Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha wanawake wanashiriki katika miradi mikubwa ya uchukuzi, ikiwemo Mradi wa SGR?

Supplementary Question 1

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kwa namna gani Serikali imeandaa programu maalumu au mafunzo ya uwezeshaji ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika miradi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali imeweka mikakati gani kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma katika fursa za zabuni na uwezeshwaji kiuchumi katika miradi mikubwa ya Serikali? (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janeth, kama ambavyo ameongezea. La kwanza, ametaka kufahamu programu na mafunzo mbalimbali, ambazo kimsingi Serikali hii inafanya katika kuimarisha wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, msingi namba moja ni uwepo wa sheria na miongozo mbalimbali. Kwa hiyo, cha kwanza Serikali inahakikisha kwamba, sheria, miongozo na kanuni mbalimbali ambazo zinawapa fursa wanawake zinapewa msukumo wa kipekee, lakini pia ziko programu mbalimbali kama vile mafunzo ambayo kwa mfano wenzetu wa TanTrade wanayo, wenzetu wa Bodi ya Wakandarasi wanayo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya elimu kwa vitendo (internship) hapa yameongelewa mara kadhaa. Yote hiyo ni kuwajengea uwezo wanawake kuhakikisha kwamba, wanapata uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeweka mafunzo muhimu ya kiufundi, kama vile kupitia vyuo vyetu vya VETA, ambapo tunawajengea uwezo wanawake, wakimaliza, wakipata ufundi huo, waweze kwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu kuwa na nguvu ya kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele mbalimbali katika utoaji wa ajira, yote haya pamoja na mengine, imekuwa ni mambo muhimu ambayo tunayafanya, kama sekta, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu mbalimbali katika masuala ya fidia, kwamba, fedha mtakazopata zitumikaje, ili isije ikatokea mtu amepata compensation halafu tena zile fedha amezitumia vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kama tulivyozungumza, mikakati mbalimbali inatolewa kuhakikisha kwamba, wanapata nafasi kama vile kwenye zabuni na kadhalika. Hii ni pamoja na fursa za kielimu. Hapa kwenye elimu, nchi yetu imetoa nafasi kubwa kwa mwanamke kuhakikisha kwamba, kila mtoto wa kike anayetaka kusoma shule au anayetaka kwenda shule kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu, anashiriki kikamilifu bila ubaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inatoa fursa maalum kama vile ambavyo Mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake amekujanavyo, kama vile Samia Scholarship Award, ambayo kimsingi inawasaidia watoto wa kike waliofanya vizuri kwenye masomo mbalimbali, kama vile sayansi, waweze kupata msukumo wa kipekee na kuwajengea uwezo waweze kufikia ndoto zao ambazo kimsingi wanazihitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, financial institution zetu (taasisi za kifedha) zimekuwa ni maeneo mengine inapotokea mwanamke ana bidii katika shughuli za uzalishaji mali, wanatoa msukumo wa kipekee katika kumpa mikopo, ili kuhakikisha kwamba, wanawake kwenye nchi yetu wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Sheria zetu za Manunuzi, imetoa fursa na upendeleo maalumu, kwamba 30% ya kandarasi zetu au tender zetu, basi msukumo utolewe kwa wananchi, kwa wanawake, na pia, upande wa udhibiti vitendo vya kikatili ni moja kati ya mikakati ambayo Serikali inafanya, ili kumfanya mwanamke asijisikie mnyonge kwenye jamii, ashiriki kwenye uzalishaji kama kiumbe mwingine kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kabla sijahitimisha ikiwa ni pamoja na kwenye uongozi, tayari unaweza kuona jinsi ambavyo wanawake wanashirikishwa katika masuala ya uongozi. Pamoja na kuwapa nafasi ya kushiriki kama watu wengine, bado wanapewa dawati la pekee kama vile kwenye Viti Maalumu ama katika uteuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kwamba, washiriki katika maamuzi wanapotunga sera au kanuni au sheria na wao waweze kuwa sehemu ya kuwasemea wanawake wenzao nchi nzima. Ninaomba kuwasilisha.

Name

Edefonce Joackim Canoni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha wanawake wanashiriki katika miradi mikubwa ya uchukuzi, ikiwemo Mradi wa SGR?

Supplementary Question 2

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Kalambo ina bandari ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi, uchumi wa Wilaya ya Kalambo na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bandari Serikali imewekeza shilingi 7,200,000,000 lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, imezama toka mwaka 2023. Nini mpango wa Serikali kuboresha bandari hii ili ianze kufanya kazi iwanufaishe wananchi wa eneo lile pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo? Ahsante.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza kufafanua kidogo. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuweza kutambua kazi ambayo Serikali imefanya kwenye upande wa Bandari yetu ya Kalambo, Mkoani Rukwa, ambapo ni moja ya bandari ambazo zilirasimishwa, lakini pamoja na kurasimishwa Serikali iliona umuhimu ikaiendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, pamoja na dhamira njema ya Serikali kuiendeleza tulipata changamoto kubwa ya maji. Kwa hiyo, maji yalijaa na yale maji hayakujaa kwenye Bandari ya Kalambo peke yake, ni karibu maziwa makuu yote. Tayari Serikali inaandaa mkakati, tumetafuta mkandarasi au mshauri mwelekezi, ambaye anatusaidia kutuambia nini tukifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni katika kutatua changamoto ya maji yaliyojaa kwa sasa hivi. Mbili, in long run, ni tufanye nini, ili tatizo kama hili likijitokeza, basi lisiweze kuathiri bandari zetu na hivyo, wananchi wa Kalambo na maeneo mengine wanufaike na bandari ambazo zipo kwenye maeneo yao.