Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maryam Azan Mwinyi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Primary Question

MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma ili wapate fursa za masoko, mafunzo na mitaji?

Supplementary Question 1

MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza, kwa niaba ya Mheshimiwa Mariam Nyoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha wanawake wanapata taarifa sahihi, fursa na mitaji na masoko mkoani Ruvuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, Serikali inashirikiana vipi na sekta binafsi au taasisi za kifedha kuongeza fursa za masoko hapa nchini? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Maryam Mwinyi kwa kumwakilisha vyema Mheshimiwa Mariam Nyoka. Hakika ameitendea haki hiyo nafasi. Ninapende kujibu maswali yako mawili; kwanza, namna ambavyo wanawake wanapata taarifa kuhusiana na hii mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi kama Wizara tuna Kitengo cha Habari ambacho kinafanya kazi kwa weledi mkubwa, kinatoa taarifa katika mitandao ya kijamii. Pia, sisi kama Viongozi wa Wizara tunaendelea kuongea mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ili wananchi wote waweze kupata taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika mikutano mbalimbali ya vijiji katika maeneo ya kata, kule tunao Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii na wenyewe wanashiriki katika mikutano ile ya shughuli zao za maendeleo ya maeneo yao, pia na ajenda ya namna ya kupata hii mikopo wanapewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tuna majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi nchi nzima na sasa hivi mikoa yote Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amehakikisha yamesimama vizuri, lakini wilayani na sasa hivi tunasisitiza hadi kwenye kata, majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi yaweze kuimarishwa na wanawake wengi waendelee kujitokeza kujiunga kwa sababu ni wanawake wote wanastahili kuingia katika majukwaa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majukwaa yale katika ajenda mbalimbali watakazoongea, wataambizana namna ya kupata mitaji, lakini wataoneshana fursa mbalimbali, lakini vilevile haya masoko pia wanapata kufundishana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kama Wizara, tunashirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Halmashauri kwa maana ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi. Wote hawa ni kuhakikisha kwamba tunaweza kuwafikia wananchi, na wote wanapata hii fursa ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona makundi haya yote yanaweza kufikiwa kwa ukubwa wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema, namna gani Serikali inashirikiana na sekta binafsi ama taasisi za kifedha kuongeza fursa za masoko kwa vikundi vya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma? Ninampongeza sana Mheshimiwa Mariam Nyoka, amekuwa akifuatilia sana suala la kuhakikisha wanawake wameshapata mikopo. Wanapataje sasa masoko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme, sisi kama Serikali tunashirikiana na taasisi binafsi hasa mabenki waweze kutoa fedha kwa kutoa kwanza elimu ya fedha na vilevile namna ya kupata masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Tanzania Women Chamber of Commerce, wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana. Wamesimamia wanawake ambao ni wajasiriamali wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, wote wanaungana. Kwa hiyo, wanabadilishana uzoefu, wanasafiri ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakina mama wanaendelea kuyapata masoko ndani na nje ya nchi. Hivi karibuni Tanzania Women Chamber of Commerce inaratibu wanawake wajasiriamali wadogo wadogo kwenda kwenye maonesho ya 66 ya biashara ya Kimataifa huko Bulawayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, biashara mbalimbali ndogo ndogo, wakina mama wanapata mwanga, wanafika kule nchi jirani, wanapata kuongeza masoko mapya. Pia, hata hapa hapa Tanzania wamekuwa wakifanya haya yote pale Arusha, Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza, lakini tunaona namna makundi ya wanawake yanaendelea kuimraika. Vilevile, taasisi kama BRAC pia inaendelea kufanya vizuri kuona kwamba masoko yanapatikana kwa wanawake, lakini kama Wizara tunafanya kazi na Wizara karibia zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa wachimbaji wadogo wadogo, kwa maana ya Wizara ya Madini, unakuta pale kuna TAWOMA. Pia wanafundishana na kupeana taarifa mbalimbali kuhusu namna ya kupata masoko ya bidhaa zao na shughuli ndogo ndogo wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Chama cha Wahandisi Wanawake na wenyewe hawako nyuma, wanafanya vizuri sana na wanaoneshana kazi mbalimbali na wanashiriki kazi mbalimbali na wanapata masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Name

Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma ili wapate fursa za masoko, mafunzo na mitaji?

