Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amina Ali Mzee
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza gati katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuhudumia meli nyingi zaidi?
Supplementary Question 1
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, pia ninaipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uendelezaji bora wa Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ni yapi manufaa ambayo yamepatikana katika uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam hasa kutokana na uwekezaji ambao umefanyika mwaka 2023?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni ipi mikakati ya Serikali katika kuboresha Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza biashara na kuweka ushindani katika East Africa na SADC?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum ambaye anawakilisha kundi la vijana, kwa sababu kupitia maelezo yake na ufuatiliaji wake anathibitisha umuhimu na namna ambavyo vijana wa CCM walivyo makini kufuatilia maendeleo ya vijana wenzao katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kazi kubwa imefanyika na ninashukuru kwa pongezi zake ambazo amezielekeza moja kwa moja kwa Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono makubwa na mapana ya namna ya kutumia bandari zetu kugeuza kuwa uchumi kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari kwenye Taifa letu, upo kwa mujibu wa sheria. Hivyo basi, baada kuona umuhimu mkubwa, ndiyo maana Serikali ikaamua kufanya hivyo. Ninapenda sasa kumjibu kwenye hoja yake aliyozungumza kuhusu manufaa ambayo tumeyapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ifahamike kwa Watanzania na Wabunge wote kwamba tuliposhirikisha sekta binafsi, especially DP World kwa ajili ya kuendesha kitengo namba moja, mwaka 2024 haikuwa mara ya kwanza. Mara ya kwanza, kazi hii iliwahi kufanyika mwaka 2000 ambapo wenzetu wa TICTS walipewa mkataba wa zaidi ya miaka 20 kuendesha sehemu ya makasha pale Dar es Salaam. Mwaka 2024 tulishirikisha wenzetu wa TICTS pamoja na wenzetu wa DP World kitengo cha kwanza, pamoja na East Africa Gateway Terminal Limited kitengo cha pili ili watusaidie katika kuendesha. Manufaa ambayo tumeyapata ni mengi na makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kwenye utoaji wa huduma ya meli. Hapo zamani, kuna kitu kilikuwa kinaitwa ship turnaround time, yaani muda ambao meli inatumia kuanzia inapofika, inakwenda kuhudumiwa na inaondoka. Zamani zilikuwa zinatumika takribani siku 30. Zimeshuka mpaka kuwa siku nne kutokana na kazi kubwa ambayo wanafanya wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna kitu kinaitwa Ship turn at berth, yaani muda ambao meli inahudumiwa ikiwa kwenye eneo la gati. Zamani tulikuwa tukitumia kuhudumia mpaka siku 10, lakini imeshuka mpaka siku tatu. Hii yote inaongeza ushindani wa bandari yetu. Ndiyo maana ukienda kwenye ranking leo za bandari unakuta bandari yetu imekuwa ya 373 wakati ya wenzetu majirani zetu pale Mombasa imekuwa ya 393. Kwa hiyo, tuko mbele yao kiufanisi. Tembeeni kifua mbele Watanzania, kwa sababu kazi hii ni nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa makubwa ambayo tunaweza kuyazungumza, mengine ni kwenye upande wa makasha. Makasha yaliyokuwa yanahudumiwa wakati huo kwa Bandari ya Dar es Salaam peke yake ilikuwa 728,000, leo imefika 1,080,000. Hivyo, kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa miongoni mwa Bandari kubwa katika Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni shehena kwa maana ya mzigo. Wakati huo tulikuwa tunahudumia tani 16,000,000 kwa maana ya Bandari ya Dar es Salaam. Leo imefika tani 27,000,000 ndani ya muda mfupi ya muda miaka michache. Hii yote ni kwa sababu ya uwekezaji ya ambao tumeufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye idadi ya meli. Meli zilizokuwa zinahudumiwa kwenye Bandari ya Dar Salaam peke yake ilikuwa ni meli 880 zimeongezeka mpaka kufika meli 1,245, wakati meli zote Kitaifa zimeongezeka kutoka meli 4,241 mpaka meli 4,888. Hii yote ni kwa sababu ya maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuamua kushirikisha wawekezaji katika bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, magari yaliyokuwa yanahudumiwa mwaka 2021/2022 mpaka 2023, yalikuwa ni machache, takribani magari 100,047. Mara baada ya kufanya maamuzi hayo, magari yanayohudumiwa yamefika 216,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, hata mapato ya TPA yalikuwa shilingi bilioni 896 kwa mwaka. Mara baada ya kufanya maamuzi haya, mapato yakaongezeka mpaka yakafika takribani shilingi trilioni mbili, ya TPA 1.3, na yanayobaki ya wawekezaji. Pesa hiyo ndiyo imekwenda sasa kwenda kujenga na bandari nyingine kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, hata wenzetu wa TRA wameongeza fedha zao maradufu zaidi. Fedha kwenye Mfuko wa Serikali zimeongezeka, ndiyo maana hata wanafunzi wa elimu ya juu sasa wamekuwa wengi zaidi takribani 235,000 kutoka 170,000. Kwa sababu gani? Mheshimiwa Dkt. Samia ameongeza fedha kwenye mfuko wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, shehena ya nchi yetu inayokwenda kwenye nchi jirani ilikuwa ni tani 5,600,000. Kutokana na ufanisi na mzigo kuongezeka, shehena imeongezeka na kufikia milioni 12.6. Hata Wabunge wenyewe wanakubali na kusema kwamba kweli Mheshimiwa Dkt. Samia ameamua kuibadilisha nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza je, ni ipi mikakati ambayo Serikali hii ya Awamu ya Sita imejiwekea kuifanya Bandari yetu ya Dar es Salaam kuwa shindani? Ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Amina Ali Mzee ambaye anatoa sauti kwa niaba ya vijana wa nchi hii wanaopenda kuona nchi yetu ikinufaika na uchumi wetu. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anayo mikakati mingi, ninaomba nitaje michache:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, ni kuhakikisha kwamba tunaongeza gati kwenye Bandari Dar es Salaam na tayari Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ameshaanza vikao, na ameielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania iharakishe mchakato huo ili tupate gati nyingi zaidi.
Muheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunaboresha reli yetu kama ulivyoona ule mradi ambao tunaufanya na mzigo tunaobeba unafanyika wakati Reli ya TAZARA ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia anaihubiri haijaanza kufanya kazi vizuri. Reli ya SGR haijaanza kutekeleza kazi yake vizuri. Je, tukikamilisha SGR, na kukamilisha TAZARA, hali itakuwaje? Maana yake ufanisi wetu utaongezeka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wote ni mashahidi, kila akisimama hapa Waziri wetu Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa Mnyaa anaelezea kwa kina na uchungu mkubwa umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta binafsi. Moja ya mkakati wetu ni kuendelea kuwaalika Watanzania na wasio Watanzania, maadamu ni wawekezaji, waje kuwekeza kwenye sekta yetu. Walete meli, wajenge SGR, walete matreni na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni nini? Kuiongezea uwezo mamlaka yetu. Hapa asubuhi mmesikia ninyi wenyewe kwamba tunakwenda kushirikisha sekta binafsi kwenye kujenga barabara kuondoa msongamano kutoka maeneo ya Kibaha mpaka Chalinze, kutoka Chalinze mpaka Morogoro na maeneo mengine. Yote hii sasa ili mzigo unaotoka Bandari ya Dar es Salaam uweze kufika maeneo husika katika muda ambao umepangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved