Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kutoka Serikalini, nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara hii inao upana wa mita saba ambazo kwa kweli ni viwango vya zamani sana. Nataka kufahamu kwamba je, huu upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umezingatia viwango vya sasa vya upana wa barabara ili watakapoanza kuijenga magari yaweze kupishana bila usumbufu kama ilivyo sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Barabara ya kutoka Mlalo kwenda Lushoto kipande cha kutoka Nyasa kwenda Majulai kilomita tatu, sasa ni takribani mwaka mmoja mkandarasi ameshasaini mkataba, lakini bado hajapewa barua ya uthibitisho kutoka Serikalini. Je, ni lini Serikali itatimiza jukumu hili ili mkandarasi yule aweze kuendelea na kazi?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu ambao umefanyika umezingatia viwango vya sasa vya upana wa barabara na carriageway ya barabara zetu huwa ni mita tatu na nusu kwa kila upande. Kwa hiyo upana wa barabara unakuwa ni mita saba ambao unaruhusu magari kuweza kupishana. Kilichoongezeka hapo ni kwamba tutapanua sasa yale mabega ya barabara (shoulders) kila upande mita moja na nusu. Kwa hiyo, barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 10 kwa maana ya barabara ambayo itakuwa inaweza kutumika tofauti na ilivyokuwa zamani, mita saba na nusu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kipande alichokisema, ni kwamba tayari tumekwishasaini mkataba na mkandarasi, muda wowote tukishamlipa fedha za awali ataanza kufanya kazi hiyo na tutaanza na kilometa tatu kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
Name
Suma Ikenda Fyandomo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 2
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya kuanzia Katumba – Suma – Mwakaleli – Ruangwa kutokea Tukuyu Mjini ni ya muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Rungwe. Bararaba hiyo inajengwa kwa kusuasua sana. Sasa, ninaomba kujua na wananchi wa Wilaya ya Rungwe wasikie, je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika? Ahsante.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli hiyo barabara mkandarasi ameshaanza kazi, na bahati nzuri mara baada ya kuteuliwa ni kati ya barabara ambazo niliweza kuzitembelea. Kinacholeta changamoto kubwa, moja ni kwamba eneo alilolitaja ni moja ya maeneo ambayo yanapata mvua nyingi sana. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo kwa sasa hawezi kufanya.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kusuasua kwake, tumetoa maelekezo, na mkandarasi huyu ameshakutana na viongozi wa TANROAD Makao Makuu, kwa maana ya viongozi wao wa juu kuhakikisha kwamba zile kazi ambazo zinaweza kufanyika zinafanyika.
Mheshimiwa Spika, kazi hii ni muhimu zaidi pia kwa sababu barabara iliyokuwa inatumika, nyingine ameshaivuruga. Kwa hiyo, tumemhimiza ili aweze kuhakikisha kwamba zile diversion zote zinapitika na barabara iweze kukamilika kwa muda kama ilivyo kwenye mkataba.
Name
Ghati Zephania Chomete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 3
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Barabara ya Musoma – Makojo – Busekera ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini. Je, ni lini sasa ujenzi huu utaendelea?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii ilishapata kibali cha kuanza kujengwa na tuko kwenye hatua za mwisho kabisa za manunuzi ili barabara hiyo iweze kuanza kujengwa.
Name
Arif Suleiman Premji
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 4
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara kwa kiwango cha lami Barabara ya Ziwani – Madimba – Msimbati – Madimba – Tangazo – Kilambo, kwani kupitia Kikao cha RCC jukumu hilo walipewa watu wa TANROADS, na ukizingatia feasibility study pia ilishafanyika?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge. Tunajua umuhimu wa barabara hiyo ambayo inaenda huko Msimbati. Sisi kama TANROADS tulishafanya upembuzi, tulishafanya usanifu na tulishapeleka maombi Wizara ya Fedha, ambao ninajua wanaandaa malipo, ili tuweze kupata kibali cha kuitangaza barabara hiyo. Hii pia ni barabara ambayo inakwenda Daraja la Kilambo ambalo tunashirikiana na wenzetu wa Mozambique, na vile vile wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Name
Edward Olelekaita Kisau
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 5
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Bajeti ya Mwaka 2025/2026 tulipitisha Barabara ya kutoka Kibaya – Kisima kilometa 50 zijengwe. Je, ni lini barabara hii inaanza?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii tunategemea kupatikana kwa fedha. Tayari sisi tumeshaomba fedha za awali ili mkandarasi aweze kulipwa, na akishalipwa, basi kazi hiyo ya kuanza kuzijenga hizo kilometa 50 itaanza.
