Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninaomba tu masahihisho madogo, humu Bungeni hakuna Jimbo linaitwa Bunda Vijijini, kuna Jimbo linaitwa Bunda. Kwa hiyo, mnapo-address muwe mnajua kuna Jimbo linaitwa Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi shule za amali maana yake ni kwamba, wananchi walipokea malengo yake vizuri sana kwa sababu, ni shule za kiufundi. Nimeomba VETA humu zaidi ya miaka kumi, nikaambiwa tutakupa shule ya amali, ambayo ni shule ya ufundi. Shule imekamilika, sasa ni miaka mitatu. Sasa hizi fedha tukisema zipo kwenye bajeti maana yake, malengo ya kutekeleza hizo shule itakuwa ngumu. Ni lini sasa hizo fedha zitaenda ili wananchi waone kwamba, sasa wanaenda kujengewa shule ya ufundi, kama ilivyokuwa imependekezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Shule ya Sekondari Sanzati na Shule ya Sekondari Tingirima nimeenda pale wameshapima, wamejenga, majengo hayajakamilika yote, Serikali ilitoa fedha pale. Ni lini mtaenda kukamilisha majengo ya shule hizo?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ujenzi wa shule za amali za sekondari ni matokeo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2014, Toleo la 2023, ambalo mambo makubwa matatu yaliyopitishwa na sera ile, kwanza ni ujenzi wa shule za amali za sekondari ya chini kwa maana ya O-Level.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhakikisha kwamba, somo la maadili na uzalendo wa Taifa linafundishwa. Tatu, ni kuhakikisha kwamba, tunaendelea kuboresha sana elimu ya msingi kwa kuweka darasa la kwanza hadi la sita na kidato cha kwanza hadi cha nne, kwa maana ya madarasa 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ujenzi wa shule hizi za amali, kwanza unahitaji shilingi bilioni 2.6, ili ukamilike. Shule zote 103 zilipewa fedha awamu ya kwanza, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa shule za day na sasa Shule hii ya Manchimweru inatoa huduma, ina wanafunzi takribani 299 na awamu ya pili ipo kwenye mpango. Wakati wowote tutapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha shule hizi zote za amali, ili ziweze kutoa mafunzo yale yanayohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Getere kwamba, mpango huu ni endelevu. Tunakamilisha awamu ya kwanza, tutakwenda awamu ya pili, ili kukamilisha miundombinu ya shule za sekondari za amali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunayo mipango mbalimbali ya kuhakikisha shule zetu zote za sekondari za kata zinakamilishwa miundombinu yake kwa awamu. Tumeshajenga shule ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja na tayari inatoa huduma na tunafahamu kwamba, kuna upungufu wa baadhi ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ipo kwenye taratibu za kupata fedha ili kupeleka Bunda kwa ajili ya kukamilisha shule hiyo ili wanafunzi waweze kupata fursa nzuri ya kujifunza. Ahsante.
Name
Tinnar Andrew Chenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 2
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Chenge Sekondari iliyopo Kata ya Somanda pale Bariadi ilijengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2016, na kuna maabara ambayo ni two in one, lakini tangu kipindi hicho shule hiyo na maabara hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha maabara hiyo ili kuunga mkono juhudi za wananchi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza Serikali inatambua mchango mzuri wa wananchi wa Jimbo la Bariadi na Bariadi Mjini kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Secondari ya Chenge. Nakuhakikishia kwamba, Serikali ilishafanya tathmini, na tunayo orodha ya shule zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zote ambazo zimejengwa kwa fedha ya Serikali, kwa maana ya Halmashauri, yaani Serikali Kuu, tayari tunafahamu upungufu wa majengo na miundombinu inayohitajika. Tunaendelea na taratibu za fedha, ili tuweze kupeleka kukamilisha shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Shule ya Sekondari ya Chenge itapewa kipaumbele. Itapelekewa fedha ili tuhakikishe miundombinu hiyo inakamilishwa.
Name
Esther Nicholas Matiko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 3
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Shule ya Amali ya Nyandoto iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshakamilika miundombinu ya madarasa, ofisi, vyoo na nyumba ya Mwalimu, lakini shule hii ilijengwa nje ya mji, hivyo tunahitaji tupate fedha kwa ujenzi wa bweni na karakana, ili shule ianze. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha hizi kwa haraka?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba, shule hii imejengwa awamu ya kwanza na tunafahamu kwamba katika mpango wa ujenzi wa shule zote 103 za amali mabweni, karakana na mitambo yote ya kihandisi ni sehemu ya ujenzi wa shule zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga awamu ya kwanza, zimeanza kutoa huduma kama shule za kutwa; awamu ya pili inakwenda kujenga mabweni, karakana pamoja na miundombinu yote ya uhandisi ili kuhakikisha shule hizo zinatoa huduma inayotakiwa. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua za mwisho za kupata fedha kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu hiyo.
