Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Primary Question
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa shule ya sekondari eneo la Mafizi ili kupunguza umbali kwa wanafunzi wa Mafizi na Nyani?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebakisha mwaka mmoja na miezi minane kuingia katika utekelezaji wa sera yetu mpya ya elimu ambayo itahitaji vijana wa Darasa la Sita na Darasa la Saba itakapofika Januari, 2028 wote waende sekondari. Pale sasa ninataka kujua, je, nini mpango wa Serikali wa haraka kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule pale Mafizi kwa lengo la kuhakikisha vijana wa Mafizi, Nyani na kutoka shule mpya ya Visimavitatu waweze kupata elimu katika eneo lile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba shule takribani 3,000 zinajengwa upya kwa lengo la ku-accommodate hawa vijana wa Darasa la Sita na Darasa la Saba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mpango wa Serikali uliopo sasa kuhakikisha kwamba tunafanya resource mobilization kupata fedha kati ya shilingi trilioni mbili mpaka trilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo nchi nzima Tanzania kusaidia vijana wa Kitanzania? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Selemani Saidi Jafo, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Mbunge madhubuti sana na kwa kweli, anawatendea haki wananchi wa Jimbo la Kisarawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo ni nguli sana wa masuala ya TAMISEMI, pia ninafahamu kwamba kwa kweli kupitia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, Darasa la Sita na Darasa la Saba ya mwakani, 2027, watajiunga kwa pamoja Kidato cha Kwanza Januari, 2028.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya madarasa yatakayohitajika ni 23,226, maabara 9,366, na matundu ya vyoo 46,632. Serikali imeshafanya tathmini, tutahitaji kuwaingiza Kidato cha Kwanza wanafunzi 3,021,177. Kwa hiyo, Serikali hii kwanza tunatambua kwamba katika eneo la Mafizi na Nyani tunafanya tathmini ili tuongeze shule nyingine katika maeneo mbalimbali na kusogeza huduma za elimu karibu zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika tathmini inayoendelea ya kutambua maeneo ya kujenga shule, tutatoa kipaumbele eneo la Mafizi na Nyani pia ili kama linakidhi vigezo hivo, shule iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga imara na madhubuti kuhakikisha wanafunzi wote 3,000,000 Januari, 2028 watakwenda madarasani bila changamoto yoyote, na tayari tunaendelea ku-mobilize resources, na kwa hakika wanafunzi wote watakwenda kwa mujibu wa Sera ya Elimu iliyopo sasa.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa shule ya sekondari eneo la Mafizi ili kupunguza umbali kwa wanafunzi wa Mafizi na Nyani?
Supplementary Question 2
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Wanakijiji wa Kata ya Salama, kijiji cha Kurusanga, wametoa eneo ekari 50, wamefyatua matofali ya block yaliyozidi ya Serikali 3,000, wamechanga fedha, na sasa wanazo shilingi milioni 21 benki, wanataka kujenga sekondari. Ni lini Serikali itawaunga mkono kujenga Sekondari ya Kurusanga?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sehemu muhimu ambayo Serikali inatoa kipaumbele ni kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya huduma za kijamii zikiwemo shule. Kwa hiyo, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Getere na wananchi katika kijiji hicho kwa kutoa eneo la ekari 50, kufyatua tofali na kuendelea kutoa michango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawahakikishia kwamba katika mpango wa utekelezaji wa sera mpya ya elimu, tayari timu zetu zinaendelea kufanya tathmini na kutambua maeneo ambayo yana sifa za kuongeza shule nyingine ili tuweze kujenga shule hizo za sekondari na wanafunzi wetu Januari, 2028 waingie madarasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifikia eneo hilo na tutaunga mkono juhudi za wananchi kuhakikisha shule hiyo inajengwa ikiwa itakidhi vigezo kwa mujibu wa taratibu za elimu.
Name
Tinnar Andrew Chenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa shule ya sekondari eneo la Mafizi ili kupunguza umbali kwa wanafunzi wa Mafizi na Nyani?
Supplementary Question 3
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Shule ya Sekondari Busangwa iliyopo Kata ya Sakasaka katika Jimbo la Kisesa ina wanafunzi wa kike takribani 250, lakini hakuna mwalimu wa kike hata mmoja. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kike? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nipokee hoja ya Mheshimiwa mama yangu, Mheshimiwa Mama Chenge, lakini nitoe tu ufafanuzi ili kuweka rekodi sawa kwamba tunafahamu umuhimu wa walimu wa kike katika shule zetu zote za wanafunzi wa kiume na wa kike. Tunafahamu pia kuna mahitaji maalum ambayo mara nyingine ni vizuri mwalimu wa kike akiwa katika shule hizo. Kwa hiyo, suala hilo tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
Name
Nyamizi Simon Mhoja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa shule ya sekondari eneo la Mafizi ili kupunguza umbali kwa wanafunzi wa Mafizi na Nyani?
Supplementary Question 4
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Shule ya Msingi ya Sanze Wilaya ya Kisarawe iliyopo Kisarawe, ni jumuishi na imeanza kupokea watoto wenye ulemavu wa bweni kabisa pale. Hata hivyo, shule ile haina walimu ikiwemo hata mkalimani wa lugha ya alama. Sasa, ni lini Serikali itafikiria kuboresha elimu maalum ili hawa wanafunzi waweze kupata haki yao? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba zipo shule maalum ambazo pamoja na wanafunzi wengine, ina wanafunzi wale wenye mahitaji maalum na hususan wenye ulemavu. Serikali imeendelea kila mwaka kuajiri walimu kadiri wanavyotoka katika vyuo vyetu kwa ajili ya kuwapeleka kwenye shule ambazo zina wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba safari ni hatua, tunakwenda kwa hatua na tunaendelea kuboresha pia mafunzo kwenye vyuo vyetu ili walimu wenye mafunzo maalum ya elimu maalum waweze kufika kwenye shule zetu. Kwa hiyo, tutatoa kipaumbele pia katika shule ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja.