Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asma Ali Mwinyi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Primary Question

MHE. ASMA ALI MWINYI aliuliza:- Je, Serikali ya Muungano na Zanzibar zina mpango gani wa kuunganisha na kukuza Utalii nchini kuzingatia bajeti, miundombinu na fursa za ajira?

Supplementary Question 1

MHE. ASMA ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, na pia ahsante sana Waziri kwa majibu yako mazuri uliyonipa. Ninaomba niongezee maswali mawili kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha kuwa ushirikiano katika Bodi hizi mbili za Utalii wa Tanzania na Kamisheni ya Utalii wa Zanzibar inaleta chanya ya moja kwa moja ya ongezeko la ajira kwa vijana wa Tanzania hususan vijana na wanawake, lakini kipekee vijana wa Jimbo la Welezo?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninaomba kuuliza. Je, Serikali italeta lini viashiria vya mafanikio (KPIs) vinavyopima ongezeko la utalii, mapato na ajira katika kupitia ushirikiano katika Bodi hizi mbili ya Utalii wa Tanzania pamoja na Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kwa maswali mazuri ya msingi Mheshimiwa Asma Ali Mwinyi Mbunge wa Welezo. Pia nimthibitishie tu kama nilivyojibu katika swali la msingi, moja, Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika swali la msingi tumeshaonesha kwamba tumeshasaini mkataba wa makubaliano kwa maana ya MoU katika kukuza Sekta ya Utalii nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii, na watalii wengi wanakaa muda wa kutosha hapa nchini. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana, hususan katika maeneo kama ya kuongoza watalii, malazi, usafiri, pamoja na sanaa (uchongaji wa vinyago pamoja na picha).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hayo tu ni sehemu ya mambo ambayo tunayafanya katika kuongeza ajira hususan kwa vijana na wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusu viashiria vya mafanikio ambavyo Serikali imekuwa ikifanya, kupitia taasisi zetu za Kiserikali ndani, kwa maana ukiangalia taasisi ya Benki Kuu ya Taifa, Uhamiaji, Bodi ya Utalii na Kamisheni ya Utalii Zanzibar zimekuwa zikitoa chapisho la kila mwaka kwa maana linalotoa zile taarifa za mwenendo wa utalii hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tumekuwa tukitumia kitu kinaitwa Visitor Tourism Exit Survey (utafiti mdogo pale watalii wanapotoka nchini) ambayo imekuwa ni sehemu ya kuonesha ule mwenedo na viashiria vya watalii hapa nchini. Kwa hiyo, hayo ni maeneo ambayo unaweza kwenda ukapata hizo KPIs ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza.

Name

Sheila Edward Lukuba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASMA ALI MWINYI aliuliza:- Je, Serikali ya Muungano na Zanzibar zina mpango gani wa kuunganisha na kukuza Utalii nchini kuzingatia bajeti, miundombinu na fursa za ajira?

Supplementary Question 2

MHE. SHEILA E. LUKUBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha na kutangaza geti la Msolwa - Kilombero kuelekea Hifadhi ya Nyerere ili kukuza zaidi utalii?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu Mheshimiwa Sheila kwamba, geti la Msolwa ni moja ya geti ama ninaweza nikasema ni kanda maalum kwa ajili ya Kanda ya Solwa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuandaa siku maalum kwa ajili ya uzinduzi wa geti hilo jipya la Msolwa ili iwe kama sehemu ya kimkakati ama promotion ya kutangaza sekta ya utalii pamoja na uwekezaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho, na hivi karibuni Mheshimiwa Mbunge atapata hiyo taarifa na ataona Wizara ikitekeleza.