Supplementary Question 2

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna baadhi ya vikundi vya wanawake katika Mkoa wa Mtwara, hawajapata mikopo kwa takribani miaka miwili, wamekuwa wakifuatilia kutoka vijijini kwenda kwenye halmashauri zao za wilaya, je, Serikali inatoa kauli gani kwa Wakurugenzi ambao hawawezeshi upatikanaji wa mikopo kwa wanawake hao? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara. Ninampongeza sana kwa kazi nzuri dada yangu amekuwa akifuatilia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema kwa Wakurugenzi wote nchini, tafadhali sana msiangushe jitihada za Mheshimiwa Rais. Makusanyo ya ndani ya 10% ni haki ya msingi, zile asilimia nne wanawake kuzipata. Hivyo ninapenda kutoa wito kwa wanawake kufika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao bado hawajapata hii mikopo maafisa maendeleo yetu ya jamii tunaendelea kuwasisitiza kuwasaidia hawa wanawake kufikia vile vigezo vyote ili waweze kupatiwa mikopo. Wengine wanachelewa kupata, huenda anakosea kitu kidogo katika kukidhi vigezo vya kupata mkopo, hivyo Maafisa Maendeleo ya Jamii niwasihi sana wafanye kazi yao ili wanawake wote kwenye halmashauri zote ikiwemo ya Mtwara waweze kupata mikopo.

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma ili wapate fursa za masoko, mafunzo na mitaji?

Supplementary Question 3

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kipekee kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kazi nzuri anayoifanya, anapambana hata kupitia mitandao kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali hii, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa baada ya maeneo hayo ya utangulizi niulize swali langu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kufupi CCM ina lengo zuri la kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kule nyuma mikopo hii ilikuwa inatolewa na halmashauri, lakini kwa sasa mikopo imehamishiwa kwenye benki. Zipo changamoto ambazo zinajitokeza ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri mimi nimewahi kufanya kikao na vijana wa bodaboda, tunafahamu kwamba bodaboda ni sehemu ya ajira. Wanacholalamika ni kwamba hata kama kajaza fomu na kuweka viambatanisho vyote, mwisho wa siku hapati mkopo, na hapati majibu yoyote kwamba umechelewa kupata mkopo kwa sababu fulani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sikudhani, swali…

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nini sasa kauli ya Serikali katika kuhakikisha inapitia upya hizo changamoto ili kurahisisha mikopo kwa makundi hayo maalumu?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE WA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa pongezi, vile vile naomba kujibu swali hili kuhusu, changamoto zinazopatikana kwenye benki. Kwa sasa hivi sisi kama Wizara, benki tunayoitumia ni NMB. Kulingana na makubaliano tuliyoyafikia changamoto hizi kwa sasa hivi zimepungua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakati mikopo hii inatolewa pale halmashauri, ilikuwa, Mheshimiwa Diwani naamini unakumbuka namna ambavyo watu wanakopa hawarejeshi, kwa hiyo, wale wengine sasa wanashindwa kupata kwa sababu waliokopa awali hawajaresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutibu hilo, Serikali iliona ni vyema sasa tuweze kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya benki, wenzetu wana uzoefu na namna nzuri ya kufuatilia ili mikopo hii iweze kurejea ili kuwe na mzunguko kwa watu wengine, baada ya wengine kurejesha. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya kutoka halmashauri kwenda benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingi tumeweza kuzishughulikia, mambo mengi yaliyokuwa ni vikwazo, tumeweza kuongea na wenzetu wa sekta binafsi kwa maana ya benki, wameyaondoa kama matumizi ya hati, matumizi ya vyeti vya ndoa, tumeweza kuyaondoa ili kupunguza kero katika upatikanaji wa mikopo hii iliyotolewa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa bodaboda ninapenda tu kutoa taarifa kwamba kwanza wamepatiwa mkopo maalumu kabisa wa wafanyabiashara wadogo wadogo na wakapunguziwa mpaka riba, wakapewa kwa asilimia saba tu single digit kwenye mkopo. Yote hii ni kuona kwamba tunaendelea kuwawezesha wakuwe. Kama Wizara, tutaendelea kusimamia kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazoendelea kujitokeza tunaziondoa ili lengo la Mheshimiwa Rais liweze kutimia.

Name

Shadya Haji Omar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma ili wapate fursa za masoko, mafunzo na mitaji?

Supplementary Question 4

MHE. SHADYA HAJI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niendelee kuipongeza Wizara hii kwa mazuri ambayo wanayafanya na mengi tukiwa tunayashuhudia. Niende moja kwa moja kwenye swali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vingi vya akina mama vinakufa kwa sababu ya mitaji pamoja na masoko ya uhakika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha wanawake hawa na masoko ya EAC na SADC badala ya kutegemea masoko ya ndani?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE WA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Shadya kwa pongezi, lakini kuona kwamba Serikali inaunganisha haya makundi ya wanawake na masoko ya nje kama nilivyotoka kujibu swali langu lile la kwanza kwa mwuliza swali la msingi. Tayari tunafanya, ila niseme kwamba tunapokea huu ushauri ili kuongeza kasi ya kuona tunawapeleka makundi ya wanawake kwenye masoko ya nje zaidi.