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 6
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa upande wa Kanda ya Kaskazini kuanzia Tanga mpaka Singida, kipande korofi cha barabara ambacho kimerekebishwa mara nyingi zaidi ni kipande cha Dareda – Gehandu, kutoka Jimbo la Babati Vijijini kupitia Jimbo la Hanang – Singida. Barabara hii imeshakarabatiwa kwa muda mrefu na bado imekuwa ni sehemu korofi.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuanza upya kukwangua kipande kile cha barabara na kujenga lami mpya ili kusaidia uchumi wa Kanda ya Kaskazini?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kipande hiki cha Dareda – Gehandu ni kipande ambacho kiko kati ya Kateshi na Singida. Sisi kama Wizara tumeiangalia kama ni barabara ambayo imechoka, yaani imeshafika mwisho. Si hiyo tu, ni barabara ambayo sasa hivi baada ya kuwa na maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga, magari yanayopita ni makubwa sana. Kwa hiyo, tumeiweka kuwa ni kati ya barabara ambazo zimewekwa kwenye mpango wa kuzitengeneza kwa matengenezo makubwa, kikiwepo hicho kipande cha Kateshi – Singida, ambapo kipande hicho alichokisema kipo hapo katikati.
Name
Jafari Wambura Chege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 7
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya Utegi – Shirati – Kirongwe yenye kilometa 56, kwa bahati nzuri kilometa 27 za Utegi – Shirati zilitangazwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami. Ninataka nipate status, so far barabara ile sasa imefikia wapi kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hiyo barabara inasubiri tu kufanya signing tutakapokuwa tumekamilisha taratibu zote.
Name
Zainab Rashid Kawawa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 8
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi wanatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha za ujenzi wa barabara ya kilometa 10 kwa Barabara ya Liwale – Nangurukuru. Barabara hii ina jumla ya kilometa 231. Pia barabra hii ndiyo kitega uchumi kikubwa sana kwa wanachi wa Liwale pamoja na wa Wilaya ya Kilwa...
SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais sifa moja kubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya 100%, je, ni lini sasa tutafuta kilio cha wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kutukamilishia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ili sasa Wilaya ya Liwale iweze kuunganishwa na wilaya nyingine kwa kiwango cha lami?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Lengo la Wizara, na kama alivyosema Awamu ya Sita ni kujenga barabara zote na hasa zinazounganisha barabara kuu na makao makuu ya wilaya ama makao makuu ya wilaya na makao makuu ya mkoa, ikiwepo hiyo Barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 231.
Mheshimiwa Spika, tumeshaanza kutoa hizo kilometa 10, lakini kikubwa zaidi katika hiyo barabara Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami, kulikuwa na changamoto kubwa sana za madaraja. Sasa tumejenga madaraja mengi sana katika huu mpango wa dharura ambao unaendelea kukamilisha ili kuhakikisha kwamba wakati tunatafuta fedha ya kujenga barabara yote wananchi hawa wawe na uwezo wa kupita kipindi chote cha mwaka.
Name
Florent Laurent Kyombo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 9
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Barabara ya Katoma – Gera – Bukabuye – Kanyigo – Bukwali – Kashenyei imekuwa ikijengwa kwa meta mia mbili mia mbili, na sasa hivi ni miaka 10 tuko kilometa tano. Ninaishukuru Serikali imeshafanyia usanifu na upembuzi yakinifu, Mheshimiwa Naibu Waziri ameitembelea, na nimeshafikisha ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri. Je, ni lini angalau nitapata bajeti ya kutosha angalau kilometa 15 hadi 20 barabara hii ianze kujengwa?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko kwenye kipindi cha bajeti, kwa hiyo, tuombe bajeti itakapokuwa imepitishwa, nina hakika tutaongeza kilometa kutoka hizo meta 200 tutakwenda kwenye kilometa nyingi zaidi. (Makofi)
Name
Abdallah Jafari Chaurembo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mombo – Soni – Lushoto km 36 kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 10
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Barabara ya Mbande – Kisewe – Msongola, je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hii barabara ilikuwa inasuasua na kimsingi ni kama ilikuwa imesimama. Mkandarasi tumeshamlipa na hatudai sasa hivi, na nina hakika tutahakikisha tunamsimamia ili aweze kukamilisha hizo kilometa ninadhani ni 3.8 kwa muda wa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwelekeze tu Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam aweze kuisimamia hiyo barabara ili tuweze kumaliza, maana yake ndiyo iliyokuwa imebaki kuwa na kipande cha barabara ambayo ni vumbi katika hiyo barabara kuja Chanika.