Name
Edwin Enosy Swalle
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 4
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Kidegembye, hasa pale kwenye Kijiji cha Image, ambako Mheshimiwa Naibu Waziri anapafahamu, wananchi wamejengewa shule nzuri sana ya amali, lakini ipo mbali na makazi ya wananchi, kwa hivyo, hakuna nyumba za waalimu wala karakana kwa ajili ya wale wanafunzi, na hakuna bweni. Ni lini Serikali itapeleka fedha, kwa ajili ya bweni, karakana na nyumba za waalimu pale Image?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa shule hizi tulianza na awamu ya kwanza ya shilingi milioni 584 na tulijenga miundombinu ya madarasa na shule zile zimeanza kutoa huduma, kwa maana ya shule za kutwa. Awamu ya pili, tunakwenda kutenga shilingi bilioni 1,600, kwa ajili ya kujenga miundombinu inayosalia, yakiwemo mabweni, karakana na kununua vifaa vya kihandisi, ili wanafunzi wanaojifunza masuala ya kiuhandisi waweze kuwa na mazingira bora ya kujifunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe, unayefanya kazi kubwa sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Lupembe, kwamba, Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua hilo, na tupo kwenye taratibu za kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha shule hizo zote 103, ili ziweze kutimiza lengo lililokusudiwa, ahsante.
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 5
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Serikali ilitoa mwongozo kwamba, inapeleka shule za amali katika majimbo ambayo hayakupatiwa Vyuo vya VETA. Je, ni lini Serikali itapeleka shule ya amali katika jimbo la Bumbuli, Wilaya ya Lushoto?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, Serikali iliweka kipaumbele kupeleka shule za mafunzo ya amali za sekondari katika majimbo au wilaya ambazo hazina vyuo vya VETA. Zoezi hilo limeendelea kufanyika na ndiyo maana tayari shule 103 zimejengwa, zipo hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, bado Serikali inaendelea kufanya tathmini kwenye maeneo yale yote ambayo yana uhitaji wa shule hizo na hayana vyuo vya VETA, tutahakikisha tunaweka mipango kwa awamu ili kufanikisha dhamira ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo, Mheshimiwa Mbunge, tutakwenda kufanya tathmini na kuona uwezekano wa kufanya jambo hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema.
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 6
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya jimbo langu ipo shule ya wasichana wenye vipaji maalum. Shule ile pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kuleta shilingi bilioni nne kwa ajili ya shule, lakini haina uzio, hivyo kusababisha wasichana wale na wenye changamoto, yaani wenye ulemavu, kuwa katika hatari ya usalama wao. Ni lini Serikali italeta fedha ili kujenga uzio katika ile shule, ili wasichana wetu, watoto wetu waishi katika mazingira salama zaidi? Ahsante sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, Serikali hii ya Awamu ya Sita, na kwa dhamira njema sana ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mpango mkakati wa kujenga shule maalum za wasichana kidato cha kwanza hadi cha sita katika mikoa yote 26, kote nchini. Tayari shule hizo zimesajiliwa na zimeanza kutoa huduma. Ujenzi wa shule zile uligharimu takribani shilingi bilioni nne nukta sita na tunafahamu kwamba, bado kuna miundombinu inayohitajika ukamilishaji wake zikiwemo fence za shule zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kwamba, Serikali inatambua uhitaji wa fence hizo. Ninatumia nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kuwasisitiza na kuwakumbusha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwamba, pia, katika mapato ya ndani wanayo fursa ya kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa fence hizo wakati Serikali Kuu ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha fence hizo.
Name
Dr. Wilson Charles Mahera
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule ya Amali Manchimweru?
Supplementary Question 7
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Bwilegi ni miongoni mwa kata ambazo vijiji vyake vipo mbalimbali sana katika Wilaya ya Butiama, lakini Kijiji cha Lyamsanga sasa hivi kwa muda wa miaka miwili, wananchi wameshakusanya mawe na mchanga trip 50 na kokoto trip 16. Je, lini Serikali itapeleka fedha ili wananchi wa Kijiji cha Lyamsanga waweze kupata shule ya sekondari? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Butiama na ninawapongeza sana wananchi kwa kutoa nguvu zao kukusanya mawe na mchanga, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ya sekondari. Ninaomba kutumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama, walete taarifa rasmi ya maandalizi kwanza, kama eneo linakidhi vigezo vya kuwa na shule hiyo ya sekondari. Pili, walete taarifa ya maandalizi kupitia mapato ya ndani na Serikali Kuu iweze kuona namna bora zaidi ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo ya sekondari.