu ninaufahamu vizuri kwa sababu nina picha nzima ya Butiama. Kikubwa tu ni kwamba ile taarifa ambayo amesema, ilishafika Wizarani, ninaomba nimhakikishie kwamba haijafika mpaka sasa, lakini tumeshawasiliana na watu wetu ili waweze kuileta kwa haraka ili tuhakikishe kwamba tunachukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu wa Buhemba utakapotangazwa, utafika mpaka katika eneo la Sirorisimba ambapo utaenda mpaka kwenye Kata ya Mirwa kule. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aondoe shaka, Serikali itakapotoa kibali na mradi ukatekelezwa maeneo yote hayo yatapata huduma ya majisafi na salama. Ninakushukuru sana.

Name

Esther Nicholas Matiko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza maji Kata za Bisumwa, Bukabwa, Nyankanga, Butuguri, Bwiregi, Buruma, Kyanyari, Buhemba, Mirwa na Kikirango?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Wananchi wa Mji wa Tarime wana adha kubwa sana ya maji, na tegemeo lao kubwa; na wanaishukuru Serikali kwa Mradi mkubwa wa Maji Ziwa Victoria wa shilingi bilioni 134 lakini mradi huu ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu. So far wamepeleka shilingi bilioni 24 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba hizi shilingi bilioni 110 zinaenda ili mradi huu ukamilike ndani ya muda na kuweza kupunguza adha ya maji kwenye Mji wa Tarime? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kabisa kwamba Mheshimiwa Esther Matiko ameendelea kupigania sana wananchi wake wa Tarime Mjini, na pia ameendelea kuhakikisha kwamba mradi huu anausukuma ili uweze kupata fedha na uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba mradi huu unaenda kuwa mwarobaini, lakini mkakati wa Serikali sasa wa namna gani mradi huu unaenda kukamilika, ni kupunguza utitiri wa kutangaza miradi mingi wakati tuna miradi ambayo bado haijakamilika na haijaanza kutoa matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tunaenda kuhakikisha kwamba badala ya kutangaza miradi mingi na kuzigawanya fedha ambazo zingeenda kukamilisha miradi kama hii, sasa tunaenda kuweka hitimisho katika utaratibu wa namna hiyo, na mkakati wetu ni kumaliza miradi viporo. Tukishamaliza baadaye tutaendelea na miradi mingine ambayo tutaweza kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mradi huu ni kipaumbele kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tuna uhakika mradi huu utakamilika na wewe mwaka 2030 utarudi, ahsante sana.

Name

Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Primary Question

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza maji Kata za Bisumwa, Bukabwa, Nyankanga, Butuguri, Bwiregi, Buruma, Kyanyari, Buhemba, Mirwa na Kikirango?

Supplementary Question 3

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri wa Maji alifanya ziara kwenye Mkoa wetu wa Songwe na alipofika pale wataalamu wa jimbo langu walimpatia andiko au maombi ya barua ili kuunganisha miradi ya Kijiji cha Muheza, Manda, Rukwa, Namkukwe, Gua Songambele na Halyongo liwe andiko moja tuweze kupata mkandarasi, na alichukua barua hiyo lakini mpaka sasa hakuna majibu. Ni lini tutapata barua hiyo ili mkandarasi aweze kupatikana kuanza kujenga miradi ya vijiji vitano kwa thamani ya shilingi bilioni 1.5?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nikiri nilifika jimboni kwa kaka yangu Mheshimiwa Mulugo na tulifanya ziara, na tulipokea andiko hilo, lakini ilikuwa tayari ndani ya bajeti ya fedha ambayo inaelekea mwishoni, na sasa tuko kwenye mchakato wa kuanzisha maandalizi ya kuelekea kwenye bajeti ya 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kuwa tutafanya tathmini vizuri na kujiridhisha na tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge, na tukisharidhika sasa kwamba tunaenda kutekeleza kwa namna gani, basi tutauingiza kwenye bajeti ya mwaka 2026/2027 ili ukatekelezwe katika vijiji hivyo vitano na wananchi wake wapate huduma ya majisafi na salama. Ninakushukuru sana.