Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholas Matiko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kimkakati ndani ya Mji wa Tarime?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kufuatia majibu ya Serikali, kwanza kabisa ningependa kusema wazi wawekezaji wengi hasa wale wakubwa wanapenda kuwekeza Mkoa wa Pwani, labda kwa sababu kupo karibu na Dar es Salaam. Huku pembezoni na kama ilivyo Mji wa Tarime, siyo rahisi sana kuweza kuvutia wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali imekiri kwamba kwa jiografia ya Mji wa Tarime, tuna upatikanaji mkubwa wa malighafi za kilimo, mifugo pamoja na madini. Pia, Mji wetu wa Tarime uko mpakani, na hivyo kuifanya Tarime Mji kuwa kituo kizuri tu cha kiwanda cha kuzalisha thamani.
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua kwa kuwa hasa bidhaa za ujenzi ni ghali sana kwa kule kwetu Mkoa wa Mara, na asilimia kubwa inatoa Kenya, Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka kuhakikisha kwamba inavutia wawekezaji wakubwa wa vifaa vya ujenzi kama uzalishaji wa mabati, nondo, vifaa vya maji ili waje kuwekeza kule ili kupunguza watu kwenda Kenya au kupata bidhaa Tanzania kwa gharama kubwa zaidi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa malighafi za kilimo zinapatikana, na pia tungependa kupata mwekezaji mkubwa ambaye anaweza kuchakata na kuwa na Kiwanda cha Biskuti kwa sababu tuna viazi vingi sana vinasafirishwa kuja huko mikoani au crips ambazo zinatokana na ndizi. Serikali haioni pia kuna haja sasa ya kumleta mwekezaji huyu mkubwa kuacha wale wadogo ambao umeeleza kwenye jibu lako la msingi?
Name
Denis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nikiri maelezo ya Mheshimiwa Mbunge. Tarime ni Wilaya ya kimkakati na hasa tunapozungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki iko mpakani na iko kimkakati, na ndio maana mkakati ambao tunao sasa hivi ni kuimarisha biashara katika mtengamano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki na kutumia Tarime na mikoa ya mipakani kama maeneo ya kimkakati wa Tanzania ku-access masoko katika Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Serikali inatoa rai kwamba tunatangaza vivutio ambavyo ni vya kikodi na visivyo vya kikodi hususan kwenye miradi ya kimkakati ambayo inaweza kuwekezwa katika maeneo maalum ya kiuchumi na hii ikiwemo misamaha na nafuu ya kikodi ili kuhamasisha wawekezaji kwenda nje ya maeneo ambayo tumeyazoea hasa katika mikoa ya Pwani ili ku-access soko kubwa zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tarime ambalo ni eneo la kimkakati ku-access masoko hayo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusiana na suala la kutafuta wawekezaji wakubwa. Kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Dira ya 2020-2050, lengo letu ni kuongeza thamani ya mazao, thamani ya madini yetu ambayo tunazalisha nchini, viwanda vya kimkakati ambavyo vinatoa ajira na kutuhakikishia pia uwepo wetu katika Jumuiya na ku-access masoko ya SADC pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved