Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Stephano Luhende

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Primary Question

MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:- Je, lini usajili wa Bodi ya Wanajiolojia nchini utakamilika ili kulinda na kuongeza ufanisi katika shughuli za utafiti na uchimbaji madini?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya mara ya pili. Suala hili la usajili ya Bodi ya Wajiolojia limeanza kushughulikiwa na Wizara tangu mwaka 2017 na limekuwa ni tatizo sugu sana kwa muda mrefu na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri Mkuu, Mawaziri mbalimbali wameweza kuhudhuria makongamano ya taasisi hii tunayotarajia kuisajili ya hawa wataalamu wa kijiolojia.

Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi, sasa hivi kama Serikali tunaelekea kufanya utafiti nchi nzima kwa kurusha drone mbalimbali pamoja na njia nyingine za utafiti. Sasa Serikali imejipangaje kuhakikisha katika utafiti huo hatupati data za uongo kwa kuwa tunaenda kwenye utafiti tukiwa hatuna Bodi wa Wajiolojia ya kusimamia ubora wa taarifa hizo za kijiolojia pamoja na policy...

SPIKA: Mheshimiwa, twende kwenye swali.

MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na vishoka wengi sana mtaani wanaendelea kutapeli wachimbaji wadogo wakijiita wao ni wataalamu wa kijiolojia. Serikali imejipangaje kuthibiti hili tatizo kwa sababu tunaendelea na shughuli za madini, lakini hatuna bodi ambayo inasaidia kuondoa hili tatizo? (Makofi)

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Luhende, Mbunge wa Bukene kwa sababu ya maswali yake kuhusu hii bodi ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu. Pili, nitambue kwamba Jimbo lake la Bukene ni moja ya maeneo yetu ya madini ya dhahabu, kwani yanapatikana pia huko kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ubora wa data inayotafutwa katika tafiti zinazoendeshwa na Taifa hili kwa maelekezo ya mama, Mheshimiwa Dkt. Samia zinasimamiwa kwa umakini mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwajulisha Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba kati ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kongwe na yenye uzoefu wa hali ya juu na wataalamu wanaojitosheleza ni Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ijulikanayo kama GST. GST imeanzisha mwaka 1925 ina miaka 101 sasa na ndiye msimamizi mkuu wa tafiti hizi zinazokwenda kufanyika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika tafiti yoyote kubwa inayokwenda kufanyika na inayofanyika, kunakuweko na mshauri mwelekezi mtaalamu anayetoka katika kampuni ya Kimataifa yenye uzoefu ambaye ndiye anayefanya kazi mbili za muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kwanza, anafanya kitu kinachoitwa quality assurance kuhakikisha kwamba data inayokusanywa ina vigezo vyote vya ubora wote unaotakiwa, lakini pia anafanya quality control kuhakikisha kwamba data inayokusanywa imesimamiwa itoe majibu yanayotarajiwa. Isitoshe katika kuhakiki hiyo data na kuikamilisha Taasisi ya GST ndiye custodian, ndiye anayetunza data zote kwa ajili ya walaji wawekezaji wakubwa, na wawekezaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la vishoka, ninaomba tena niseme hapa kwamba GST pamoja na STAMICO ambaye ndiye mlezi mkuu wa wachimbaji wadogo ambao ndio wanaumizwa sana na hawa vishoka, wana mandate na jukumu la kuwasimamia wachimbaji wadogo. Nitoe wito kwamba wasiwatumie wanajiolojia ambao hawajahakikiwa na GST kwa sasa wakati ambapo hatuna bodi.

Mheshimiwa Spika, kazi ya GST ni kutoa ushauri, ni kusaidia kupima sampuli, na pia ina watalaamu wanaoweza kutumiwa. Kwa hiyo, unapomchukua ambaye sio wa Serikali, pitia GST uliza kama huyu mtu anafaa?

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kwa sababu hili suala lake ni la muhimu sana, ninaomba tu nitoe wito kwamba kwa kuwa bado bodi hii haijasajiliwa, na sisi pia tuko nyuma yao kuwasukuma wasajiliwe. Bodi hii itakaposajiliwa, kazi yao siyo kuhakiki data, wala ubora wa data, kazi yao ni kuwadhibiti wa jiosayansi ambao wamesajiliwa.

Mheshimiwa Spika, hiyo bodi wanapokwenda kufanya kazi yao, wawe na sifa, na Watanzania watakwenda kuwatumia hao sasa katika tafiti zao. Wakishasajiliwa, usimchukue mtu ambaye hajasajiliwa na bodi hii ambayo inakwenda kuanzishwa siku za karibuni. Ahsante sana. (Makofi)